Owen ampa Lukaku bao za kutosha

Muktasari:

Lakini, gwiji huyo wa England ametia shaka pia kama straika huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 75 milioni ataruhusiwa kufunga kirahisi sambamba na washambuliaji wenzake kwenye kikosi cha Manchester United.

MANCHESTER, ENGLAND. Mshambuliaji wa zamani Manchester United, Michael Owen anamtabilia Romelu Lukaku atafunga mabao 25 katika Ligi Kuu England msimu huu.
Lakini, gwiji huyo wa England ametia shaka pia kama straika huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 75 milioni ataruhusiwa kufunga kirahisi sambamba na washambuliaji wenzake kwenye kikosi cha Manchester United.
Lukaku hajaonja utamu wa kufunga bao kwa mechi saba sasa kwenye klabu yake ya Man United baada ya kufunga mara 11 katika mechi 10 za kwanza kwenye timu hiyo tangu alipojiunga nayo akitokea Everton katika dirisha lililopita la usajili. Wiki iliyomalizika, aliweka rekodi Ubelgiji kwa kuwa kinara wa mabao wa muda wote akifikisha mabao 31 huku akiwa na umri wa miaka 24 tu.
Lakini, Owen, ambaye pia aliwahi kuichezea Man United anaamini Lukaku atazinduka upya na kuanza kupiga mabao.
Owen alisema: “Atafunga kuanzia mabao 25 na kuendelea. Nina hakika atafanya hivyo. Nadhani ni tatizo dogo tu kutokufunga na amekuwa na rekodi nzuri kwenye mechi dhidi ya Newcastle."
Man United leo Jumamosi itakipiga na Newcastle United kwenye Uwanja wa Old Trafford na hilo linatajwa kwamba, ni wakati mwafaka kwa staa huyo kuanza kufunga tena. Man United inahitaji kweli kweli mabao ya Lukaku ili kukimbizana na mahasimu wao Manchester City, ambao wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi nane dhdi yao.