Ujasiri wa Mwalimu Joyce uzibue akili zilizolala

Muktasari:

  • Kilichosababisha mwanadada huyo kutumia maisha yake yote kuwa kitandani ni ajali aliyopata mwaka 1979 akiwa na umri wa miaka minane tu. Mdogo wake alifariki katika ajali hiyo lakini yeye aliachiwa majeraha mgongoni ambayo baadaye iligundulika kuwa pingili ziliachana.

Katika ukurasa wa kwanza wa gazeti hili Jumapili iliyopita tuliandika simulizi ya maisha ya Joyce Kantande, ambaye kwa miaka 18 amekuwa kitandani. Tangu mwaka 1999, maisha yake ni kitandani.

Kilichosababisha mwanadada huyo kutumia maisha yake yote kuwa kitandani ni ajali aliyopata mwaka 1979 akiwa na umri wa miaka minane tu. Mdogo wake alifariki katika ajali hiyo lakini yeye aliachiwa majeraha mgongoni ambayo baadaye iligundulika kuwa pingili ziliachana.

Madaktari walijitahidi kadri ya uwezo wao na pingili hizo zilipoanza kuungana ulijitokeza uvimbe ambao taratibu ulianza kusababisha mawasiliano katika mwili yasiwe mazuri. Bado aliweza kuendelea na masomo ya sekondari na kumaliza kidato cha nne na baadaye kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano na sita.

Huku akiwa na maumivu makali bado alijiunga na chuo cha uhasibu ambako alisomea masuala ya uboharia. Juhudi za kusaka kazi zilikwama kwa kuwa safari nyingi zilikuwa za kusaka matibabu na mara miguu ikaanza kuwa mizito. Siku zilivyozidi kwenda miguu ilimkatalia kuinuka, akajikuta amekwama kitandani hadi leo.

Baada ya kugundua kuwa asingepona tena alikata tamaa, alitamani angekufa aondokane na shida na ugumu wa maisha.

Kwa kuwa akili yake bado ilikuwa inafanya kazi, alitafuta mbinu nyingine. Alianza kufundisha watoto chumbani kwake; alianza na watoto wa ndugu na marafiki na baada ya watoto hao kupata mafanikio ndipo alipofungua darasa ambalo kwa mwaka anapata watoto 50.

Maoni haya hayana lengo la kusimulia upya mkasa uliompata Joyce, maana kuna watu wengi waliozaliwa wazima lakini wakapata ulemavu ukubwani kutokana ama na ajali au magonjwa kama ya kupooza au kiharusi.

Lengo ni kutaka jamii ijifunze kutokana na ujasiri wa Joyce katika kukabiliana na changamoto iliyomkuta maishani kutokana na ajali. Kwamba hakutaka kuridhika na hali aliyonayo na wengine wangeweza kutumika kama kitegauchumi cha familia – kuchukuliwa na kuzungushwa barabarani kuomba msaada.

Mwalimu Joyce hakutaka kukabiliana na maisha kwa njia hiyo ya kuombaomba, bali ametumia akili yake, elimu yake, na ujuzi mpya.

Ndiyo maana tunahoji watu wanaolalamikia ugumu wa maisha wanatumia kigezo kipi? Maana watu wengi wanaolalamika wamelaza akili. Vijana ambao akili zao zimelala hukimbilia kupiga debe au kuomba fedha kwa mtindo wa “niungishie” na kubwia dawa za kulevya.

Wengine ambao akili zao zimelala ni wanaotaka ajira za ofisini tu. Pia, wengine ambao akili zimelala ni wanaolalamika kwamba wamepangiwa kazi maeneo ambayo wanadai hayaendani na hadhi yao au hayawapi uhuru wa kufika mjini na wapo wanaolalamika kukosa kazi za masomo waliyosomea.

Je, kama akili ya Mwalimu Joyce ingelala maisha yake yangekuwaje kitandani? Kama Joyce angefikiria hadhi, eneo la kuzunguka, masomo aliyosomea kwa vyovyote asingeweza kufanya kazi. Bila shaka anawasuta wote wanaonung’unika maana yeye alisomea uhasibu lakini ametumia akili kufanya kazi ya ualimu, tena kitandani chumbani ambako hawezi kutembeatembea na watoto wanafurahia kazi yake.

Tunatoa wito kwamba simulizi ya maisha ya Mwalimu Joyce iwazibue akili vijana, walemavu na hata wazee kutafuta njia ya kupambana na changamoto za maisha kadri zinavyojitokeza.

Aidha, jamii na Serikali waone ni namna gani wanaweza kuwasaidia watu wa aina ya Mwalimu Joyce ili watumie ujuzi wao kutoa mchango wao katika kulijenga Taifa.