Tunachelewa kuwaona nyota wa Zanzibar

Muktasari:

  • Ni dhahiri kuwa kiwango kilichoonyeshwa na Stars, ambacho kocha wake Ammy Ninje amekiita “fantastic perfomance”, hakijamfurahisha mwingine yeyote isipokuwa kocha huyo.

Juzi timu ya Tanzania Bara ilitolewa kwenye michuano mikongwe ya Kombe la Chalenji baada ya kufungwa mabao 2-1 na Rwanda na hivyo kutokuwa na uwezo wa japo kuzipiku Kenya na Zanzibar zenye pointi tano na saba hata kama itaishinda Kenya katika mchezo wa mwisho.

Ni dhahiri kuwa kiwango kilichoonyeshwa na Stars, ambacho kocha wake Ammy Ninje amekiita “fantastic perfomance”, hakijamfurahisha mwingine yeyote isipokuwa kocha huyo.

Wengi wataibuka na hoja nyingi za kukosoa timu ya Bara na uteuzi wa kocha huyo, ambaye amekuwa akitoa maoni ya ajabu kila baada ya mechi, na kuimwagia sifa Zanzibar ambayo imepigana kiume kushinda mechi mbili za mwanzo na kutoka sare na wenyeji katika mechi ya Jumamosi.

Kuna video inatembea mitandaoni inayomuonyesha kijana mmoja akizungumza kwa hasira kuitaka Zanzibar Heroes irudi nyumbani kwa kuwa imeshapata mafanikio ambayo Wazanzibari wanayataka; kuishinda Tanzania Bara.

Kijana huyo anadiriki hata kusema kombe la ubingwa wapewe Bara kwa kuwa kazi ya Zanzibar ilikuwa hiyo moja tu ya kuiondoa Bara. Na maoni yanayofuata baada ya video kutumwa na watu tofauti ni maoni kwamba Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) yafuatilie kinachofanywa na Zanzibar.

Hayo ndiyo maoni ya wengi.

Na unapoiangalia Zanzibar, unaona jinsi ilivyoundwa na wachezaji wanaojituma, wanaofuata maelekezo na wanaopigania Taifa lao kwa udi na uvumba, achilia mbali vipaji vyao tofauti.

Pamoja na hili kuonekana linakosekana kwa timu ya Bara, mimi nimeona kitu cha ziada. Ukiangalia wachezaji tegemeo wa Zanzibar ambao hawakupata nafasi ya kuonekana na timu za Bara, kama Mudathir Yahya, wengi ni ambao wanaonekana kuwa na umri kuanzia miaka 25 kwenda juu.

Si wachezaji kama Mudathir, ambaye alionekana wakati wa michuano ya vijana walio na umri wa miaka 17 ya Copa Coca Cola, yaani walioonekana katika umri mdogo.

Wale wanaoonekana katika umri mkubwa, huja wakiwa na matatizo kidogo na hivyo hawadumu sana na mifano iko mingi. Au kwa maana nyingine, wengi huonekana katika mashindano ya wiki mbili kama Kombe la Chalenji au Kombe la Mapinduzi.

Wachezaji hawa huwika sana kwenye mashindano hayo na viongozi wa mpira huwa kama wamepigwa ganzi na baada ya muda utasikia mara klabu hii imemsajili huyu na nyingine yule na hata makocha wa Taifa Stars kuita wachezaji kutokana na msisimko unaoibuka katiuka mashindano hayo.

Naloliona hapa ni kukosa ufuatiliaji wa wachezaji wa Zanzibar na kuja kustukia wanawika katika mashindano ya wiki mbili, ambayo kwa kawaida si mazuri kutafutia wachezaji.

Kuna haja kubwa ya kuwa na mfumo wa kufuatilia mashindano tofauti visiwani Zanzibar kujaribu kutafuta wachezaji wakiwa katika umri mdogo ili walelewe katika mazingira mazuri ya kuweza kutumika hapo baadaye.

Ni wazi kuwa klabu kubwa kama za Azam, Simba na Yanga huchangia kwa kiasi kikubwa kuwajenga wachezaji kuwa tayari na mashindano na hivyo viongozi na mawakala hawana budi kutupia macho kwa karibu vijana wanaosakata soka Zanzibar.

Kama Morocco ameweza kuwaona nyota wanaosumbua Kenya katika umri huo, kuna uwezekano wa kuwaona nyota hao katika umri mdogo zaidi kama juhudi zitafanyika kuwasaka Zanzibar. Na njia ziko nyingi, lakini iliyo rahisi ni kuangalia mashindano ya visiwa hivyo kila wakati ili tuwapate akina Mudathir wengi.