Tuseme imetosha kwa ajali hizi, tuchukue hatua madhubuti

Jonathan  Musa

Muktasari:

Agosti 22, mabasi mawili ya shule za Nyamuge na Kivulini jijini Mwanza yaligongana na kusababisha kifo cha dereva na kuwaacha majeruhi wengi wakiwa ni wanafunzi. Ilidaiwa kwamba mmoja kati ya madereva wa magari hayo alikuwa amelewa ingawa uchunguzi bado unaendelea.

Kasi ya ajali barabarani inazidi kuongezeka licha ya mamlaka husika kuanzisha mbinu mbalimbali kupunguza kama siyo kuzimaliza kabisa kwa kuwa matukio haya yamegharimu maisha na mali za watu wengi kwa miaka mingi.

Agosti 22, mabasi mawili ya shule za Nyamuge na Kivulini jijini Mwanza yaligongana na kusababisha kifo cha dereva na kuwaacha majeruhi wengi wakiwa ni wanafunzi. Ilidaiwa kwamba mmoja kati ya madereva wa magari hayo alikuwa amelewa ingawa uchunguzi bado unaendelea.

Vilevile magari yaliyokuwa yakisafirisha bidhaa mbalimbali kwenda Rwanbda yaliteketea wilayani Ngara mkoani Kagera baada ya moja ya magari hayo kuyagonga mengine. Ajali hiyo ilisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kujeruhiwa. Mashuhuda walisema mmoja kati ya madereva alikiuka sheria za barabarani.

Kabla ya hapo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alipata ajali mkoani Manyara na kumsababishia majeraha, huku maisha ya mwandishi Hamza Temba yakipotea.

Shadrack Sagati ambaye alikuwa ofisa habari wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji naye yumo kwenye orodha ya wananchi waliokatishwa ndoto zao kutokana na ajali za barabarani. Alifariki dunia akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Geita.

Mwaka jana Taifa liliomboleza vifo vya wanafunzi zaidi ya 30 wa Shule ya St Vincent ya jijini Arusha baada ya gari lao kuhusika katika ajali ya barabarani. Kulingana na sheria za usalama barabarani, kuna madaraja ya madereva na aina ya magari ya kuendesha. Kwa mfano, dereva wa gari au basi la shule anatakiwa kuwa na zaidi ya miaka 35 na kiakili awe sawa.

Hilo halijazingatiwa kwa asilimia 100 hapa nchini, mifano ya kuona na kutajwa ipo ya baadhi ya madereva hususan wa magari ya shule baadhi yao wakiwa na chini ya miaka 30.

Awali Serikali iliwahi kutoa maagizo kwamba hata magari ya Serikali yanayokwenda kinyume na taratibu za barabarani hususan mwendo kasi, yakamatwe na kupigwa faini.

Lakini, utaratibu wa sasa uliopo wa ‘kupigwa tochi’ umezua mijadala maana unaonekana kuelemewa na ajali. Wapo wanaodai unaonea na wapo wanaokiuka sheria na kustahili adhabu lakini haijasaidia kupunguza ajali. Huenda Serikali ingeangalia mfumo mwingine wa kufuatilia magari haya muda wote yakiwa kwenye huduma. Hili lingesaidia.

Kwenye barabara zetu hizi, baada ya kupita au kuiona alama inayoonyesha kilomita 50 kwa saa (KPH), dereva anapaswa kupunguza mwendo, lakini baada ya hapo ataendesha kwa kasi inayozidi maelezo ili kulipiza ile hamsini aliyopunguza muda huo.

Kwa mfano kwenye mikusanyiko ya watu, shule na kona, zimewekwa alama za kumuongoza dereva nini cha kufanya. Alama hizi zipo zilizoandikwa hamsini, kwa maana ya mwendo kasi usizidi hamsini. Kuna alama ya vifusi za kuashiria bumps au matuta na alama nyingine nyingi ambazo ni lazima dereva awe na ufahamu.

Ni dhahiri pia kwamba ajali zina chochewa na abiria. Ni mara chache sana abiria atasikika akihoji mwendo kasi na hata akihoji, hawezi kupata ushirikiano kutoka kwa abiria wenzake. Binadamu tumetofautiana.

Ili kudhibiti haya yote ni vyema Serikali ilete mfumo wa kudhibiti magari yote ya uchukuzi na kwa madereva wa shule wahakikiwe akili na uraibu kabla ya kuanza shughuli za kusafirisha abiria na wanafunzi.

Mbali na mfumo wa ufuatiliaji magari Serikali iongeze adhabu kwa madereva wote wanaosababisha ajali.

Kwa wanunuzi wa magari pia wana kila sababu ya kuchagua ambayo ni bora na nadhifu kwa matumizi sahihi. Matukio ya gari mpya kufeli breki au kwenye mfumo mzima wa injini hapa Tanzania ni mengi.

Hii ina maana kwamba magari mengi yanakuwa tayari yametumika na kuchoka, hivyo yamerudishwa gereji kupigwa rangi kama kiini macho. Serikali nayo iangalie upya barabara zetu ikiwamo alama zilizopo. Zipo ajali zilizosababishwa na ubovu wa barabara au kuwa nyembamba ukilinganisha na mahitaji ya sasa.

Serikali ipitie upya alama zote zilizopo barabarani, inapotakiwa kubadilishwa ifanye hivyo na panapostahili kuwekwa mpya ifanye hivyo. Askari wa usalama barabarani wawe waadilifu katika kuzisimamia sheria na kuwashughulikia madereva wanaokiuka kwa makusudi na pia watoe elimu katika makosa madogo madogo yanayohitaji maelekezo.

+255744205617