Yanga yapangua mtego wa kwanza

Muktasari:

  • Yanga haijawahi kutolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na timu za kutoka visiwani

Yanga imelazimika kubadilisha hoteli waliyopanga kupikia chakula cha wachezaji wake baada ya kubaini mmoja wa viongozi wa St.Louis ni wammiliki wa hoteli hiyo.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanajiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya St Louis keshokutwa Jumatano wakiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 waliopata nyumbani.

Awali Yanga ilipanga kuwatumia wapishi wawili maalum ambao ni vijana wa Kitanzania waishio Shelisheli kuwapikia chakula katika hoteli wanayofanyia kazi na kisha kukipeleka mahali ambako timu imefikia ili kukwepa hujuma.

Hata hivyo, viongozi wa Yanga wakiongozwa na Katibu wa Kamati ya Mashindano, Samuel Lukumay na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika walishtukia kwamba mahali walikopanga kupikia chakula pana uhusiano wa karibu na viongozi wa Louis jambo lililofanya waachane napo.

"Kuna mahali ambako tulipanga kupatumia kwa ajili ya kupikia chakula cha timu, lakini tumekuja kufahamu kwamba panamilikiwa na kiongozi wa St. Louis.

“Hivyo tumeona wanaweza kutumia mwanya huo ili kutuhujumu hivyo uamuzi tulioufikia ni kuachana napo na sasa tunaangalia mahali kwingine," alisema Lukumay.