Polisi Tanga wameanza, tunasubiri wengine

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika gazeti hili toleo la jana, mbali ya waendesha bodaboda hao, hata abiria wasiovaa kofia ngumu (helmet) nao wameanza kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutozingatia usalama barabarani wakiwa wamepanda pikipiki.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeanza kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani vinavyofanywa na waendesha pikipiki ambao ni maarufu kwa jina la bodaboda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika gazeti hili toleo la jana, mbali ya waendesha bodaboda hao, hata abiria wasiovaa kofia ngumu (helmet) nao wameanza kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutozingatia usalama barabarani wakiwa wamepanda pikipiki.

Habari hiyo imeeleza kuwa jumla ya abiria 20 wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani huku waendesha bodaboda 152 wakishikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na makosa mbalimbali ikiwamo kutokuwa na leseni na bima na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alikaririwa akisema, “Operesheni hii haitawaacha salama wasiofuata sheria barabarani,” na amewaonya abiria wasikimbilie kupanda bodaboda bila kuvaa kofia.

Tunapongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na polisi mkoani Tanga dhidi ya waendesha bodaboda. Kero, vilio na malalamiko ya wananchi dhidi ya watoa huduma hii ya usafiri yamekuwa ya muda mrefu na mara zote tumekuwa tukisikia kauli za onyo na ahadi za “tutawachukulia hatua kali za kisheria” bila kuona utekelezaji wake kwa vitendo.

Kauli ya kuwashughulikia waendesha bodaboda wakaidi iliwahi kutolewa na aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu akiwataka makamanda wa polisi kote nchini kuendesha operesheni kali ya kuwachukulia hatua kali za kisheria waendesha pikipiki wasiotii sheria za usalama barabarani ikiwamo kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu pamoja na kutovaa kofia ngumu.

Alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila kamanda ahakikishe kuwa wale wote wasiofuata sheria na kukaidi wanakamatwa bila kuoneana muhali kwakuwa wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.

“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha operesheni kali dhidi ya bodaboda ili kupunguza ajali zinazosababishwa na bodaboda ambao wengi wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria tu,” alisema Mangu lakini hadi anampisha Simon Sirro hakuna operesheni yoyote iliyofanywa kuwadhibiti madereva hao wa pikipiki.

Mei 31, siku mbili baada ya kuapishwa kuliongoza Jeshi la Polisi, Kamanda Sirro pia alisikika akitoa ahadi ya kuwashughulikia bodaboda wasiotii sheria za usalama barabarani na wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwamo uporaji na ujambazi kwa kutumia mwamvuli wa biashara ya kusafirisha abiria. Aliwaagiza makamanda wote wa mikoa kuwashughulikia wote wanaofanya vitendo hivyo.

Tunaamini kazi ya Jeshi la Polisi ya kulinda raia na mali zao itatekelezwa kikamilifu kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu ambazo Taifa limejiwekea zinafuatwa kikamilifu. Tunapenda kuwakumbusha polisi nchini kuhakikisha kwamba vijana hawa wa bodaboda wanaangaliwa kwa macho mawili.

Jicho la kwanza, tunataka liangalie mafunzo stahiki siyo ya udereva tu wa pikipiki , bali hata namna ya kuwahudumia wateja (customer care). Wajue wajibu wao wakiwa barabarani na pia kuhakikisha abiria wao wanapata huduma bora na kwa usalama kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Jicho la pili, tunataka Jeshi la Polisi lisimamie utekelezaji wajibu wa madereva hao ili kupunguza ajali na kukomesha uhalifu kupitia kwa kutumia aina hiyo ya usafiri. Ndiyo maana tunasema Tanga wameanza, wengine wanangoja nini?