Tumuenzi Bendera kwa kufuzu Afcon 2019

Muktasari:

  • Bendera alifariki akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikofikishwa kwa ajili ya matibabu zaidi akitokea Hospitali ya Bagamoyo alikokuwa amelazwa.

W iki iliyopita, tasnia ya michezo na duru za kisiasa zilipatwa na pigo zito baada ya kuondokewa na mtu muhimu, Joel Nkaya Bendera.

Bendera alifariki akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikofikishwa kwa ajili ya matibabu zaidi akitokea Hospitali ya Bagamoyo alikokuwa amelazwa.

Bendera ameacha simanzi kwa familia yake, ndugu, jamaa na marafiki lakini eneo kubwa jingine ambalo limepoteza moja ya nguzo zake ni nyanja ya michezo ambako alitumikia kwa nafasi tofauti; waziri, kocha na mkufunzi.

Mbunge huyo wa zamani wa Korogwe Mjini alizikwa jana nyumbani kwake Korogwe mkoani Tanga.

Bendera ameondoka lakini ameacha alama kubwa kwenye michezo, lakini iliyo kuu ni jinsi alivyoshiriki kuiwezesha timu ya taifa ya soka, Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 nchini Nigeria.

Wakati huo alikuwa mmoja wa makocha wasaidizi wa Slawomir Wolk, kocha kutoka Poland. Msaidizi mwenzake alikuwa Ray Gama, ambaye kwa sasa pia ni marehemu.

Si rekodi hiyo tu, bali enzi za uhai wake, Bendera, ambaye ni mnazi wa klabu ya Yanga, aliiongoza Simba mwaka 1979 kupata ushindi wa kihistoria nchini iliposhinda kwa mabao 5-0 dhidi ya wenyeji Mufurila Wanderers nchini Zambia baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) jijini Dar es Salaam.

Kwa hilo na mengine mengi katika michezo, yatabakia kuwa kumbukumbu kubwa na yameingia katika rekodi na historia ya michezo nchini.

Wakati Taifa likijifuta machozi kwa kumpoteza kiongozi huyo, michezo inakabiliwa na mashindano tofauti yaliyo mbele, hasa michezo mikubwa kama fainali za Mataifa ya Afrika, Michezo ya Olimpiki na mingine.

Kama kuna wanamichezo wanawiwa sana, basi ni wachezaji, viongozi na mashabiki wa mpira wa miguu ambao wanatakiwa wafanye kitu ili kufuta machozi hayo na kuenzi kazi zilizofanywa na Bendera katika tasnia hiyo.

Ili kuyafuta machozi hayo, viongozi, makocha, wachezaji na wanamimichezo wengine hawana budi kuhakikisha wanapata mafanikio katika mashindano yanayofuata, kwa kuanzia na fainali zijazo za Mataifa ya Afrika za mwaka 2019.

Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na Lesotho, Uganda na Cape Verde kuwania nafasi tiketi mbili za kwenda Cameroon kwenye fainali hizo kubwa katika soka barani Afrika.

Ni vizuri basi kwa viongozi kupanga programu nzuri ya Stars kwa mwaka wote wa 2018 kwa ajili ya kuhakikisha timu inapata maandalizi mazuri na inacheza mechi zake kwa kujituma kuhakikisha Tanzania inarudi tena AFCON kamaambavyo Bendera na wenzake walifanya mwaka 1980.

Makocha na wachezaji hawana budi kutumia programu hiyo vizuri kwa kujituma uwanjani kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ya kutuwezesha kufuzu.

Na mashabiki hawana budi kuhakikisha kuwa wanakuwa nyuma ya timu wakati wote inapocheza nyumbani ili timu za wageni zinapokuja zione zinakuja katika uwanja mgumu kupata ushindi kutokana na mashabiki wake.

Tunaamini kuwa tunaweza kufuzu na hivyo tutumie uwezo wote kuenzi juhudi za Joel Bendera.