Serikali imesikia, imetekeleza kazi iko kwenu wasambazaji wa taulo za kike

Pendekezo la Serikali la kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (Vat) kwa taulo za usafi za kike ni faraja kubwa kwa maendeleo ya mtoto wa kike kielimu, kijamii na kiuchumi.

Nasema hivyo kwa sababu wanafunzi wengi wa kike hasa wale wa vijijini wanashindwa kuhudhuria masomo yao kipindi cha hedhi kutokana na kukosa dhana muhimu za kujihifadhia.

Wengi wao hutumia njia za kienyeji kujihifadhi na kujikuta hali hiyo ikiwatia aibu mbele ya wanafunzi wenzao wawapo darasani. Hali hiyo ndiyo inayowafanya wengi wao kuamua kuacha kuhudhuria masomo mara waingiapo kwenye kipindi hicho ambacho huchukua takriban siku nne hadi tano katika juma la kila mwezi.

Wanafunzi wengi wa kike na hasa wasichana wanakiri kuwa hedhi ni kikwazo kwao katika kutekeleza mambo mbalimbali. Wengi wanakiri kutumia vitambaa, na huwa wanahofia kama kwa mfano wakiwa darasani au katika shughuli za kawaida za ujasiriamali, wanaweza kuchafuka kwa kupata madoa kwenye nguo zao halafu wakachekwa. Ndiyo maana kwa wanafunzi huona bora wakae nyumbani hadi hedhi itakapokatika ndipo warejee darasani au katika shughuli nyingine.

Mwanafunzi huyu wakati hedhi inapokwisha, kama mwalimu alianza kufundisha mada mpya basi atajikuta akiikosa yote kwa sababu ya hedhi.

Kwa mfano ikianza mada leo, inaweza kuisha kwa siku tatu au nne ambazo ndizo hizo mabinti wanakuwa kwenye hedhi.

Tukumbuke kuwa hawa wanaozungumza hivyo hawajawahi kubahatika kutumia taulo za kike (pedi) za dukani tangu walipopevuka kutokana na kukosa fedha za kununua bidhaa hiyo.

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Geita, Upendo Peneza anasema inakadiriwa kati ya siku 186 na 187 kwa mwaka,wanafunzi wa kike hawafiki shuleni kwa sababu ya hedhi. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na mashirika mbalimbali mwaka 2015 ikiwamo Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), unaonyesha kitendo cha wasichana wengi kutohudhuria masomo kikamilifu kila mwezi kwa kukosa huduma ya hedhi salama, huchangia kuzorotesha elimu. Akizungumza katika moja ya mikutano iliyowahi kufanyika katika ofisi za mtandao huo Mabibo, Dar es Salaam, mkurugenzi mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi alisema katika kipindi wapobaadhi yao hupatwa na maumivu makali ya tumbo, wengine huishi katika mazingira yasiyo rafiki hasa ya ukosefu wa maji safi.

Alisema hiyo nayo ni changamoto nyingine ya kushindwa kwao kuendelea na masomo siku za hedhi. Mbunge Suzan Lyimo anasema hali hii ingepungua na kuwafanya mabinti wasome kwa amani kama wangekuwa na uhakika wa nyenzo za kujihifadhia mfano taulo za kike.

Ukweli unabaki palepale, hizi taulo zinauzwa bei ambayo msichana au mzazi anayeishi kijijini hawezi kumudu gharama kutokana na hali ya uchumi.

Hali hiyo ndiyo inayowaumiza wengi wao na kujikuta wakichukua uamuzi usio sahihi wa kujifungua nyumbani hadi kipindi hicho kipite, kisha warejee darasani au katika shughuli zingine. Hata hivyo, wiki iliyopita, akiwasilisha bungeni Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali inakusudia kuondoa Vat kwa bidhaa hiyo. Ni dhahiri kuwa pendekezo hilo sasa litakapopitishwa na Bunge litamwezesha mwanamke kuokoa fedha nyingi kwa mwaka. Kwa kufuta kodi hiyo, gharama za bidhaa hiyo itapungua kwa wastani wa asilimia 15 kulingana na aina na bei ya bidhaa husika. Kwa wastani, mwanamke hutumia zaidi ya Sh36,000 kwa mwaka kwa ajili ya kununua taulo hizo na kutokana na kuondolewa Vat gharama inatarajiwa kupungua hadi kufikia Sh29,232.

Hesabu hizi zinazingatia kiwango cha taulo 144 anazoweza kutumia mwanamke kwa mwaka iwapo atatumia mbili hadi tatu kwa siku, katika kipindi cha siku nne kwa mwezi. Katika mfano huu bei iliyotumika ni ya wastani wa Sh2,000 kwa rejareja kwa pakiti moja yenye taulo nane.

Mbunge Margareth Sitta anasema akina mama na wasichana hutumia gharama kubwa kununua bidhaa hizo, hivyo kuondolewa Vat kutawezesha wazalishaji na wasambazaji kushusha bei. Anasema wazalishaji wengi wamekuwa wakilalamikia kodi ya Vat na hasa kwa kuzingatia kuwa wengi wanaagiza kutoka nje. Mbunge Catherine Ruge anasema punguzo hilo si haba kwa kuzingatia kuwa ni kilio cha muda mrefu cha watumiaji.

Hatua hii ya Serikali inapaswa kupongezwa licha ya kwamba punguzo ni dogo, lakini pia inapaswa kuanza kufanya uchunguzi ili kujiridhisha na mwenendo wa bidhaa hiyo na kubaini mtumiaji atalazimika kutoa kiasi gani cha fedha hadi inamfikia mkononi.

Tunataka bei iwe rafiki ili kila mtu aweze kuimudu. Nimefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Serikali kuanza kuyafanyia kazi mahitaji yetu, anasema mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi.

Mkurugenzi huyo na wabunge wengine kwa kushirikiana na TGNP wamekuwa mstari wa mbele kupigania usambazaji bure wa bidhaa hiyo katika shule za msingi na sekondari wakisema Serikali pia ingeanza kutoa ruzuku kwa wasambazaji kama ilivyo kwa wale wa kondomu.

Binafsi nadhani hilo nalo ni wazo jema na pia kama Serikali italizingatia na kulipa uzito wa aina yake wa utekelezaji, lengo likiwa ni kumlinda na kumwezesha mtoto wa kike kufikia ndoto yake ya maisha bora kupitia elimu.

0713235309