Friday, November 3, 2017

Saratani inavyotafuna uhai wa wanawake nchini

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Saratani ya matiti ni ugonjwa unaowapata wanawake na husababishwa na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake, hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo.

Ikiwa katika hatua za mwanzo, kwa kawaida huwa haina maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Na kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa sababu ugonjwa unaweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema na miongoni mwa dalili za saratani ya mititi ni uvimbe kwenye matiti ama makwapa. Titi kubadilika kiumbo, kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Dalili zingine ni rangi ya ngozi ya titi kubadilika na kuonekana kama ngozi ya nje ya chungwa na ile hali yake ya kuonekana kuwa na ngozi laini hutoweka.

Kwa hapa nchini, saratani hiyo natajwa kuwa ya pili kwa kusababisha vifo kwa wanawake na hali ya kuchelewa kupata ugunduzi na tiba haraka kumeelezewa kuchangia kwa kiwango kikubwa kuleta ugumu wa matibabu.

Takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) hivi karibuni, zimeainisha wagonjwa wapya wanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka kwa wastani wa wagonjwa 206 mwaka 2005 hadi kufikia wagonjwa 816 mwaka jana.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka taasisi hiyo, Crispin Kahesa anasema hizo ni zile za wagonjwa wapya wanaofika kwenye taasisi hiyo pekee na haihusishi wagonjwa wa Tanzania nzima.

“Taasisi hii kwa kipindi cha miaka 10, imepokea wagonjwa wapya 5,867, hata hivyo asilimia 80 yao wamefika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa na hivyo kufanya matibabu yao kuwa magumu,” anasema Dk Kahesa.

Mratibu wa Programu ya Via vya Uzazi kutoka Wizara ya Afya, Dk Safina Yuma anasema saratani ya matiti ni ya pili kwa kuchochea vifo vinavyohusisha saratani kwa wanawake nchini na kuchelewa kupata ugunduzi na tiba ya haraka kukitajwa kuchangia kuleta ugumu wa matibabu.

INAENDELEA UK.16

“Asilimia 80 ya watu wakiugua hupona, lakini Afrika inaonekana ni asilimia 40 pekee mtu akiugua anaweza kupona. Inabidi kuweka mkakati maalumu wa kuhamasisha watu wauelewe ugonjwa huu,” anasema Dk Yuma.

Anasema tatizo la wagonjwa wengi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma katika hatua za mbele za ugonjwa, husababisha kushindwa kuishi kwa muda mrefu, wakigundulika baada ya mwaka mmoja au miwili, hufariki dunia.

Sababu za ugonjwa wa saratani ya matiti

Dk Yuma anasema sababu ya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mama asiponyonyesha mtoto maziwa, kuna homoni fulani lazima zitoke.

“Sasa asiponyonyesha anazizuia zile homoni ambazo zinaweza kufanya mabadiliko katika chembechembe za mwili na ikatokea saratani,” anasema Dk huyo na kuongeza

“Kidunia saratani ya matiti inaongoza lakini kwetu Tanzania ni ya pili katika takwimu kutoka ORCI, inaonyesha saratani inaongoza kuua na asilimia 11 ya wagonjwa wapya ni wa saratani ya matiti na takribani asilimia 10 ya vifo vinatokana na saratani hiyo,” anasema.

Dk Yuma anasema kila mwaka idadi inaongezeka kwa kuwa jamii haina uelewa na wengi hufika hospitali dalili zikiwa zimeshaonekana hata kwa macho.

Anasema ili kupunguza vifo vitokanavyo na saratani ya matiti na kizazi, wizara ilishaanzisha programu ya kusaidia kukinga saratani hizi kwa kuangalia dalili zake mapema ili kuwanusuru kina mama wengi kwa kuwapatia matibabu mapema na kukinga dalili za awali na kuandaa mwongozo na kutoa elimu kwa jamii ili ichukue hatua mapema.

“Saratani inapoanza huwezi kuona dalili na ukiona dalili ujue imefika mbali, kwahiyo, tunahimiza wanawake wengi wahudhurie kwenye vituo vya afya ili wachunguzwe mapema kusudi kuizuia na pia kupunguza gharama kwa Serikali,” anasema.

Nani yuko katika hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti

Dk Yuma anasema mwanamke yeyote yupo katika hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti ikilinganishwa na wanaume, kwani asilimia 99 ya wanaopata ni wanawake na asilimia 1 ni wanaume.

“Mtu akizaa watoto akiwa na zaidi ya miaka 35, hiyo pia huchangia kuugua ugonjwa huo, kwasababu vichocheo vyake vinakaa kwa muda mrefu katika mirija ya maziwa yake, sasa visipotoka, vinaweza kusababisha saratani ya matiti,” anafafanua.

Daktari bingwa wa maradhi ya saratani kutoka ORCI, Crispin Kahesa anasema saratani ya matiti huchukua asilimia 12 ambayo hata hivyo ni ya tatu kati ya zinazosumbua kwa takwimu za kitaifa huku wagonjwa 6,300 waliripoti mwaka 2016, idadi ambayo anasema ni kubwa na imekuwa ikiongezeka, kama hatua zisipochukuliwa, itaongezeka zaidi.

“Kinachokuza saratani hii pia ni umri wetu wa kuishi umeongezeka, kinamama wengi wamepata mafunzo ya kujichunguza wenyewe, lakini haya maradhi yanakuja wakiwa kwenye utu uzima na wengi huwa na wastani wa miaka 49 na wastani wa umri wa kuishi ni miaka 59.

“Lakini pia kuboreshwa kwa mfumo wa afya utakaowezesha kugundua na kuchunguza kampeni mbalimbali za awali,” anasema Dk Kahesa.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinasema kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 hugundulika huku asilimia 26 pekee ndiyo hufika hospitalini kupata matibabu.

Na takwimu za ORCI zinaonyesha idadi ya wagonjwa wapya inazidi kuongezeka kutoka 2,416 kwa 2005 hadi kufikia 6,338 mwaka 2016.

Na aina nne za saratani zikionyesha kuchukua theluthi mbili za wagonjwa wote wa maradhi hayo.

Kutoka 2005 hadi 2016, asilimia 68 ya saratani zinazosumbua Tanzania ni ya matiti, ya ngozi ‘caposis sarcoma’, shingo ya kizazi na mfumo wa njia ya chakula, kwa kila wagonjwa 10, saba wanasumbuliwa na saratani hizo.

Rekodi hiyo ni kwa wale wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo pekee, ukiachana na hospitali zingine zinazotibu saratani nchini ikiwamo ya Bugando, KCMC, Mbeya na kwingineko.

Na inaelezwa saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa asilimia 34 sawa na mgonjwa mmoja kwa kila watatu wanaoumwa ugonjwa huo, nayo inapanda kutoka wagonjwa wapya 879 mwaka 2005 hadi kufikia 2,081 mwaka jana.

Dk Kahesa anasema saratani inayofuatia ni ya ngozi ‘caposis Sarcoma’ inayochukua asilimia 13 ya saratani zote, matiti asilimia 11 na ile ya mfumo wa njia ya chakula ni kwa asilimia 10.

Anazitaja saratani zingine zinazokuja kwa kasi hivi sasa kuwa ni ya shingo na kichwa inayochukua asilimia 7 ya wagonjwa wote, saratani ya matezi kwa asilimia 6 na ile ya damu kwa asilimia 4.

Saratani ya mfumo wa mkojo ina asilimia 3, saratani ya ngozi asilimia 3, jicho asilimia 2 na tezi dume ni asilimia 2 wakati huohuo aina zingine za saratani zikichukua asilimia 5.

Dk Kahesa anasema tangu 2005 mpaka sasa wagonjwa wapya wanaotibiwa katika taasisi hiyo wamefikia 129,075 na kwa wale wanaohudhuria kliniki ni 222,470.

“Waathirika wakuu wa saratani ni wanawake kutokana na aina ya zinazowashambulia wao pekee kuchukua asilimia 44, lakini carposis Sarcoma inaathiri wote hasa wale ambao mfumo wao wa kinga ya mwili umepungua, lakini madhara yake tunaweza kuyaona kwenye ngozi, mfumo wa chakula, hewa na sehemu zingine.

Serikali yaamua kupambana

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitoa Sh1 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, ili kupambana na ongezeko la wagonjwa wapya wa maradhi hayo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema mashine 100 za tiba mgando (cryotherapy) na mashine tisa za upasuaji mdogo (LEEP) pamoja na mitungi ya gesi 173 itakayowezesha mashine hizo kufanya kazi, tayari vimenunuliwa kupitia fedha hizo.

Ummy anasema mashine hizo zitatumika kwa ajili ya matibabu ya awali ya saratani kwa wanawake watakaofanyiwa uchunguzi na kukutwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Tumeshatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma ili kuweza kuhudumu bila vikwazo. Vifaa hivi vimekwishawasili nchini na vimesambazwa katika vituo vya Tiba 100 nchini kwa mikoa 10, Halmashauri 31 ambazo tumebaini zina vituo vichache vya kutolea huduma hizi ukilinganisha na Mikoa mingine.”

Anaitaja mikoa hiyo ni Mara, Singida, Geita, Dodoma, Tanga, Arusha, Manyara, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Anasema tangu 2008 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara imeshaanzisha vituo 459 kati ya hivyo, 343 ni vya Serikali na 116 vya mashirika na watu binafsi.

Kwa pamoja vinatoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa uzazi.

-->