Guardiola ameshindikana England anajipigia tu

Muktasari:

  • Man City imeindeleza rekodi yake ya kutofungwa msimu huu ikiwa inaongoza Ligi Kuu kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Liverpool inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.

HAKUNA namna ya kumzuia Pep Guardiola na Manchester City kwenda kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England kwani, Jose Mourinho aliyekuwa akitegemewa kumdhibiti Mhispaniola huyu ameshindwa kabisa.
Uwezo, mbinu na kasi ya Mourinho kupambana na Guardiola ni kama imefikia mwisho baada ya jana kukubali kipigo cha mabao 3-1 kwenye dimba la Etihad.
Mbali na kuchapwa mabao hayo, lakini bado jeshi la Guardiola likiongozwa na David Silva lilipiga mpira mwingi huku muda mwingi Man United wakiuonekana kucheza kwa kujilinda zaidi.
Iliwachukua Man City dakika 12 tu kuandika bao la kwanza kupitia kwa Silva, ambaye alitumia makosa ya mabeki wa United kushindwa kuondoa mpira uliopigwa na Bernado Silva, ambaye alipokea krosi ya Raheem Sterling.
Katika mchezo huo, Mourinho aliingia uwanjani bila mastaa wake Paul Pogba huku Romelu Lukaku na Alexis Sanchez wakianzia benchi na mashambulizi yake kuongozwa na Marcus Rashford na Anthony Martial huku akijaza viungo wengi eneo la katikati mwa uwanja.
Man City ilimiliki mpira kwa dakika zote 45 za kwanza na kama isingekuwa kukosa umakini kwa mastaa wake akiwemo Sterling, basi zile bao sita kama alizopigwa Shartak Donestic kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, mpaka dakika 45 zinamalizika Man City walikwenda wakiwa kifua mbele kwa bao hilo la Silva. Dakika tatu baada ya kuanza kipindi cha pili, Sergio Aguero ‘Kun’ alipiga msumari wa pili kwenye jeneza la Mourinho akiunganisha kwa shuti kali pasi ya Bernado, ambapo David De Gea aliyekuwa na kazi nzito akishindwa kabisa kuzuia mpira huo.
Bao hilo lilimuasha Mourinho usingizini na kufanya mabadiliko kwa kumtoa Jesse Lingard na kumwingiza Lukaku, ambaye ndani ya sekunde 30 tu alisababisha penalti baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari na kipa wa Man City, Ederson na mwamuzi Anthony Taylor kuamuru ipigwe penalti.
Martial alifunga penalty hiyo dakika 58 na kuonekana kama Man United inaweza kurudia ile came back yake iliyoifanya kwa Juventus kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini haikuwa hivyo kwani, super sub Ilker Gundogan alipiga bao la tatu na kumaliza shughuli.
Kwa ushindi huo, Man City imerejea kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 32 huku Man United ikibaki nafasi ya nane na pointi zake 20.
Awali, Liverpool ambao walidhaniwa kama pumzi imekwisha walichomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham kwenye dimba lake la Anfield na kukaa kileleni mwa msimamo kwa muda.
Mabao mawili ya Mohamed Salah katika kipindi cha kwanza na Xherdan Shaqiri yalitosha kuipeleka Liverpool kileleni kwa muda na kurudisha imani kwa mashabiki wao.
Ushindi huo umeifanya iendelee kuweka rekodi ya kucheza bila ya kufungwa, ambapo kabla ya mechi za jana wao na Chelsea na Manchester City walikuwa bado hawapoteza pambano lolote msimu huu.
Katika pambano la jana, bao la kwanza la Mohamed Salah lilikuwa linamaanisha kwamba staa huyo wa kimataifa wa Misri aliyeanza msimu huu kwa kusuasua alikuwa amefunga mabao 19 dhidi ya wapinzani 21 aliowahi kukumbana nao katika Ligi Kuu ya England.
Ni klabu za Manchester United na Swansea City ndizo ambazo hazijawahi kukumbana na makali ya Salah, ambaye msimu uliopita aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England akiwa na mabao 33 miongoni mwa timu ambazo alicheza nazo.
Salah alifunga bao hilo katika dakika ya 41 ikiwa ni tofauti ya sekunde 14 tu tangu Fulham inyimwe bao lao kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Serbia, Aleksandar Mitrovic ambaye bao lake lilionekana kuwa alifunga akiwa ameotea.
Bao la pili la Liverpool lilifungwa na kiungo wao wa kimataifa wa Uswisi, Shaqiri ambaye anazidi kuibua makali yake. Katika mechi sita zilizopita michuano mbalimbali, Shaqiri aliyenunuliwa kutoka Stoke City katika dirisha kubwa lililopita amehusika kwa mabao matano. Amefunga mawili na kupika matatu.
Chelsea ilijikuta ikibanwa mbavu nyumbani kwake Stamford Bridge na Everton kwa kwenda sare ya bila kufungana huku Arsenal ikipewa kipigo cha bao 1-0 na Wolves.