Serikali inahofia nini kupiga marufuku mifuko ya plastiki?

Muktasari:

  • Hata hivyo, ahadi hiyo haijafikiwa japo ukweli ni kwamba matumizi ya mifuko ya plastiki yana madhara makubwa kimazingira na kiafya.

Kwa muda mrefu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imekuwa ikiahidi kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ili kuhamasisha mbadala wake.

Hata hivyo, ahadi hiyo haijafikiwa japo ukweli ni kwamba matumizi ya mifuko ya plastiki yana madhara makubwa kimazingira na kiafya.

Wataalamu wa mazingira wanasema mifuko hiyo ikitupwa haiozi na ina uwezo wa kuishi zaidi ya miaka 100 hadi 500 ardhini bila kuoza.

Kiafya mifuko hiyo imekuwa ikitumika wakati wa kuhifadhi vyakula ikiwamo kufunikia wakati wa kupika, jambo ambalo wataalamu wa afya wanasema ni hatari.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani wa Taasisi ya Saratani yya Ocean Road (ORCI), Dk Stephano Magulia, matumizi ya plastiki kwenye vyakula ni hatari kwa sababu utafiti mwingi umethibitisha kuwapo kwa kemikali zinazosababisha saratani.

Ukiangalia, kusikiliza na kusoma maelezo mbalimbali ya wataalamu utabaini kuwa matumizi ya mifuko ya plastiki siyo sahihi kwa binadamu kutokana na madhara.

Ndio maana baadhi ya nchi kama Rwanda na Kenya ziliamua kupiga marufuku matumizi hayo na badala yake waliingia kwenye mifuko mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Ukiachilia mbali Rwanda na Kenya, Zanzibar ambayo ipo ndani ya Tanzania ilifanikiwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na sasa hivi wanatumia mifuko mbadala iliyotengezwa kwa teknolojia mbalimbali ambayo haiharibu wala kuchafua mazingira.

Tumeshuhudia kwa nyakati tofauti Serikali ikiahidi kushughulikia changamoto ya mifuko ya plastiki ikiahidi kupiga marufuku kutokana kuwa na madhara mbalimbali kwa binadamu na mazingira.

Jambo hili linaonekana kuchukua muda sasa na bado halijafanyika huku mifuko hiyo bado inaendelea kutumika katika maeneo mbalimbali ya nchi jambo ambalo linachangia kwa namna moja au nyingine uharibifu na uchafuzi wa mazingira.

Ni wakati muafaka kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), chini ya Waziri January Makamba akishirikiana na timu ya wataalamu ipige marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kwa utaratibu maalumu kama ilivyokuwa kwenye sakata viroba.

Nafahamu jitihada mbalimbali zilizoanza na zinazoendelea kufanywa na Makamba akishirikiana na viongozi wenzake katika kuhakikisha matumizi ya mifuko ya plastiki yanafika kikomo na mifuko mbadala inachukua nafasi.

Lakini muda unazidi kwenda na matumizi ya mifuko yanakwenda kwa kasi ikiwemo kutumiwa kama watu kwenye kufungasha na kufunikia vyakula pindi wanapopika au kununua.

Kwa mujibu wa Julius Enock wa Idara ya mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), alisema Watanzania wanatumia mifuko ya plastiki mitatu hadi minne kwa wiki.

Enock alifafanua kwamba kwa mahesabu ya haraka haraka Watanzania wanatumia bilioni 7,8 hadi 10 kwa mwaka.

Tayari wizara husika imeshaitisha vikao mbalimbali vya wadau wa mazingira kupokea maoni na mapendekezo kwa namna watakavyoweza kuondokana na matumizi ya mifuko ya plastiki na kuingia kwenye mifuko mbadala.

Katika kikao hicho, wadau wengi walionekana kulalamikia Serikali kutokana na hatua ya kuchelewa wa kutoa katazo la marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki ilhali nchi za Rwanda, Kenya na Zanzibar zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Tusiende mbali, ikiwa Zanzibar tu kama sehemu ya Tanzania imeweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mifuko hii, inashindikana nini kwa huku Tanzania Bara?

Nani anafaidika na mifuko hii hatari kwa afya zetu, mazingira na hata vizazi vijavyo?

Ni vema Serikali ikasikia kilio cha wadau hao na ikachukua hatua madhubuti ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki ili kulinda afya za wananchi na kuzuia uharibifu na uchafuzi wa mazingira unaosababisha na mifuko hiyo.

Bakari Kiango ni mwandishi wa Mwananchi, anapatikana kwa baruapepe: [email protected]