Makocha hao wameanza kusaka wachezaji wa kujenga vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao

Muktasari:

  • Makocha hao wameanza kusaka wachezaji wa kujenga vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao 

LIVERPOOL, ENGLAND. Liverpool na Arsenal zimeingia vitani kuwania saini ya mchezaji wa AS Monaco, Thomas Lemar mwishoni wa msimu huu.

Taarifa zinaweka wazi kwamba makocha wa timu hizo mbili, Jurgen Klopp na Arsene Wenger wote wana fedha za kufanya usajili wakati dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa na kwamba, kila mmoja ametenga Pauni 90 milioni kuinasa huduma ya staa huyo wa Ufaransa.

Liverpool na Arsenal zote zimeondokewa na mastaa wake wa maana katika dirisha hili la usajili, ambapo Philippe Coutinho ameachana na wababe hao wa Anfield akitimkia Barcelona, wakati Alexis Sanchez aliondoka Emirates kwenda Manchester United. Kuna mastaa wengi wanaosakwa na makocha hao, lakini vita inaripotiwa kwamba, itakuwa kali kwelikweli kwa Lemar.

Hata hivyo, Arsenal na Liverpool si wao tu watakaoitaka huduma ya Lemar baada ya Manchester City nao kutajwa kwenye vita kutokana na kumkosa Sanchez, huku matajiri wa Paris, PSG wakimweka kwenye mipango yao ya msimu ujao Mfaransa huyo.

Wenger alikaribia kumnasa Lemar katika dirisha lililopita baada ya kukubali kulipa Pauni 92 milioni, lakini staa huyo mwenyewe aligoma kuihama Monaco katika dakika za mwisho na kubaki katika timu hiyo ya huko kwenye Ligue 1.