Kagera Sugar yaikamia Makambako FC

Muktasari:

  • Bingwa wa mashindano ya Kombe la FA anakata tiketi ya moja kwa moja kufuzu kwa Kombe la Shirikisho Afrika

Kagera Sugar imeipiga mkwara mzito Makambako FC isitarajie chochote pindi watakapokutana katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho Azam (ASFC).

Timu hizo zitakutana Desemba 21, kwa Kagera Sugar itakuwa nyumbani kuikaribisha timu hiyo ya mkoani Njombe inayoshiriki ligi ya Mkoa.

Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar ‘Wanankurukumbi’, Ally Jangalu alisema wamejiandaa vyema kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kusonga mbele.

Alieleza kuwa licha ya kufahamu wazi kuwapo kwa ushindani kwenye mchezo huo kutokana na wapinzani wao kuhitaji nafasi,watahakikisha hawafanyi uzembe wowote hadi washinde.

“Mchezo utakuwa mgumu, hatuwadharau hata kidogo ni muhimu kwetu kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele,” alisema Jangalau.

Msimu uliopita, Kagera iliondolewa ikiwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani Kaitaba kwa kufungwa bao 1-0 na Mbao FC.