Sakilu,Ngimba kuipeperusha bendera Hispania

Muktasari:

Tanzania ilipanga kupereka wanariadha wanne katika mbio hizo za dunia

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limemtaja Jackline Sakilu na Ezekiel Ngimba kubeba bendera ya Taifa kwenye mbio za dunia za nusu marathoni zitakazofanyika Alhamisi ijayo nchini Hispania.

Awali RT ilipanga kupeleka nyota nane kwenye mbio hizo za kilomita 21 ambazo zinatanyika kwenye mji wa Valencia, lakini imekwama baada ya wanariadha tisa wa timu ya taifa kukosa ruhusa jeshini.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelim Gidabuday alisema wanapeleka wanariadha wawili pekee kwenye mbio hizo za IAAF kutokana na hali iliyopo ya kunyimwa ruhusa wanariadha wao waliopo JKT akiwamo Alphonce Simbu bingwa wa medali ya shaba ya dunia

 

"Tunaamini Ngimba na Sakilu watatuwakilisha vyema na wote wanaendelea na mazoezi kwenye kambi ya timu ya taifa kule Sakina nje kidogo ya jiji la Arusha," alisema Gidabuday.

Mtendaji huyo wa RT alifafanua kwamba wanariadha hao wataondoka nchini Jumanne ijayo ambapo wataambatana na yeye Gidabuday nchini Hispania.

"Mimi nakwenda kwenye mkutano wa Kamati ya fedha ambapo nimeteuliwa kuwa mjumbe kwa kanda ya tano ambako tuko na wajumbe wengine watatu kutoka Kenya, Sudan na Ethiopia," alisema Gidabuday.