Njombe choo bora kwanza, nyumba baadaye

Muktasari:

Uzuri wa shule hiyo unakamilika pale ninapoamua kwenda maliwatoni ambako nakuta vyoo safi vya wanafunzi vyenye matundu 17; wasichana wakitumia tisa na wavulana manane.

 

Ni asubuhi  tulivu ya kipupwe, naingia Shule ya Msingi Welela na macho yangu yanavutiwa na mazingira safi yenye kuvutia, ikiwamo ramani ya dunia iliyotengenezwa kwa chupa za plastiki zenye rangi ya kijani.


Uzuri wa shule hiyo unakamilika pale ninapoamua kwenda maliwatoni ambako nakuta vyoo safi vya wanafunzi vyenye matundu 17; wasichana wakitumia tisa na wavulana manane.

Maliwato haya yana sehemu ya kunawa mikono yakiwa na maji yachuruzikayo yakiwa na uwezo wa kuhudumia watoto 14 kwa wakati mmoja. Kuna sabuni ya maji kwenye tanki lenye ukubwa wa lita 1,500.

Kwa miundombinu hiyo, magonjwa yamepungua shuleni hapo. Ayubu Kidagayo, mwanafunzi wa darasa la sita anakiri hilo.

“Zamani homa za matumbo na kuhara ilikuwa ni jambo la kawaida lakini sasa ni historia. Hatuendi tena mashambani au msituni kujisaidia,” anasema mwanafunzi huyo.

Mafanikio hayo hayakupatikana bure, kuna juhudi ziliwekwa. Kampeni ya afya na usafi wa mazingira imeleta mabadiliko hayo, siyo kwa shule hiyo pekee bali kijiji kizima cha Welela chenye kaya 295.

Mafanikio haya yamepatikana muda mrefu kidogo na inaelezwa kuwa hadi Novemba 2015, kaya zote kijijini hapo zilikuwa na vyoo bora vyenye kuta imara, paa lisilovuja, mlango unaofungika, sakafu inayosafishika kwa maji na kibuyu chirizi chenye majisafi na sabuni kwa ajili ya kunawa mikono. Kabla ya hapo, kumbukumbu zinasema ni kaya nne pekee zilizokuwa na vyoo bora.

Baada ya kukamilisha awamu ya kwanza, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Welela, Thomas Mwinami anasema, Januari 2016 tuliingia katika mpango wa utekelezaji wa awamu ya pili kwa kubainisha sifa hizo.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Sovi, Mariam Mbwambo anasema wamefanikiwa kujenga vyoo bora kanisani, ofisi ya kijiji na Kituo cha Afya cha Sovi.

Anasema kaya 202 zenye wakazi 743 zina vyoo bora na kwamba kampeni ya afya ya usafi na mazingira ni agenda endelevu katika mikutano na mikusanyiko mbalimbali.

“Tumefanikiwa kuwa washindi wa tatu Tanzania bara kwa utekelezaji wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira mwaka 2016 na tukazawadiwa pikipiki kwa ajili ya kutekeleza kampeni hii,” anasema Mbwambo.

Katika Kijiji cha Maduma kilichopo Kata ya Kichiwa, hakuna mwananchi anayeruhusiwa kuanza kujenga makazi mapya kabla hajajenga choo bora na cha kisasa chenye sifa zote.

Mikakati na mbinu za utekelezaji inatofautiana baina ya vijiji. Kijiji cha Lyalalo kilichopo Kata ya Matembwe hufanya vikao vya kamati ya kuhakiki ujenzi wa vyoo. Vijiji vya Kanikelele, Isoliwaya, Ikuna na Image licha ya kuwa na vyoo bora shuleni, kanisani, vilabu vya pombe na maeneo yenye mikusanyiko kama vile zahanati, wamefanikiwa kuwa na vyoo bora kwa asilimia 100.

Uwapo wa mradi wa maji unaohudumia vitongoji sita katika Kijiji cha Image umeifanya kampeni hiyo kutekelezeka kwa wakati kutokana na maji hayo kutumika katika ujenzi wa vyoo na katika usafi na mazingira kwa ujumla.

Bibi Anjelika Lihawa (88), ambaye ni mjane, mkazi wa Kijiji cha Image tayari ana choo bora.

“Zamani nilikuwa na choo cha shimo, lakini kwa sasa nimefanikiwa kujenga cha kisasa zaidi,” anasema.

Malengo ya Milenia ya 2025

Utamaduni wa usafi wa mazingira umekuwa ni maisha ya kila siku ya wakazi wa Wilaya ya Njombe ambayo inaongoza kwa vyoo bora kati ya halmashauri zote 184 Tanzania, hivyo kuing’arisha nchi Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Valentino Hongoli anasema siri ya mafanikio ni kuwa na malengo katika sekta ya afya na mazingira.

Anasema wataalamu walianza kufanya utafiti uliogundua kulikuwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na baadhi ya maeneo kutokuwa na usafi wa kutosha.

“Tulianza ngazi za vijiji ili kutokomeza magonjwa haya katika kuboresha usafi wa mazingira. Ilitolewa elimu ambayo wananchi wanaizingatia na kila mmoja kuagizwa kutekeleza mkakati uliopo. Mikutano iliitishwa kupitia uongozi wa vijiji,” anasema Hongoli.

Mratibu wa kampeni ya usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima anasema kampeni hiyo ilianzishwa mwaka 2012 na inatekelezwa katika halmashauri zote nchini.

Anasema hadi sasa wizara imezifikia halmashauri 184 na vijiji 12,500 na kuhamasisha jamii kuhusu ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika kaya na maeneo yenye mikusanyiko.

Mwakitalima anasema awamu ya kwanza ilianza mwaka 2012 na kukamilika Juni mwaka jana na ya pili inatekelezwa kuanzia mwaka 2016 na kutarajiwa kukamiliaka mwaka 2021.

Anasema wakati kampeni hiyo inaanza, ni asilimia 19 pekee ya kaya nchini zilikuwa na vyoo bora lakini hadi Juni 2016 tathmini ilionesha zimepanda mpaka asilimia 62 na unawaji mikono ilikuwa asilimia 5.9 na imefika asilimia 43 katika vijiji vilivyokuwa vinatekeleza kampeni hiyo.

Kwa shule za msingi na sekondari, anasema awamu ya kwanza vyoo vya kisasa ilijengwa kwenye shule 2,113; lakini awamu ya pili, wigo utapanuliwa zaidi.

“Tunataka tuzifikie zaidi ya kaya milioni 5.6; kaya milioni 3.8 za vijijini na milioni 1.8 za mjini. Hii itaenda sambamba na shule 3,500 za msingi na 700 za sekondari,” anasema Mwakitalima.

Anafafanua kuwa awamu ya pili itajumuisha zahanati 1,000 ili kukidhi haja za wagonjwa, wasindikizaji, watoa huduma na katika barabara kuu ambako abiria husimama kuchimba dawa.

“Tumepanga kujenga vyoo bora maeneo nane ya kimkakati katika barabara mbalimbali, kufika mwaka 2025 tunataka tuwe na Tanzania safi na kila kaya nchini itakuwa na choo bora,” anasema Mwakitalima.

Mratibu wa huduma za maji, afya na mazingira shuleni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mwalimu Theresia Kuiwite anasema Wilaya ya Njombe imekuwa mfano wa kuigwa baada ya vikao kati ya viongozi, walimu na wanavijiji kuongeza uhamasishaji.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri anasema ikilinganishwa na wilaya nyingine alizowahi kufanya kazi, amejifunza uongozi wa ushirikiano kutoka ngazi za juu kwenda kwa wananchi wa kawaida.

“Watu wa Njombe wana wivu wa maendeleo na hiyo imekuwa chachu katika kuharakisha mipango iliyowekwa na hawapendi kusukumwa. Tayari kata zote 24,211 zina vyoo bora,” anasema Ruth.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka anawataka wakuu wa mikoa nchini kuiga mfano wa mkoa wake katika utunzaji wa mazingira

Anasema mafanikio hayo hayakushuka kama mvua, bali kulikuwa na mshikamano baina ya viongozi wa mkoa, wilaya mpaka kata, vitongoji na wananchi wa kawaida.

“Mafanikio ya mkoa wetu yanatokana na utashi wa viongozi na utayari katika kutekeleza majukumu yao. Kujipanga na nguvukazi ya pamoja ndiyo msingi wa mafanikio tuliyonayo,” anasema Ole Sendeka.

Njombe ambayo mwaka jana ilikuwa wilaya bora kwa usafi wa mazingira, ujenzi wa vyoo bora na matumizi kwa asilimia 97 bado ni safi.