Wasanii kujiachia mwisho Aprili 30

Muktasari:

  • Msanii wa bongo fleva, Nickson Saimon ‘Nick wa Pili’ amesema anaunga mkono uamuzi wa Basata na amewataka wasanii kufuata utaratibu.

BARAZA la Sanaa Tanzania (Basata), limewataka wasanii na wadau wa sanaa kulipia vibali vya kusimamia kazi zao kabla ya Aprili 30, mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Basata, Godfrey Mwingereza, Ofisa Habari wa baraza hilo, Agnes Kimwaga amesema mchakato wa kutoa vibali utakwenda sanjari na usajili.

"Zoezi hili ni sehemu ya mkakati wa Serikali katika kurasimisha sekta ya sanaa, Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 inasema ni kosa la jinai wadau wa sanaa kuendesha shughuli zao bila kusajili na kupata kibali hai kutoka Basata,” anasema Agnes.

Ofisa Habari huyo amesema wadau wa sanaa zikiwamo kampuni, taasisi, wamiliki wa kumbi za sanaa na burudani wanaojihusisha

na kazi sanaa wana wajibu wa kulipia vibali hivyo.

Agnes amesema agizo hilo linawahusu wasanii binafsi, vikundi, kwaya, mapromota na bendi za muziki.Ofisa Habari huyo amesema Basata itachukua hatua kwa wahusika ambao watakiuka masharti ya kulipia vibali katika muda uliopangwa.

Msanii wa bongo fleva, Nickson Saimon ‘Nick wa Pili’ amesema anaunga mkono uamuzi wa Basata na amewataka wasanii kufuata utaratibu.