Kocha afichua Morata kutimka Chelsea

Muktasari:

  • Morata amefichua kuwa aliomba kuondoka kiangazi cha mwaka huu akitaka kuelekea kwenye klabu za Italia au kurudi zake Hispania, baada ya kushindwa kufunga mabao ya kutosha katika msimu wake wa kwanza.

Madrid, Hispania. Kocha wa timu ya Taifa ya Hispania, Luis Enrique, amemsababisha mshambuliaji wa Chelsea, Alvaro Morata kufunguka kwa mara ya kwanza, kuhusiana na namna alivyoomba kuondoka timu hiyo kiangazi cha mwaka huu.

Morata amefichua kuwa aliomba kuondoka kiangazi cha mwaka huu akitaka kuelekea kwenye klabu za Italia au kurudi zake Hispania, baada ya kushindwa kufunga mabao ya kutosha katika msimu wake wa kwanza.

Mshambuliaji huyo aliyeandamwa na majeruhi alifunga mabao 15 katika mechi 48 alizocheza huku akionyesha kiwango duni jambo lililomsababisha atemwe kwenye kikosi cha Hispania kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2018 zilizofanyika nchini Russia.

Morata amefichua hayo baada ya Kocha Enrique, kumjumuisha mshambuliaji huyo katika kikosi cha Hispania alichokitangaza kwa ajili ya kuivaa England, Jumamosi hii katikia mashindano mapya ya UEFA Nations League.

"Hakika sikuwa na furaha kabisa Chelsea, katika kipindi cha mwisho cha msimu uliopita, nilifikia uamuzi wa kuondoka Stamford Bridge," alisema Morata.

Hata hivyo alikiri kuwa ujio wa Kocha mpya wa Chelsea, Maurizio Sarri ndio uliomshawishi aamue kubaki na anafurahi  kuona ameaminiwa na kupewa nafasi.

“Kwa sasa ninafuraha sana nimeanza vizuri, sote tuna furaha Chelsea, nilipanga kurudi Hispania au kwenda Italia, natamani kuwa na msimu mzuri tena,” alisema.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid, alisajiliwa na Chelsea kuziba pengo lililoachwa na mhispania mwenzake Diego Costa, aliyeikataa kufanya kazi na Kocha Antonio Conte na kuamua kurudi zake Atletico Madrid.

Mbali ya Morata wachezaji wengine wa Chelsea waliotokea Real Madrid na wapo katika kikosi cha kwanza ni pamoja na kipa Kepa Arrizabalaga, Marcos Alonso na Cesar Azpilicueta.