Saccos zijiendeshe tofauti kuwakomboa wanachama wake

Muktasari:

  • Linapokuja suala hilo, kila mmoja ana uwezo tofauti na mwenzake. Hii ni sehemu ambayo kila mmoja hujitofautisha na kufahamu anatokaje eneo alipo ili kufanikisha mipango yake.

Kutokana na ongezeko la mahitaji kila mwananchi anawaza namna ya kujinasua kiuchumi.

Linapokuja suala hilo, kila mmoja ana uwezo tofauti na mwenzake. Hii ni sehemu ambayo kila mmoja hujitofautisha na kufahamu anatokaje eneo alipo ili kufanikisha mipango yake.

Tunazo taasisi za fedha na benki za biashara ambazo huduma zake ni muhimu ingawa bado zinawafikia wachache sana.

Tanzania ina wananchi wengi ambao ni maskini wanaohitaji mikopo midogo midogo kuanzisha na kuendeleza biashara kabla hawajaanza kukopa kiasi kikubwa cha kukuza miradi yao.

Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) ni suluhisho la uhakika kwa watu wengi wenye kipato cha chini, hivyo zinatakiwa kuwa na mipango ya kuwawezesha wanachama wake.

Licha ya umuhimu wake katika kuwakomboa wananchi kiuchumi, saccos nyingi nchini zimedumaa kwa kukosa mipango endelevu na ari ya ushindani na taasisi za fedha.

Udumavu huu unatokana na changamoto zinazovikabili vyama vya kuweka na kukopa (saccos) hivyo kutowanufaisha wanachama kwa kiwango kilichotarajiwa.

Ili kuwanufaisha wananchi wanaokubaliana na mfumo huu, ipo haja kwa taasisi hizi kuchukua hatua stahiki kushughulikia changamoto hizo kwa wakati.

Kutokuwa na ubunifu kwenye bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi hizi ni miongoni mwa changamoto zinadhorotesha ufanisi wake. Huduma za kuweka na kukopa zilizopo ni za kizamani zisizoendana na mahitaji ya wateja au spidi ya mabadiliko ya sayansi ya teknolojia.

Huduma hizi hazifanyiwi uboreshaji hivyo kuzifanya ziendelee kuwa duni kukidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa.

Kutokuwa na wataalamu wa asasi ndogo za fedha ni changamoto nyingine inayohitaji kufanyiwa kazi. Ukosefu wa rasilimali watu wenye sifa na vigezo stahiki unadumaza saccos nchini.

Taasisi hizi zinakosa wataalamu wa uongozi wa ushirika na asasi ndogo za fedha jambo linalozifanya zishindwe kukua vizuri na kuboresha huduma kutokana na kukosa ubunifu na ugunduzi kuanzia utawala, bidhaa na kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Kutegemea zaidi fedha kutoka nje kwa ajili ya kujiendesha kunadhohofisha nguvu ya taasisi kujitegemea katika utoaji huduma. Benki za biashara zimekuwa zikifaidika na nafasi hii kwa kutoa mikopo mikubwa kwa vyama hivi na kuibua migogoro mingi ambayo kwa kiasi kikubwa imevifanya vyama vyingi kuyumba.

Saccos zinahitaji kujijengea uwezo wa kifedha kwa kuandaa na kuweka mikakati ya kibiashara ambayo itasimama na kutoa dira ya kuwezesha vyama kufika mbali.

Vyama hivi vinapaswa kuepuka sasa badala yake vibuni miradi na huduma nyingi ili kujiwekea mizizi imara ya kibiashara. Kupokea na kutumia fedha kutoka nje siyo tatizo ila viongozi kubweteka kiasi cha kukosa dira ya kujiendesha.

Saccos hazitakiwi kuachwa nyuma na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Hii ni changamoto inayotakiwa kutafutiwa majibu ya haraka kutokana na vyama vingi kukosa mifumo ya kieletroniki inayohifadhi kumbukumbu za biashara kamma vile miamala na taarifa muhimu za taasisi.

Taasisi nyingi zinatumia mafaili kutunza taarifa zao hivyo kuchelewesha huduma pale zinapohitajika. Kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa intaneti na umeme, hakuna haja ya kutotumia teknolojia kufanikisha shughuliza saccos.

Vyama hivi pia vinahitaji mipango endelevu ya biashara ili kuwa na dira. Vyama vinahitaji kuwekeza kwenye utafiti utakaosaidia kubaini njia sahihi ya kuandaa mpango utakaoleza yanayoweza kufanyika kwenye masoko, ushindani, uongozi, mitaji na kunufaisha taasisi.

Ni jambo lililowazi kuwa taasisi za ushirika hazina mipango ya muda mrefu kibiashara hivyo kuhitaji wataalamu wa kutoa mwelekeo sahihi ili kufika mbali kiutendaji.

Taasisi hizi pia zinatakiwa kuacha kuendelea kutumia sera na sheria zilizopitwa na wakati kwenye utoaji wa huduma kwani haziakisi mabadiliko ya uchumi wa kisasa.

Wateja wasiendelee kupata huduma kwa mifumo ya kizamani ambayo haina sura ya maendeleo na haiendani na shughuli za wananchi inayowalazimu wanachama kutafuta huduma kwenye taasisi kubwa za fedha.

Kumekuwa na ushindani mkubwa kwenye sekta ya fedha kutokana na idadi ya taasisi za fedha na mahitaji ya watumiaji.

Pamoja na wingi huo ni vizuri vyama vya kuweka na kukopa vikashughulikia changamoto zilizotajwa kwa kuzifanyia kazi ili kuboresha huduma na kutengeneza mazingira ya kupiga hatua kibiashara.

Tuwasiliane: 0657 157 122