Kumbe Samatta, Morocco waliwatosa Modric, Salah

Muktasari:

  • Tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa inapatikana kwa kupigiwa kura na makocha na manahodha wa timu za taifa duniani

Dar es Salaam. Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta na kocha Hemed Morocco hawakumpigia kura ya mchezaji bora wa mwaka wa Fifa, Luca Modric wala Mohammed Salah.

Kwa mujibu wa kura zilizopigwa na manahodha na makocha wa kumchagua mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa zimeonyesha Samatta na Morocco hawakumpa chaguo la kwanza Modric huku Salah mwanasoka pekee wa Afrika hawakumchagua kabisa.

Katika upigaji wa kura hizo nahodha wa Stars, Samatta alipiga kura ya kwanza kwa Eden Hazard alimpa pointi 5, Modric (pointi3) na Kylian Mbappe pointi mmoja.

Katika kura ya kocha ya Morocco chaguo lake la kwanza lilikuwa kwa Mbappe pointi 5, Ronaldo (pointi 3) na Modric pointi mmoja.

Kiungo wa Real Madrid na nahodha wa timu ya Taifa ya Croatia, Luka Modric ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani ‘The Best FIFA Men’s Player 2018’.

Modric amemaliza utawala wa miaka kumi mfululizo wa Cristiano Ronaldo aliyekuwa Real Madrid na timu ya Taifa ya Ureno na Lionel Messi wa Barcelona na Argentina ambao ndio pekee waliotwaa tuzo hiyo ya heshima zaidi kwa wanasoka tangu mwaka 2007 hadi 2017 wakibadilishana, kila mmoja akiitwaa mara tano, wawili hao walionekana kugawana karibu nusu nzima ya mashabiki wa soka barani Ulaya.

Kiungo huyo mahiri ameendeleza mafanikio yake kwa msimu huu, baada ya iwezesha Real Madrid kutwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo, pia aliiwezesha Croatia kuandika historia kwa kufika kwa mara ya kwanza katika fainali ya Kombe la Dunia 2018.

Kabla ya kutwaa tuzo hiyo ya Dunia, Modric alitwaa tuzo ya mchezo bora wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Ulaya ‘UEFA Player of the Year’.

Mshambuliaji wa Liverpool na Misri, Mohamed Salah alimaliza nafasi ya tatu akimzidi kidogo Mbappe katika kura hizo baada ya kupata kura 130, nyingi zikitoka katika nchi za Afrika.

Baadhi ya kura zilivyopigwa

Hemed Morocco: Mbappe, Ronaldo na Modric

Mbwana Samatta: Hazard, Modric, Mbappe

Lionel Messi: Modric, Mbappe, Ronaldo

Cristiano Ronaldo: Varane, Modric, Griezmann

Didier Deschamps: Griezmann, Varane, Mbappe

Harry Kane: Ronaldo, Messi, De Bruyne

Gareth Southgate: Modric, Varane, Hazard

Sergio Ramos: Modric, Ronaldo, Messi

Ryan Giggs: Modric, Mbappe, Ronaldo