Rais Mkapa amenena, tumuunge mkono

Rais mstaafu Benjamin Mkapa

Muktasari:

  • Pia, ameshauri uitishwe mdahalo wa wazi utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyeongoza Serikali ya awamu ya tatu, amekuwa kiongozi wa kwanza aliyeshika madaraka ya nchi kuvunja ukimya na kueleza bayana kwamba kuna mushkeli katika elimu nchini.

Pia, ameshauri uitishwe mdahalo wa wazi utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Mkapa anaamini kuna janga katika elimu kutokana na anayoyasoma kwenye magazeti, maoni anayopelekewa na sekta binafsi, walimu, vyuo vikuu binafsi na pia anapata minong’ono kutoka vyuo vya umma kwamba kuna janga katika elimu.

Licha ya Mkapa, siku za nyuma enzi za utawala wa awamu ya nne, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipaza sauti kuiomba Serikali iliyokuwa madarakani kuunda kamati maalumu ya wataalamu kwa ajili ya kuifanyia marekebisho sekta ya elimu nchini kwa maelezo kuwa viongozi katika wizara ya elimu wameshindwa kazi.

Msingi wa hoja ya Mbatia ulitokana na ufaulu duni wa matokeo ya kidato cha nne aliyoyaita ni maafa na janga kwa taifa. Mfano halisi wa janga la elimu ni malalamiko yaliyoripotiwa katika gazeti hili toleo la Januari 30, 2012 na mkazi wa Kijiji cha Mohoro wilayani Rufiji, Saidi Makwangu akihoji kuhusu mwanaye kufaulu mtihani wa darasa la saba wakati hajui kusoma wala kuandika.

Hoja ya Mkapa haifai kubezwa wala kupuuzwa hasa ukitilia maanani usemi wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela kwamba elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, mtoto wa kibarua wa mgodini anaweza kuwa mkuu wa mgodi na mtoto wa kibarua wa shambani anaweza kuwa Rais wa nchi. Kauli ya Mandela inatukumbusha usemi uliotamba sana kwa wanasiasa wa hapa nchini miaka ya nyuma kwamba ‘vijana ni taifa la kesho’ , kwa maana hiyo vijana hawa wanatakiwa kupewa elimu itakayokuwa chanzo cha wao kuwa na uwezo, maarifa, ujuzi na kupata mabadiliko yatakayotokana na mafunzo waliyoyapata.

Hivyo, Mkapa ameona mbali kwamba janga la elimu linaloelekea kuota mizizi katika nchi yetu hatuna budi kuanza kulichukulia hatua sasa, mjadala alioshauri unapaswa kuitishwa haraka kwa kuwa kuzidi kuchelewa taifa linazidi kuangamia.

Ni ukweli usiofichika kwamba sekta ya elimu ina changamoto nyingi zikiwamo lugha ya kufundishia ambayo kwa shule za msingi ni Kiswahili na sekondari ni Kiingereza, hivyo wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wanapata kikwazo wanapokutana na lugha ya Kiingereza.

Pia, uhaba wa walimu hasa wa masomo ya hisabati na sayansi, uwezo mdogo wa baadhi ya walimu na motisha ndogo ni miongoni mwa mambo yanayochangia washindwe kuwasaidia watoto kwa viwango tarajiwa.

Tunaunga mkono juhudi za Serikali za kutoa elimu bure, ujenzi wa vyumba vya madarasa na utengenezaji wa madawati ya kutosha, lakini kama ilivyowahi kuelezwa na baadhi ya wadau wa elimu kwamba umuhimu wa kwanza katika elimu ni walimu, vitabu na kwa sayansi ni maabara.

Hivyo, wakati tukiendelea kusubiri utekelezaji wa ushauri uliotolewa na Mkapa ni vema hoja zetu tukazielekeza zaidi katika kupata dira ya elimu iliyo bora na kutoigeuza elimu mtaji wa kisiasa. Pia, tunamshauri waziri mwenye dhamana na elimu kuupokea kwa mikono miwili ushauri wa Mkapa.