UCHAMBUZI: Tufanye haya kuinua ubora wa elimu yetu

Dr Godfrey Malisa

Muktasari:

  • Nilikazia hoja ya umuhimu wa Serikali kuvisaidia vyuo vikuu binafsi ili vitoe elimu bora na sio kuvifungia.

Hivi karibuni niliandika makala katika gazeti hili kuhusu hatua ya Serikali kufungia vyuo vikuu na mustakabali wa elimu yetu nchini.

Nilikazia hoja ya umuhimu wa Serikali kuvisaidia vyuo vikuu binafsi ili vitoe elimu bora na sio kuvifungia.

Ieleweke kuwa kufungwa kwa chuo cha elimu ya juu si tija kwa taifa letu, lakini matamko yanayotolewa na baadhi ya watumishi wa mamlaka zinazosimamia elimu, utaona dhahiri kwamba hawalioni hili na wanafanya bidii kuendelea kufunga vyuo binafsi zaidi ili kuonyesha kwamba wanasimamia ubora wa elimu nchini.

Sioni jinsi gani ufungaji wa vyuo utaimarisha ubora wa elimu. Serikali tangu tupate uhuru ilitangaza maadui watatu wa maendeleo yetu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi

Hata hivyo, kuna mambo kadhaa ambayo yakitekelezwa, yatainua kwa kiwango kikubwa ubora wa elimu ya juu hapa Tanzania. Makala haya yanalenga kutaja mambo machache.

Tunahitaji kushirikiana ili kuinua ubora wa elimu. Wadau wa elimu kutoka sekta ya umma na wale wa sekta binafsi watafanikiwa ikiwa kutakuwa na mikakati ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Kubadilishana uzoefu, mbinu za utafiti, kushirikishana mitalaa, ziara za wahadhiri na wanafunzi katika vyuo vingine kujionea na kujifunza kile wengine wanachofanya ni baadhi ya mambo yanayopaswa kufanywa ili kuinua ubora wa elimu.

Ni muhimu pia kuwa na vikao vya pamoja kati ya wahadhiri wa vyuo vya umma na vile vya binafsi kujadiliana jinsi ya kuinua ubora wa elimu kwani baadhi ya wahadhiri ni wale wale kwenye vyuo hivi.

Nchi zilizopiga hatua kubwa katika maendeleo ya elimu zimefanikiwa kuwa na mtandao mpana wa ushirikiano miongoni mwa taasisi zao na miongoni mwa wahadhiri bila kubagua kati ya vyuo vya umma na binafsi.

Tukumbuke kwamba hatimaye mwanafunzi aliyehitimu katika chuo cha umma au binafsi, anaishia kulitumikia taifa hili hili bila kujali alisomea chuo gani. Msingi wa upatikanaji wa elimu bora hutokana kwanza na upatikanaji wa walimu bora.

Hii ni changamoto kubwa inayolikabili Taifa hivi sasa. Ubora wa walimu katika ngazi zote za ufundishaji unatia shaka.

Wanafunzi bora wa vyuo vikuu hutokana na wanafunzi bora katika ngazi ya sekondari na ya shule za msingi.

Ukiwa na walimu wenye uwezo mdogo katika shule za msingi, kutaathiri shule za sekondari. Na walimu wenye uwezo mdogo shule za sekondari, wataathiri uwezo wa wanafunzi wakiwa vyuo vikuu. Vyuo vikiathirika taifa litaathirika kwa kuwa na wataalamu wasio na viwango. Ingawa ukweli huu unafahamika na mamlaka zinazohusika, bado tatizo hili ni kubwa.

Ufike wakati sasa wadau wote wa elimu wakae chini na kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hili sugu la ubora wa walimu ambalo linachangiwa na sababu mbalimbali.

Ili tuinue kiwango cha elimu, tena kwa haraka, ili hatimaye twende sambamba na mataifa mengine, wakati umefika wa kupitia upya sheria na kanuni zinazosimamia utoaji wa elimu.

Kwa muda mrefu sasa ubora wa elimu umeathiriwa kwa kutokuwapo kwa msimamo mmoja katika sera za elimu. Tumeshuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ya sheria, kanuni na sera za elimu kiasi kwamba hazitekelezeki.

Mathalani, sheria zinazosimamia uanzishwaji na uendeshaji wa vyuo vikuu na hata Tume ya Vyuo Vikuu zinahitaji kupitiwa upya, kwani utekelezaji wake unavibana sana baadhi ya vyuo. Upitiwaji huu ufanyike kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta ya umma na binafsi.

Elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya taifa lolote, na taifa ambalo halitatoa kipaumbele cha kwanza kwenye elimu, litabaki nyuma kimaendeleo daima.

Baadhi ya mataifa kama Korea Kusini, Singapore na Malaysia yalikuwa na maendeleo duni kama sisi, lakini walipolipa kipaumbele suala la elimu, leo ni miongoni mwa mataifa yenye maendeleo hali ya juu.

Kama kweli Watanzania wote tunataka kuona Taifa letu linapata elimu bora, tusiiachie Serikali peke yake; kila mmoja wetu ajitose katika kusaidia sekta ya elimu.

Inakuaje tunachangia kwa wingi sherehe za harusi, ubarikio, sikukuu za kuzaliwa, kipaimara, lakini katika suala la elimu tunakuwa mkono wa birika?

Hata kama umewasomesha watoto wako, bado unaweza kuendelea kuchangia kwa sababu Taifa likipiga hatua kubwa ya maendeleo, hata hao watoto wako watafaidi.

Mwandishi ni mhadhiri mstaafu aliyewahi pia kugombea urais na uspika wa Bunge mwaka 2015

0716 - 810677