Tusiwabebe makandarasi wasio na sifa

Muktasari:

  • Hoja ya Makamu wa Rais ni kuwa watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania, kukuza uwekezaji wa ndani kwa kuwa fedha hizo zitabaki ndani ya nchi.

Akifungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi mwaka 2017, Makamu wa Rais, Samia Suluhu aliagiza miradi yote isiyozidi Sh10 bilioni wapewe makandarasi wa ndani hasa inayotekelezwa kwa fedha za ndani.

Hoja ya Makamu wa Rais ni kuwa watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania, kukuza uwekezaji wa ndani kwa kuwa fedha hizo zitabaki ndani ya nchi.

Lakini pia hiyo ni njia pekee ya kuwaendeleza na kuwawezesha kuingia kwenye ushindani wa zabuni za kimataifa.

Pamoja na uamuzi huo mzuri uliozingatia maslahi mapana ya wawekezaji wazawa, lazima wabanwe kwa kuwa baadhi yao wamechangia kuzorotesha juhudi za Serikali za kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Kwa mfano barabara ya Makutano Natta, Mugumu mkoani Mara hadi Mto wa Mbu mkoani Arusha ambazo kampuni 10 za makandarasi wazawa walipewa kipande cha kilomita 50 tangu mwaka 2013 na kukamilisha mwaka 2015 kwa gharama ya Sh 50 bilioni, mpaka sasa ndio kwanza wanadai wamefanikiwa kujenga kwa zaidi ya asilimia 42.

Kutokamilika kwa wakati mradi huo, kunamaanisha gharama za maisha kwa wakazi wa maeneo hayo zinazidi kupanda kwa kuwa wenye magari hupandisha bei ya nauli na bidhaa kutokana na ubovu wa barabara

Anayetwishwa mzigo huo ni mwananchi ambaye kodi yake imewalipa makandarasi hawa wazawa.

Kwa utendaji huu, nadhani kunachangia kuwafanya wananchi kuichukia Serikali yao, kwa kuwa wanaendelea kupata shida kubwa ya usafiri wao na wa mazao.

Pamoja na utekelezaji mdogo wa mradi, makandarasi hawa wameendelea kutoa ahadi lukuki ambazo pia hawazitimizi. Mathalani, mwaka 2016 walimwahidi Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbawalla kuwa wangekamilisha ujenzi Aprili mwaka huu.

Hadi sasa makala haya yanapochapishwa hata nusu ya hawajafikia;uwekaji lami umefanyika maeneo machache.

Kama kweli tunataka Tanzania ya viwanda ionekane, lazima tuangalie namna ya kupunguza kampuni za kibabaishaji ili zijipange upya, kwa kuwa zinachezea fedha za walipakodi.

Pamoja na kuhimiza Tanzania ya viwanda kila wilaya na mkoa, ikumbukwe hakuna barabara ya lami inayounganisha mikoa ya Mara na Arusha, licha ya kuwapo kwa fursa nyingi za kiuchumi ambazo zingeweza kusaidia kukuza uchumi wa jamii, mkoa na Taifa kwa jumla.

Miundombinu mizuri ina mchango mkubwa kwenye suala la uwekezaji na inachangia kushusha gharama za maisha.

Barabara nzuri inachangia ongezeko la utalii wa ndani kwa wazawa ambao una mchango mkubwa pia kwenye uchumi wa Taifa.

Lakini kutokana na ubovu wa barabara za kuingia na kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mugumu, inakuwa vigumu kuunganisha utalii wa wanyamapori na Ziwa Victoria .

Kama kilometa 50 kampuni 10 zinajenga kwa zaidi ya miaka mitano,kwa utendaji huu wahusika wanasaidia kweli kukuza uchumi?

Nionacho ni ongezeko kubwa la gharama za maisha, kwa kuwa wananchi wanalazimika kulipa nauli kubwa huku bidhaa zikipanda bei.

Nia njema ya Makamu wa Rais inatakiwa kutumika kwa kuangalia zaidi uwezo wao. Na wanaposhindwa kutekeleza kama ilivyopangwa, hatua zichukuliwe haraka ili kampuni zenye uwezo hata kama ni za nje zipewe kazi ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.

Naomba Serikali iwe makini katika utekelezaji wa miradi ya barabara hasa wanayopewa wazawa. Kazi zisitolewe kwa hoja ya uzawa bali uwezo na rekodi zao za utendaji.