TFF, ZFA zikae kujadili mustakabali wa Zanzibar

Muktasari:

  • Bila shaka uamuzi huo umestua wengi, hasa Wazanzibari ambao waliona kuwa hatua ya kupata uanachama ingeweka jukwaa zuri kwa soka la Zanzibar kujitangaza kimataifa na kuwapa wachezaji fursa ya kuonekana duniani.

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limeamua kuivua Zanzibar uanachama, ikiwa ni takriban siku 120 tangu lililopitisha kwa kura nyingi uamuzi wa kuiruhusu kuwa mmoja wa wanachama wake.

Bila shaka uamuzi huo umestua wengi, hasa Wazanzibari ambao waliona kuwa hatua ya kupata uanachama ingeweka jukwaa zuri kwa soka la Zanzibar kujitangaza kimataifa na kuwapa wachezaji fursa ya kuonekana duniani.

Lakini katika mkutano wake wa dharura uliofanyika Morocco wiki hii, CAF ilibatilisha uamuzi wake kwa kusema kuwa Zanzibar ilipewa uanachama kimakosa kwa kuwa katiba ya shirikisho hilo inaeleza bayana kuwa mwanachama ni lazima awe taifa kamili linalotambuliwa na Umoja wa Mataifa na pia nchi moja haiwezi kuwa na vyama viwili tofauti.

Ni hatua ambayo imezingatia Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na katiba ya CAF na hivyo, uamuzi wa awali kuonekana kuwa ulikuwa wa kisiasa uliolenga kuongeza idadi ya wanachama bila ya kuzingatia misingi muhimu.

Wakati huu ambao Taifa linatafakari kitendo hicho cha CAF kughairi, ni vizuri wahusika wa soka nchini; Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mabaraza ya michezo ya Bara na Visiwani kukaa pamoja kujadili jinsi ya kuenenda kulingana na uamuzi wa shirikisho hilo la Afrika.

Uamuzi umeshafanywa na hivyo ni kuufuata na kutafuta njia za kwenda sambamba nao na kama kuna jitihada za kutafuta mkakati mwingine, basi zifanyike wakati uamuzi huu wa sasa ukitekelezwa.

Ni kweli kwamba Zanzibar inaona haina uwakilishi wa kutosha katika uendeshaji soka la nchi kwa kuwa unaonekana kuipa nafasi zaidi Tanzania Bara. Pamoja na ukweli kwamba, uongozi wa TFF ni wa kuchaguliwa, ni vigumu kwa mgombea kutoka visiwani akashinda uchaguzi katika mkutano wa wajumbe wengi kutoka Bara.

Kwa hiyo, vyombo hivyo havina budi kukutana na kuangalia njia bora za uwakilishi wa Zanzibar katika vyombo vikuu vya uamuzi vya TFF, kama Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu ambazo zitavihakikishia visiwa hivyo kuwa na uwakilishi.

Suala jingine muhimu ni uwakilishi wa klabu za Zanzibar katika mashindano ya klabu barani Afrika. Wakati Zanzibar ilipopewa uanachama wa muda kusubiri maombi yake Fifa, takriban miaka mitano iliyopita, klabu za Zanzibar ziliingizwa katika mashindano ya klabu ya Afrika.

Lakini uamuzi mpya wa CAF unaweza kumaanisha kuwa katika mashindano yajayo, klabu za Zanzibar zinaweza zisishirikishwe na hivyo hiyo inatakiwa kuwa ajenda muhimu wakati vyombo hivyo vitakapokutana kujadili mustakabali wa visiwa hivyo kimataifa.

Mgawanyo wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na vyombo vya kimataifa kama Fifa na CAF pia ni suala muhimu kuwekewa msimamo. Ni dhahiri kuwa TFF imekuwa ikitekeleza miradi hiyo; kama kozi za makocha, waamuzi, madaktari na soka la wanawake, kwa kushirikisha Wazanzibari.

Lakini hilo limekuwa halionekani na kutumiwa na wanasiasa kuonyesha kuwa Zanzibar hainufaiki. Ni jukumu la taasisi hizo kukubaliana katika hilo na kuweka utaratibu utakaoeleweka ili kusiwe na malalamiko yasiyo na msingi hapo baadaye.

Tunaamini kuwa iwapo TFF, ZFA, BTMZ na BMT zitakutana na kujadili kwa dhati suala hilo, malalamiko na siasa zitaondoka katika uendeshaji soka nchini.