Uchunguzi ghorofa lenye nyufa uwekwe wazi

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamdun alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema mbali na uamuzi wa kuwahamisha, wameunda timu ya wataalamu kuchunguza uimara wa jengo hilo kama linaweza kuendelea kutumika bila kusababisha madhara.

Jeshi la Polisi limelazimika kuwahamisha wakazi waliokuwa wanaishi ndani ya jengo la ghorofa 10 lililopo Mtaa wa Mfaume, Upanga jijini Dar es Salaam baada ya kupata nyufa zinazohatarisha uimara wake. Pia, wakazi wa majengo ya jirani nao wamehamishwa kwa usalama wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamdun alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema mbali na uamuzi wa kuwahamisha, wameunda timu ya wataalamu kuchunguza uimara wa jengo hilo kama linaweza kuendelea kutumika bila kusababisha madhara.

Waswahili wana msemo kwamba “Tahadhari kabla ya hatari”. Jengo hilo tayari lina viashiria vya hatari, hivyo uchunguzi utakaofanyika urejee mapendekezo ya Kamati ya Lowassa iliyoundwa mwaka 2006, kuchunguza uimara wa ghorofa za jijini Dar es Salaam.

Akiwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliunda kamati iliyobainisha kuwa zaidi ya nyumba 100 za ghorofa jijini Dar es Salaam zimejengwa chini ya kiwango na nyingine kinyume cha sheria.

Lakini, Machi 2013 jumba la ghorofa 16 liliporomoka wilayani Ilala na kuua watu 36 na uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa sheria zilikiukwa kwa kuwa mchoro wa jengo hilo ulikuwa ni wa ghorofa 10, lakini zikaongezwa sita kinyume na utaratibu.

Kampuni ya utaalamu wa majengo iliyoteuliwa na Manispaa ya Ilala kuchunguza majengo mengine ya ghorofa yaliyopo kwenye manispaa hiyo, ilitoa ripoti iliyobainisha kuwa kati ya majengo 90 yaliyokaguliwa, 67 yaligundulika kuwa yalijengwa chini ya kiwango na kinyume cha sheria.

Mbali na ripoti hizo, pia kuna madai ya rushwa katika sekta ya ujenzi kuwa ndiyo inayosababisha ujenzi hasa wa ghorofa kufanyika bila vibali, kujenga bila kufuata michoro iliyoidhinishwa na baadaye watu kuruhusiwa kuanza kuishi humo kabla ujenzi haujakamilika.

Tunachokiona hapa pamoja na kwamba kisheria madiwani ndio wenye dhima ya kusimamia sera za ukuaji wa miji, kwa hali iliyofikia sasa hasa kwa Jiji la Dar es Salaam, kuna haja ya Serikali kuingilia kati na kurekebisha hali hiyo kwa kuweka mwongozo ambao hautakiukwa na wajenzi.

Ni kweli ujenzi wa ghorofa hauepukiki katika jiji kama hilo kutokana na ukuaji wake wa haraka, lakini ni vyema ujenzi huo ukafuata sheria na maoni ya wataalamu.

Wakati umefika sasa kwa uchunguzi wa majengo yote jijini Dar es Salaam kufanyika ili yale ambayo yatakayoonekana kuwa yanahatarisha usalama wa wananchi, tahadhari zichukuliwe mapema na yale ambayo yana matatizo lakini kunaweza kufanyika marekebisho, utaratibu ufanyike badala ya kusubiri ajali ndipo hatua zichukuliwe.

Pia wale waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi, wafanye kazi yao ipasavyo ili kuepusha ukiukwaji wa sheria na taratibu za ujenzi unaosababisha kuibuka kwa majengo yaliyojengwa chini ya kiwango.

Kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha ujenzi usiofuata sheria, kanuni na taratibu unazuilika iwe ni mmiliki wa jengo, mjenzi, msimamizi wa ujenzi, mshauri au mamlaka za Serikali zinazohusika.

Ndiyo maana tunasema, tunasubiri kuona kazi ya uchunguzi wa jengo hilo ukifanyika mapema na kitaalamu na taarifa yake kuwekwa wazi.