Thursday, February 16, 2017

Serikali isiwatupe waliopata mimba shuleni

 

By Mwananchi

Gazeti hili toleo la jana lilikuwa na habari iliyozungumzia ripoti ya Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (Human Rights Watch) iliyopewa jina la ‘nilikuwa na ndoto za kumaliza shule’, ikizungumzia asilimia 40 ya watoto walioshindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na sababu kadhaa ikiwamo mimba za utotoni.

Ripoti hiyo iliyotokana na utafiti uliofanywa mwaka 2016 ilibaini wasichana zaidi ya 8,000 waliacha masomo baada ya kupata mimba au kuolewa kwa nguvu.

Utafiti huo uligundua kuwa maofisa wa shule hufanya vipimo vya lazima vya ujauzito mara kwa mara, jambo wanaloaamini ni udhalilishaji.

Hii si mara ya kwanza kutolewa taarifa za utafiti kuhusiana na tatizo hilo ambapo wasichana wengi hukatishwa masomo kutokana na mimba za utotoni.

Mbali na ripoti hiyo, pia kuna mifano mingi inayoonyesha ukubwa wa tatizo, mwaka 2009 wasichana 300 wa Mkoa wa Tanga walikatishwa masomo kutokana na mimba, 2010 mkoani Kagera walikuwa 880, mwaka huohuo mkoani Pwani walikuwa 500.

Pamoja na jitihada mbalimbali za kumkwamua mtoto wa kike, bado sheria yetu ya elimu ya mwaka 1978 imeendelea kumnyima haki binti anayepata mimba akiwa bado shuleni.

Kifungu cha 35 na kanuni zake za mwaka 1978 na marekebisho ya 1995 na 2002, kinaeleza wazi kuwa mtoto wa kike akipata mimba ni ushahidi tosha kuwa amefanya vitendo vya ngono vilivyo kinyume na sheria za shule, hivyo afukuzwe shule.

Tunaamni umefika wakati sasa wa kubadilisha sheria kwa lengo la kumsaidia mtoto wa kike, kwa kuwa takwimu za kila mwaka zinazoonyesha ongezeko la mimba za utotoni hazifurahishi.

Mbali na hoja ya kubadili sheria, lakini ifike mahali wanaume wanaowapa mimba wanafunzi nao wachukuliwe hatua za kisheria, tena sheria zitamke wazi kwamba ‘mafataki’ hao wapewe adhabu kali, hata kama ni mwalimu au mwanafunzi mwenzake.

Tunaamini ile dhamira ya Serikali ya kuruhusu wasichana wenye mimba kurudi shule na kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua, itaongeza kasi hata kutungiwa sheria ili kunusuru kundi la wasichana wanaopoteza mwelekeo wa maisha kutokana na mimba za utotoni.

Kwani hatutakuwa wa kwanza kutekeleza hilo la kuwarudisha wasichana wenye mimba shuleni. Nchi nyingi zinafanya hivyo na faida zimeonekana wazi. Hakuna faida ambazo nchi yetu imepata tangu ianze kuwaondoa shuleni mabinti wenye mimba.

Nchi za Kenya, Zambia na Rwanda ni mfano mzuri wa mataifa yaliyofanikiwa kuwarejesha wasichana wenye mimba shule na wakaendelea na elimu yao kisha wakanufaika nayo.

Jambo muhimu ni kuandaa mazingira rafiki yatakayowafanya watoto wetu warejee shuleni kwa utaratibu mzuri na watoto wao wabaki wakilelewa katika mazingira ya mwendelezo mzuri wa makuzi.

Wanaopata mimba wakiwa shule ndiyo kundi kubwa la nguvu kazi ya taifa wanaohitajika sana kuiendeleza nchi yetu.

Tusipowaelimisha wataindelezaje nchi yao? Wakiendelea kufukuzwa shule tutaendeleza kudhoofisha nguvu kazi ya taifa letu wenyewe na kushindwa kusonga mbele.

-->