Mpira wa kikapu umepotea, waje wa kuufufua

Muktasari:

Soka itabaki kuwa namba moja kupendwa na mashabiki, lakini mpira wa kikapu ulitoa presha kubwa kulinganisha na michezo mingine.

Vuta hisia huku ukirudisha nyuma takribani miaka 15 iliyopita mchezo wa mpira wa kikapu nchini ulivyokuwa ukishindana na soka kwa umaarufu.

Soka itabaki kuwa namba moja kupendwa na mashabiki, lakini mpira wa kikapu ulitoa presha kubwa kulinganisha na michezo mingine.

Mpira wa kikapu uliitangaza Tanzania kimataifa kutokana na ubora wa wachezaji wetu ambao walitamba kwa mchezo mzuri na baadhi yao walipata fursa ya kwenda kucheza nje ya nchi.

Katika miaka ya 1990 hadi 2000 mpira wa kikapu ulikuwa sehemu ya maisha ya vijana wengi hususani Mkoa wa Dar es Salaam uliokuwa umesheheni wachezaji nyota.

Nimeitaja Dar es Salaam kwa sababu ilikuwa kitovu cha mchezo huo ingawa ipo baadhi ya mikoa ilifanya vyema katika mchezo huo kama Morogoro, Mwanza, Zanzibar, Tanga na Tabora.

Bila shaka wengi tunakumbuka enzi za Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (DARBA), kilichokuwa chini ya mwenyekiti Simon Msofe na katibu mkuu wake, Mbamba Uswege.

Vigogo hawa watabaki kwenye kumbukumbu ya familia ya mpira wa kikapu kwa mchango mkubwa waliotoa katika uongozi wao.

Mbamba alikuwa ndiye mwenye mpira wa kikapu Dar es Salaam na kifo chake kimechangia kushusha ari ya mchezo huo ambao kwa sasa umepoteza dira.

Mbamba alikuwa mhimili wa mpira wa kikapu na wengi tunakumbuka Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) ilivyokuwa na ushindani wa aina yake kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Sipati picha shamrashamra zilizokuwa zikipambwa na wasanii nyota wa bongo fleva zilivyonogesha ligi hiyo huku mashabiki lukuki wakifurika uwanjani na wengine kulazimika kusimama au kubaki nje.

Udhamini mnono wa baadhi ya kampuni kubwa nchini ulichagiza ukuaji wa mpira wa kikapu uliowaibua wachezaji nyota kutoka kila pembe ya Dar es Salaam.

Vijana wengi kutoka maeneo ya Upanga, Chang’ombe na sehemu nyingine za Dar es Salaam waliufanya mpira wa kikapu kuwa sehemu ya maisha yao.

Wengi tunamkumbuka ‘fundi’ Abdallah Ramadhani “Dulla” aliyetamba na timu ya Vijana “City Bulls” akiwa mchezaji bora wa aina yake kuwa kutokea nchini.

Dulla jina lililokuwa maarufu enzi zake, alikuwa MVP wa ukweli katika kikapu na vijana wengi wa wakati huo wana kumbukumbu nzuri ya vitu vyake uwanjani.

Mbali na Dulla wapo baadhi ya nyota waliotamba na klabu tofauti akiwemo aliyekuwa nahodha wa muda mrefu wa JKT na timu ya taifa, Franklin Mbwatila Simkoko.

Pia walikuwepo mastaa wengine kina Frank Bategeki, Michael Mwita, Ally Dibo, Adam Jegame, Michael Casmir, Juma Kisoky, Frank Kusiga, Haleluya Kavalambi, Shisrya Mwiki, Bahati Mgunda, Patrick Nyembela, Shaaban Kayumba ‘Shabobo’ na wengine wengi tu waliotamba.

Baada ya kizazi cha kina Dulla aliyewahi kucheza mpira wa kulipwa Uganda, hakuna mchezaji mwenye jina anayetamba hivi sasa.

Hakuna tena ushindani wa watani wa jadi Pazi na Vijana. Enzi zile, zikicheza timu hizo Dar yote inatikisika na Uwanja wa Ndani wa Taifa unakosa nafasi. Pia hatuzioni tena Savio, Oilers, Chang’ombe Boys, JKT na Don Bosco zile zilizotamba enzi hizo.

Bila shaka kuzorota kwa mpira wa kikapu kumechangiwa na viongozi wa vyama husika, kama Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kukosa dira ya maendeleo.

Tatizo la viongozi wa vyama vya michezo kushindwa kupata mafanikio ni kipaumbele chao cha kwanza kuwa ni kujinufaisha wanapoingia madarakani.

Ni viongozi wachache wenye dhamira ya dhati ‘wanaoumwa’ na maendeleo ya michezo nchini ambao pia wameshindwa kutimiza ndoto zao kwa sababu ya kufanyiwa figisu na baadhi ya vigogo wasiopenda maendeleo.

Kama Mbamba aliutangaza mpira wa kikapu kwanini viongozi wa sasa wanashindwa. Hapa kuna tatizo.

Uchaguzi wa TBF utafanyika Desemba 29 na 30 mwezi ujao, hivyo ni fursa nzuri ya kupata viongozi bora wenye uchungu na mpira wa kikapu ambao watafuata nyayo za kina Mbamba.

Wengi watajitokeza kuomba ridhaa ya kuchaguliwa lakini wapiga kura ndiyo wenye dhamana ya kuchagua kiongozi bora atakayeleta maendeleo.

Wakati umefika TBF kuongozwa na watu wenye weledi na dhamira ya dhati ya kurejesha mpira wa kikapu katika makali ya miaka 1990. Wapigakura watafanya kosa kubwa endapo watachagua viongozi kwa kuangalia sura kwasababu watawaumiza Watanzania ambao wana kiu ya kuona mabadiliko katika taasisi hiyo.

Mpira wa kikapu unahitaji viongozi makini wenye uzalendo, hivyo ninashauri wapigakura watumie busara kuchagua viongozi makini wenye mwelekeo chanya