Ni vizuri kuepuka siasa katika shughuli za Serikali

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Kila anapopata nafasi, hasa katika mikutano ya hadhara amekuwa akihimiza kila Mtanzania bila kujali rangi, dini, kabila wala chama, kulipa kodi na kushiriki katika shughuli za maendeleo bila ya kujali tofauti hizo.

Rais John Magufuli amekuwa mwalimu mzuri wa somo la uraia nchini akifundisha kwa lugha ya msisitizo mada kuhusu umuhimu wa kila mwananchi kulipa kodi na kwamba maendeleo hayana itikadi za vyama.

Kila anapopata nafasi, hasa katika mikutano ya hadhara amekuwa akihimiza kila Mtanzania bila kujali rangi, dini, kabila wala chama, kulipa kodi na kushiriki katika shughuli za maendeleo bila ya kujali tofauti hizo.

Pia, amekuwa akifafanua kwamba kodi inayolipwa na kila Mtanzania ndiyo inatumika katika uendeshaji wa Serikali na ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo haina chama.

Tukirejea namna Watanzania walivyojitokeza kusimama katika mistari mirefu kulipa kodi ya majengo ni ushahidi kwamba somo hilo lilieleweka vizuri na kwa nia njema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyopewa jukumu la kukusanya kodi hiyo iliamua kuongeza muda kuwezesha kila mmoja kutimiza wajibu huo.

Tunampongeza Rais kwa uelimishaji na tunamuunga mkono kwa kuwa barabara, shule au hospitali zikijengwa hutoa huduma kwa Watanzania wote.

Hata hivyo, ili mada kwamba “maendeleo hayana chama” iweze kueleweka vizuri, viongozi wa Serikali ambao wanatokana na chama wanatakiwa kujitahidi kutochanganya shughuli za Serikali na shughuli za kisiasa.

Kati ya mwaka 1965 na 1991 wakati Tanzania ilipokuwa inafuata mfumo wa chama kimoja, ilikuwa kawaida kuona viongozi wa Serikali wakishika pia madaraka katika chama na hivyo, shughuli za Serikali zilichanganywa na shughuli za chama.

Maeneo yote ya kazi – viwandani, ofisini, jeshini, shuleni, mahakamani na kwingineko – yalikuwa na ofisi za matawi chama.

Baada ya Katiba ya mwaka 1977 kufanyiwa marekebisho na kurejesha mfumo wa vyama vingi, wazee waliona busara kuondoa siasa katika maeneo hayo. Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 1995 iliharamisha siasa katika maeneo ya Serikali, kama ofisi za wizara, wilaya, mikoa, majeshi ya Ulinzi na Usalama, mahakamani, shuleni na vyuoni.

Halafu, kwa kuzingatia umoja wa kitaifa na kujenga uwajibikaji zaidi, sheria hiyo ikazuia wanajeshi, majaji, walimu, makamishna wa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na wengine wenye wajibu wa kutoa haki, kujihusisha na siasa.

Maadamu katazo hilo ni la kisheria ni vizuri utekelezwaji wake ukaendelea kuzingatiwa kikamilifu.

Tunasema haya kwa kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita katikati ya sherehe za kuwatunukia kamisheni askari waliohitimu mafunzo, shughuli za kisiasa ziliibuka.

Wakati akiendelea na hotuba yake, Rais Magufuli alidokezwa na kiongozi mmoja wa CCM kuwa kuna watu walitaka kujiunga na chama hicho kwa kutumia mkutano huo.

Japo Rais Magufuli alijaribu kutoa nafasi pia kwa viongozi wa upinzani kutumia mkutano huo kukaribisha wanachama wapya, ni wazi kuwa siasa ilishapenyezwa katika shughuli hiyo na hivyo isingekuwa rahisi kuzuia lawama, manung’uniko na mashambulizi kutoka vyama vilivyochukulia shughuli hiyo kuwa ya kiserikali tu.

Kama ilivyotarajiwa, kila mwanasiasa ameibuka na tafsiri yake kuhusu kitendo hicho na kuondoa dhana nzima ya shughuli hiyo. Shughuli za siasa zina viwanja vyake na hivyo viongozi wajiepusha kuchanganya mambo hayo na shughuli za Serikali.