Shule za Serikali zinashindwaje kuingia 10 bora?

Muktasari:

  • Tunachokiona hapo kwa miaka miwili mfululizo shule zinazoingia 10 bora zote ni binafsi huku zile za Serikali zikishindwa kuonekana zikifanya vizuri. Matokeo haya yanaonyesha bado kuna safari ndefu kwa shule za Serikali kuingia katika kundi la 10 bora.

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) juzi lilitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba huku wanafunzi 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani huo wakifaulu kwa viwango vizuri. Ufaulu huo umeelezwa umepanda kwa zaidi ya asilimia mbili, mwaka 2015 ikiwa asilimia 67.84, mwaka 2016 (asilimia 70.36) na mwaka 2017 (asilimia 72.76).

Tunachokiona hapo kwa miaka miwili mfululizo shule zinazoingia 10 bora zote ni binafsi huku zile za Serikali zikishindwa kuonekana zikifanya vizuri. Matokeo haya yanaonyesha bado kuna safari ndefu kwa shule za Serikali kuingia katika kundi la 10 bora.

Sote tunafahamu kati ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ni utoaji wa elimu bure, lengo likiwa ni kupanua wigo na kuhakikisha elimu inapatikana kwa wote hasa uboreshaji wa elimu ya msingi.

Pia, sera ya elimu bila malipo ya ada kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari inaonekana kuongeza viwango vya uandikishaji wa wanafunzi kwa hali ya juu. Hii ni kwa sababu vikwazo vyote vya uandikishaji vimeondolewa.

Tunaipongeza Serikali kwa kuwekeza zaidi katika kutatua changamoto za miundombiunu kama vile madawati na madarasa. Lakini, juhudi zote hizo za Serikali katika kipindi cha miaka miwili bado zimeonekana kutoleta manufaa kwa waliokusudiwa, ufaulu wa shule za Serikali ukiashiria kwamba kuna mahala panahitaji kurekebishwa.

Swali la kujiuliza ni kwa kiasi gani mfumo wa elimu nchini umejipanga kuwezesha ongezeko la wanafunzi kwenye shule za Serikali kujifunza na kupata stadi zinazotakiwa? Au nchi itabaki katika upatikanaji wa bora elimu kwa wengi na si kuhakikisha ubora wa elimu kama wananchi wengi waonavyo?

Baadhi ya watafiti wa masuala ya elimu ripoti zao ziliwahi kubainisha kuwa ubora na njia za ufundishaji kwa wanafunzi ambao idadi imeongezeka maradufu, hasa shule za msingi ukilinganisha na siku za nyuma bado haujaboreshwa.

Ni ukweli usiofichika kwamba tatizo la walimu linatajwa na wananchi wengi ikiwa ni changamoto ambayo idadi ya wanafunzi ni kubwa kulinganisha na walimu wanaofundisha, huku katika shule za binafsi uendeshaji wake ukiwa na uwiano kati ya walimu na wanafunzi darasani sanjari na miundombinu bora.

Changamoto zingine zilizobainishwa ni za muda mrefu tangu miaka ya nyuma kama vile ukosefu wa vyumba vya madarasa, vitabu, walimu kutofundisha vizuri huku wengine wakitaja suala la ukosefu wa chakula shuleni kuwa ni tatizo kwa shule za Selikali.

Mbali na changamoto hizo ambazo Serikali inapaswa kuziangalia upya ili shule zake ili ziweze kushindana na shule binafsi ambazo kila mwaka zimeonekana kutamba kwenye kundi la 10 bora, Serikali ijikite kutafuta suluhisho la kudumu kwa matatizo mengine yakiwamo ya uwiano wa walimu katika shule, makazi na huduma kwa wakufunzi hao.

Tunaamini hilo linawezekana iwapo Serikali itaamua kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Pia, Necta imetangaza kufuta matokeo yote ya watahiniwa 10 waliofanya udanganyifu katika mtihani huo, hili nalo tunaliona ni dosari ambayo inatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Haiwezekani kila Necta wanapotangaza matokeo lazima kuwapo na waliofanya udanganyifu, lakini chanzo cha udanganyifu hakijawahi kuwekwa hadharani kama ni walimu au wasimamizi wa mitihani.

Tunadhani Necta wafike mahala wawashughulikie kwa mujibu wa sheria wale wote wanaochangia kuendelea kwa tatizo la udanganyifu wakati wa ufanyaji wa mitihani. Rai yetu kwa Serikali washughulikie changamoto katika shule zake ili ziweze kushindana na shule binafsi. Pia Necta ihakikishe inamaliza tatizo la udanganyifu kwenye mtihani.