Tuesday, October 10, 2017

Tanzania inaweza kuamua hatima ya Sahara Magharibi

Noel Shao ni mhitimu wa shahada ya elimu Chuo

Noel Shao ni mhitimu wa shahada ya elimu Chuo Kikuu cha Dodoma 

By Noel Shao

Waasisi wa vuguvugu la ukombozi wa Afrika wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, waliwahi kutamka maneno haya: “Afrika moja, Afrika huru”

Waasisi hawa wakiwamo Nelson Mandela, Edward Mondlane, Samora Machel, Patrice Lumumba, Kwame Nkurumah na wengineo, kwa pamoja walifanya harakati za kuhakikisha mataifa yote ya bara la Afrika yanapata uhuru.

Viongozi hao waliamini katika umoja wa Afrika; walishikamana, waliungana na walitiana moyo kuhakikisha Afrika inaondokana na mateso ya ukoloni, wakisukumwa na imani ya Afrika ni moja kiasili na kiutamaduni.

Ni kwa sababu hiyo, walitaka kuona asili hiyo inarejea ili kuhitimisha mifarakano ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni, iliyochochewa na ujio wa ukoloni.

Hawakusita kusaidiana katika mafunzo ya kijeshi, silaha, ujuzi, na hata raslimali watu ili kufanikisha lengo lililokuwa mbele yao. Walijua kumuondoa mkoloni haikuwa kazi rahisi; haikuwa kazi ya kiongozi mmoja au nchi moja, ni jambo lililohitaji maono na nguvu ya pamoja.

Walikuwa tayari kupambana kwa pamoja na kukabiliana na changamoto pamoja, lengo likiwa ni uhuru wa Mwafrika kwa faida ya vizazi vya leo.

Dhana ya Afrika moja, Afrika huru ilianzishwa ili kuhimiza mapambano ya pamoja kama bara na si kama nchi mojamoja, vinginevyo ingekuwa rahisi nchi moja kupata uhuru na kuamua kuendelea na ujenzi wa mambo yake ya ndani.

Hata pale nchi moja ilipotangulia kupata uhuru, mapambano yaliendelea katika nchi nyingine ili kutimiza kauli mbinu ya Afrika Moja, Afrika Huru.

Katika mapambano hayo ni wazi Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kitovu cha vuguvugu la ukombozi wa nchi nyingi Afrika.

Tanzania ilifanya kazi kubwa kiasi cha kujijengea heshima katika anga mbalimbali duniani kwa harakati za ukombozi na uhuru wa nchi za Afrika.

Sasa ni wakati wa kurejea historia yetu kama Taifa. Ni wakati wa kudumisha umoja, amani, na udugu wetu wa kutetea wanyonge popote walipo duniani.

Taifa la Sahara Magharibi, ndiyo nchi pekee Afrika ambayo mpaka wakati huu haijajipatia uhuru wake kutoka kwa taifa la Morocco linaloikalia tangu mwaka 1975 .

Watu wa Sahara Magharibi hawapo huru, bado wana manyanyaso na vidonda vya ukoloni, njia mbalimbali za kivita na mazungumzo zimeshafanyika kuitaka Morocco kuipatia Sahara Magharibi uhuru bila ya mafanikio.

Katika mkutano wa 72 wa Umoja wa Mataifa uliomalizika hgivi karibuni jijini New York, Marekani, jambo hili lilijtokeza. Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga ni miongoni mwa viongozi waliohutubia kutaka kuona uhuru wa Sahara Magharibi unapatikana.

Tanzania ikiungana na nchi za Afrika kusini, Zimbabwe, Namibia, Lesotho, Angola, Msumbiji na nchi nyingine nje ya Afrika kama Timor Mashariki na Ufaransa ambazo zilitoa tamko la kupenda kuona watu wa Sahara Magharibi wakipatiwa uhuru.

Binafsi naamini ukiachilia mataifa mengine yenye ushawishi juu ya suala hili, Tanzania bado inasimama kwa namna ya kipekee katika kuamua hatima ya watu wa Sahara Magharibi kutokana na historia ilivyo.

Hivyo, Tanzania ikiwa na nia ya dhati kwa vitendo kama ilivyo onyesha katika mapambano ya Afrika Kusini na Msumbiji, uhuru, haki, na suluhu ya kudumu itapatakana na Sahara Magharibi itajitawala.

0769735826

-->