Tume itoe elimu ya uchaguzi kuzuia vurugu za mara kwa mara

Mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jaji Semistocles Kaijage akiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan.

Muktasari:

  • Wanasiasa na hata wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa uchaguzi ama haupo huru au haki haijatendeka kwa sababu ya kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi husika. Hata kile kitendo cha kuchelewa kutoa matokeo ya uchaguzi huchagiza vurugu kwani wasiwasi wa kutokea hujuma huwa mkubwa. Uhuru wa Tume ya Uchaguzi unapimwa kwa vigezo kadhaa ambavyo ni muundo wake (uteuzi), uhuru wa rasilimali fedha, kuwa na wafanyakazi wa kutosha na nafasi ya wadau kuhoji maamuzi ya tume.

Uchaguzi mdogo wa ubunge wa Dimani, Zanzibar na madiwani katika kata 19 za Tanzania Bara umemalizika na malalamiko kama kawaida yamesikika. Imekuwa ni kawaida kutokea vurugu wakati wa uchaguzi na mara nyingi vurugu hizi huashiria kukosekana imani kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Wanasiasa na hata wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa uchaguzi ama haupo huru au haki haijatendeka kwa sababu ya kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi husika. Hata kile kitendo cha kuchelewa kutoa matokeo ya uchaguzi huchagiza vurugu kwani wasiwasi wa kutokea hujuma huwa mkubwa. Uhuru wa Tume ya Uchaguzi unapimwa kwa vigezo kadhaa ambavyo ni muundo wake (uteuzi), uhuru wa rasilimali fedha, kuwa na wafanyakazi wa kutosha na nafasi ya wadau kuhoji maamuzi ya tume.

Makamishna wa Tume zetu za uchaguzi huteuliwa na mamlaka ambazo kwa namna moja au nyingine zina masilahi katika vyama.

Tume kutegemea fedha kutoka serikalini pia kunakwaza uhuru wake kwani bila shaka anayemlipa mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo.

Kadhalika, tume zetu za uchaguzi zina wafanyakazi wachache, hivyo wakati wa uchaguzi hubidi zitumie wafanyakazi wengine wa serikali kama vile walimu kuwasaidia kusimamia uchaguzi. Katika mazingira hayo ambayo tume inategemea wafanyakazi wa Serikali, ambao kimsingi ni watiifu kwa Serikali ya chama kilicho madarakani, inaweza kuzusha hofu kuwa haipo huru kwa sababu tu ya mazingira hayo.

Tume huru ni ile ambayo wananchi/wadau wako huru kuhoji matendo na maamuzi ya tume. Tume iliyoundwa katika misingi ya kuipa hifadhi na kinga na kuifanya iko juu ya kila kitu hiyo ni Tume isiyozingatia matakwa ya utawala bora.

Kwa mujibu wa Ibara ya 74 (12) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, maamuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi hayahojiwi popote. “Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.”

Kipengele hiki hakiipi uhuru Tume bali kinaipa mamlaka ya makubwa sana. Uamuzi wa Tume haupingwi popote wala hautenguliwi, hali hiyo haiakisi misingi ya utawala bora, misingi ya kuwapo uangalizi na uwiano katika kuendesha mambo hasa kwa sababu hata hao wanaoiongoza Tume wana utashi wao na kisiasa.

Ikiwa Tume ya Uchaguzi itajitosheleza na kujisheheni kimamlaka pengine hata hizi vurugu zinazotokea katika uchaguzi zitaweza kudhibitiwa na kazi za mawakala wa vyama vya siasa zitarahisishwa.

Tume ya Uchaguzi ilipoulizwa kuhusu vurugu zilizodaiwa kutokea katika baadhi ya maeneo Arusha, Morogoro, Kagera na Zanzibar ilisema kuwa haina taarifa ya kutokea kwa vurugu kwa sababu hakuna aliyejaza fomu Na 16 ya kukataa matokeo.

Hiyo ina maana ya kuwa wapigakura na hata mawakala walio wengi hawafahamu kwamba kama wana malalamiko kuhusu uchaguzi wanapaswa wayaweke katika maandishi kwa kujaza fomu husika. Hivyo ndiyo kusema kuwa wananchi wanapaswa wapewe elimu kuhusu haki na wajibu wao wakati wa uchaguzi.

Inawezekana kuendesha chaguzi zisizo na migogoro ikiwa Tume ya Uchaguzi itajiweka katika mazingira ambayo watu wataamini kuwa ipo huru, lakini pia inapaswa kutoa elimu bila kuchoka.