Ninja, Makambo noma, Yanga yaifanya kitu mbaya Biashara Utd

Muktasari:

  • Yanga na Azam ni timu pekee ambazo hazijapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara

Dar es Salaam. Yanga imerejea kileleni mwa Ligi Kuu Bara kibabe baada ya kutoka nyuma na kuichakaza Biashara United kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 41, na kuishusha Azam yenye pointi 39, huku Simba ikiwa ya tatu na pointi zake 27, na michezo mitatu mkononi.

Shangwe za mashabiki wa Yanga ilibidi kusubiri hadi dakika 70, wakati beki Abdallah Shaibu 'Ninja' aliposawazisha bao kabla ya Heritier Makambo kupachika bao la pili dakika 80, huku bao la kufutia machozi kwa Biashara United likifungwa na Abdulmajid Mangalo katika dakika 37.

Mabadiliko ya kuingia Amiss Tambwe na Pius Buswita yameonekana kubadilishia mchezo kipindi cha pili.

Yanga ambao mbali ya kuonekana kufika langoni mwa Biashara United mara nyingi, lakini walishindwa kupata bao la kusawazisha.

Mara baada ya kuingia kwa Tambwe na Buswita walionekana kushambulia zaidi ya awali na kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Shaibu dakika 70.

Mara baada ya kupata bao hilo mpira ulisimama kutokana kipa wa Biashara, Nouridine Balora kuumia.

Wakati Biashara wakiwa hawaamini kilichotokea Makambo aliiandikia Yanga bao la pili dakika 80 baada ya kuingia ndani ya 18 na kumpiga chenga Abdulmajid Mangalo na kisha alimchungulia kipa Balora wa Biashara mpira na kuweka mpira wavuni.

Biashara katika mchezo huo dhidi ya Yanga katika dakika 45 za mwanzo walionyesha umahiri katika umiliki wa mpira hali ambayo iliwasaidia kutuliza kasi ya Yanga.

Yanga walikuwa wakipeleka mashambulizi kwa kutumia upande wa Haji Mwinyi, ambaye mara kwa mara alikuwa akipiga krosi lakini Makambo alikuwa haonyeshi utulivu katika umaliziaji.

Dakika 37, Biashara United wanapata bao kupitia kwa Mangalo baada ya kupigiwa pasi katikati ya uwanja na Lambele Jerome na kuchomoka na mpira mpaka anaingia ndani ya 18 na kupiga shuti kali lililomshinda Ramadhan Kabwili.

Dakika 51, Biashara United wanafanya mabadiliko kwa kumtoa George Makang'a na kuingia Mpapi Nassib, na Godfrey Mapunda na kuingia Kauswa Benard.

Wakati kocha wa Biashara akioneka kuridhika na matokeo na kuwaingiza wachezaji kwa ajili ya kujilinda mwenzake Mwinyi Zahera wa Yanga aliingiza wachezaji wa kushambulia zaidi.

Zahera alimtoa Raphael Daud aliyeonekana akitoka akichechemea na kuingia Papy Tshishimbi na Thaban Kamusoko na kuingia Amis Tambwe katika dakika 56, pia alimtoa Feisal Salum na kuingia Pius Buswita kuingia kwa wachezaji hao kulibadilisha hali ya mchezo kwa Yanga na kuanza kulisakama zaidi lango la Biashara.

Dakika 68 Makambo alipenyezewa pasi na Jaffary Mohammed na kukutanayo ndani ya 18, lakini alipoucheza mpira alipaisha na kuikosesha goli Yanga

Dakika 70, Abdallah Shaibu 'Ninja' anaipatia bao la kusawazisha Yanga baada ya kuucheza mpira ndani ya 18 akiwekeana kigingi na kipa wa Biashra Utd, Nouridine Balora.

Makambo anaiandikia Yanga bao dakika 80 baada ya kuingia ndani ya 18 na kumpiga chenga Abdulmajid Mangalo na kisha alimchungulia kipa wa Biashara mpira na kuweka mpira wavuni.