Thursday, December 7, 2017

Serikali sasa igeukie rasilimali misitu

 

        Ilipoingia madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza mara moja kupambana na mambo mengi ambayo huko nyuma yaliachwa yatawale na hivyo kuathiri maisha ya wananchi kwa njia moja ama nyingine.

Mathalan, Serikali hiyo ilianza na wafanyakazi hewa waliokuwa wakitafuna takriban Sh17 bilioni za walipakodi bila uhalali wowote kama mishahara yao, huku ikirejesha nidhamu ya utendaji serikalini iliyokuwa kwa kiasi fulani imeporomoka.

Baada ya hapo, ilianza kushughulikia rasilimali za wananchi hususan madini ambayo kwa miaka mingi wageni walikuwa wameyageuza kuwa sawa na haki yao, wakijipangia namna ya kuyafaidi bila kuguswa.

Ingawa zipo pia changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizojitokeza hapa na pale, lakini hatuna budi kuipongeza Serikali kwa kusimamia msimamo thabiti wa kuhakikisha Watanzania wananufaika na madini yao.

Itakumbukwa kwamba wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliwahi kujiweka kando na suala la madini mpaka hapo kizazi cha Watanzania wazalendo watakapokuja kuyachimba kwa manufaa ya wote na si wachache.

Wakati tunafurahia juu ya Serikali kudhibiti utoroshaji madini ndani ya nchi, uboreshaji wa sheria ya madini na msimamo iliouonyesha tangu ilipoanza majadiliano na wawekezaji katika sekta hiyo ikitaka taifa linufaike, bado kuna rasilimali zingine inazopaswa kuziangalia ikiwamo ya misitu.

Tofauti na madini ambayo wengi tunaowalalamikia kutotenda haki kwetu ni wageni, hili la misitu ni sisi wenyewe. Misitu inaharibiwa kwa kasi na inatishia kutoweka iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa. Zipo taarifa kwamba kila mwaka ekari 372,000 zinaharibikiwa. Uharibifu huo wa misitu unatokana na uvunaji holela, uchomaji wa mkaa na kilimo cha kuhamahama ambavyo katika maeneo mengi nchini vimeshamiri.

Bahati mbaya ni kwamba, kilio cha uharibifu wa misitu ni mamlaka chache zinazokiangalia kwa jicho la pili ili kukabiliana nacho, na kuna kila dalili kwamba zinategeana kuchukua hatua kuwabana wahusika.

Tukiondoa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zenye uoto mzuri wa asili unaolindwa kutokana na kuwapo kwa misitu, lakini hili linatishiwa na uharibifu unaofanyika.

Hivi ni kweli kwamba mamlaka zimeshindwa kukomesha kilimo cha kuhamahama? Wameshindwa kutokomeza uchomaji mkaa? Nani atasaidia kumaliza haya kama wahusika wako kimya?

Zipo taarifa kwamba mkaa na kuni kutoka Tanzania umekuwa ukisafirishwa kwenda katika mataifa ya Uarabuni na biashara hiyo imekuwapo miaka mingi. Je imeshindikana kukomeshwa? Au kuna wahusika mamlakani wanaonufaika na biashara hii?

Hapana, Taifa hili ni letu. Tunataka mvua na maji ili tuishi maana hatuna mahali pa kukimbilia iwapo tutakosa maji kuendeshea uhai wetu. Misitu inakaribisha mawingu yanayoleta mvua. Tuilinde.

Kama alivyosema mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa juzi, inabidi uangaliwe utaratibu mpya wa utoaji wa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu na wasiopanda miti kwanza kabla ya kukata ni vyema wasipewe vibali.

Ni lazima tubadilike sasa. Haiwezekani mtu avune asichopanda, hata maandiko ya dini yanakataza kula asichokitafuta. Mtu asipewe kibali cha kuvuna mkaa endapo hatakuwa na shamba la miti.     

-->