Beki wa Yanga aanza kukimbia Z’bar

Muktasari:

Beki huyo alikuwa moja wa majeruhi tisa walio katika kikosi cha Yanga kwa sasa

Dar es Salaam. Beki wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' ameanza mazoezi mepesi baada ya kutolewa plasta ngumu ‘P.O.P.’ katika mguu wake.

Ninja alisema baada ya kugundulika kuvunjika sehemu ya mfupa katika kifundo chake cha mguu wa kushoto aliwekewa plasta ngumu kuweza kuunga sehemu hiyo ambayo tayari imetolewa Februari 15 wiki iliyopita.

Beki huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea Taifa ya Jang'ombe ya Zanzibar alisema ameanza mazoezi mepesi kisiwani huko akianza kukimbia taratibu.

Alisema kwa sasa sihisi tena maumivu katika jeraha hilo ambapo ataendelea kujifua taratibu kurudisha ubora wake mpaka hapo daktari atakapomruhusu kufanya mazoezi makali.

"Nashukuru Mungu Alhamisi iliyopita nilitoa ile P.O.P na baada ya kutoa niliambiwa nitembee taratibu na sikuwa nahisi tena yale maumivu kama awali,"amesema Ninja.

"Nimemaliza hatua ya kutembea na sasa nimeanza kukimbia taratibu ufukweni najisikia niko sawa,naamini nitarudi katia hali yangu ya awali niweze kuisaidia timu yangu."