Serikali iingilie kati kuunusuru mtaa wa One Way Dodoma

Muktasari:

  • Mwaka 1973 Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Nyerere, alitoa tamko la Serikali kuhamia mkoani hapa.

Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, ni uamuzi sahihi ambao umeondoa makovu ya hofu iliyokuwa imetanda kwa zaidi ya miaka 43 tangu kutolewa kwa tamko hilo.

Mwaka 1973 Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Nyerere, alitoa tamko la Serikali kuhamia mkoani hapa.

Baada ya hapo, Mwalimu aliendelea kuwa madarakani kwa miaka mingine 12 baada ya tamko hilo, lakini hakufanikiwa kuhamia kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mtikisiko wa uchumi uliosababishwa na vita ya Tanzania na Uganda 1978-1979.

Hata hivyo, ndani ya utawala wa Awamu ya Tano, ndoto hiyo imetimia na uhalisia umeonekana kwa vitendo, licha ya kwamba kinachosubiriwa kwa sasa ni sheria kupelekwa bungeni kwa ajili ya kuitambua Dodoma kama ndiyo makao makuu ya Tanzania.

Lakini, ile kauli ya mgeni njoo mwenyeji apone bado haijawaingia zaidi wenyeji wa mkoa huu; wengi wanaonekana kutojiandaa kuwa Serikali sasa iko katika mkoa wao wa Dodoma.

Si wananchi tu, hata baraza la madiwani lenye jumla ya madiwani 60 wanaonekana kama watu ambao hawajaamua kujipanga licha ya kuwa uwezo huo wanao.

Madiwani hawajafikiria namna bora ya kuuboresha mji wao hasa katika maeneo ambayo yanaubeba na kuutambulisha mji katika sura ya kitaifa na kimataifa. Baadhi ya maeneo ambayo yanajulikana mjini hapa tangu zamani ni mitaa ya Msalato, Zuzu, Area C, Makole, Chamwino na eneo maarufu la One way.

Kwa sasa maeneo hayo hayajakumbukwa, hakuna utambulisho maalumu kwenye maeneo hayo pamoja na wadau ambao mwaka 2016 waliamua kubadilisha majina baadhi ya barabara na mitaa na kuifanyia maboresho makubwa.

One Way ikanufaika kwa ukarabati wa mita 20, lakini vigae vilivyowekwa havifai. Miezi sita tu baada ya kuwekwa vikachoka kuliko vilivyowekwa miaka mingi. Kwa ujumla vigae vilivyowekwa ni vibovu.

Kama hiyo haitoshi, One Way inapotea, mpangilio wake si ule uliokuwapo tangu mwanzo pamoja na maboresho ya majengo ya wafanyabiashara ambayo yamepunguza majengo ya kuta za tope.

Kuanzia barabara ya sita hadi barabara ya 12 kumeharibika, mpangilio wake hauna maana tena, msongamano ni mkubwa na biashara zimepangwa vibaya kiasi mtu hawezi kununua kitu kwa uhuru.

Barabara hiyo imekosa usimamizi wa kutosha na sijui kama ipo sheria ndogo ya kulinda maeneo kama hayo.

Kilichopo sasa eneo hilo ni mvurugano mtupu na sijui nani anayepaswa kusimamia eneo hili lililogeuka kuwa gulio. Hilo ni eneo ambalo wakazi wengi wa mkoa walikuwa wakiingia mjini lazima wapite ama kwa kutafuta mahitaji au kupitia kwa nia ya kukamilisha safari ya mjini.

Nakumbuka Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kabla ya kuingia madarakani ilikuwa kama hajafika One Way kutafuta mahitaji yake, basi mji wa Dodoma kwake usingekuwa na maana. Alipenda hata kupita na kununua sare za chama chake.

Kwa sasa eneo hilo linatishia kurudisha wizi wa mifukoni ambao enzi hizo ulitamba katika mjini huu.

Naamini wahusika wanaliona lakini sijui ni kwa nini wamefumbia macho bila ya kujua huko mbele hali itakuaje kwani ni dhahiri huko tunakoelekea mji wa Dodoma utakuwa na hadhi ya jiji.

Sina uhakika wenye maduka pembezoni ambao ndio walipa kodi wakubwa kama wanaifurahia hali hiyo.

Msongamano wa eneo hilo hauruhusu watu kutembea wawili kwa hatua za pamoja bila ya kuongozana.

Aidha, kupishana na mtu wa mbele yako ni lazima usimame upande mmoja, hivyo kufanya kuwapo kwa foleni ndefu.

Mali zilizomwagwa chini ni nyingi tena zenye thamani maana ni milima ambayo kama si kuzifungulia maduka, zilipaswa kutafutiwa maeneo mengine ili kuruhusu One Way kubaki na uhalisia wake wa kuwa na maduka pekee kwa pande zote.

Mkurugenzi wa Manispaa anapaswa kuingilia kati na kunusuru hali, ili eneo hilo libaki wazi na Serikali iendelee kupata mapato yake kupitia kodi za wafanyabiashara wenye maduka.

Shughuli za Wamachinga katika eneo hili maarufu zinalishushia hadhi.Kutafutwe namna ya kuwasaidia wafanyabiashara hawa, lakini si kuwaacha wakitamalaki katika eneo la One Way.

Kama yalivyo maeneo mengine ambayo ni vitambulisho vya mji wa Dodoma, One Way nalo linaweza kusimamiwa likaupendezesha mji huu.

Habel Chidawali ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Dodoma.