Ubutu wa ushambuliaji Azam wamvuruga kocha

Muktasari:

  • Azam ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2012-13

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche amesema tatizo la timu yake kwa sasa ni washambuliaji, hivyo katika kipindi cha dirisha dogo watahakikisha wanalitatua.

Akizungumza baada ya mchezo wao na Mbao uliomalizika kwa suluhu jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Cheche alisema wanatatizo katika safu ya ushambuliaji.

Alisema kuwa timu inacheza vizuri, lakini shida inajitokeza kwenye umaliziaji, hivyo kipindi cha dirisha dogo wataanza kuziba pengo hilo na kwamba wanahitaji mabao.

“Timu inacheza vizuri,lakini bado tuna tatizo kwenye safu ya ushambuliaji ambayo tunaamini wakati wa dirisha dogo lazima tuanze nalo ili kufikia malengo yetu kwa msimu huu,” alisema Cheche.

Kocha huyo aliongeza kuwa matokeo ya pointi mbili kwenye mechi zao za Kanda ya Ziwa si haba, kwani timu zote zinaonekana kujipanga zaidi.

 Kocha wa Mbao, Ettiene Ndayiragije alisema licha ya sare ya nne mfululizo katika uwanja wa nyumbani siyo tatizo na kwamba vijana wake wanacheza vizuri.

 Alisema kuwa yeye haandai timu kushinda nyumbani, isipokuwa anatengeneza kikosi cha ushindani katika uwanja wowote na kusema kuwa timu yake ya msimu huu ni hatari kuliko hata ya msimu uliopita.

 “Haya matokeo siyo mabaya, hatupambani kushinda nyumbani pekee na ligi haina cha nyumbani wala ugenini,niseme hivi wachezaji wangu wako vizuri na ni tofauti na msimu uliopita,” alisema Mrundi huyo.