Kamati Mapinduzi yaikingia kifua Singida Utd

Muktasari:

  • Singida United imeingia katika mashindano hayo kuchukua nafasi ya timu ya Shaba iliyoondolewa dakika za mwisho

Baada ya uwepo wa sintofahamu ya Singida United kuingizwa katika mashindano ya Mapinduzi Cup kimya kimya, kamati ya mashindano hayo yaibuka na kuweka hadharan ukweli wa tukio hilo.

Msaidizi Katibu wa Mapinduzi Cup, Khamis Shaal alisema kilichofanyika kwa timu ya Singida ni miongoni mwa utaratibu wa kawaida wala kulikuwa hakuna upendeleoa hata kidogo.

Alisema baada ya kamati hiyo kuona kuwa kuna upungufu wa timu moja katika timu shiriki za mashindano hayo walilazimika kukutana ili kuona njia gani wanafanya juu ya kuipata hiyo timu ambayo itaungana na timu zilizoteuliwa awali.

 Alisema kuwa kitu cha kwanza walichokiangaliwa katika uteuzi wa timu moja ni kupitia maombi yaliotumwa na baadhi ya timu ambazo zilionesha nia ya ushiriki ikiwamo Singida United, Polisi Kenya pamoja na Gor Mahiya.

 Alisema baada ya kufanya upembuzi yakinifu kwa timu zote hizo na kubaini kuwa zote zina sifa za kushiriki mashindano hayo, ila kwa wakati huo ililazika muingizwa timu moja tu kama maandalizi ya awali yalivyofanyika.

Shaal alisema kuwa lengo la uongozi wa mashindao hayo ni kuona kila timu iliyoomba ushiriki inapatiwa nafasi ila kutokana na uhaba wa maandalizi ndio maana baadhi ya timu ililazimika kutopatiwa nafasi.