Ukuta wa Mirerani uwe mwanzo wa manufaa ya tanzanite

Muktasari:

  • Pamoja na mambo mengine, aliliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kujenga ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite yanayopatikana nchini ili kukabiliana na utoroshwaji unaofanywa.

Septemba 20, akiwa kwenye ziara ya kikazi wilayani Simanjiro, Rais John Magufuli alizindua barabara yenye urefu wa kilometa 26 inayotoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro hadi Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani.

Pamoja na mambo mengine, aliliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kujenga ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite yanayopatikana nchini ili kukabiliana na utoroshwaji unaofanywa.

Tangu serikali ya awamu tano iingie madarakani imemua kuzilinda rasilimali za taifa ili zitumike kwa ajili ya maslahi ya Watanzania kwa kudhibiti mianya ya udanganyifu ikiwamo ukwepaji kodi.

Wakati ikiwa fahari kwenye nchi zilizoendelea kulipa kodi, hali ni tofauti katika mataifa yanayoendelea ambako ukwepaji ni jambo la kawaida wakati mwingine wakwepaji hupongezwa kwa ujasiri na mbinu ovu wanazotumia kuhakikisha hawatekelezi wajibu huo. Hata baadhi ya wananchi wasiofahamu faida ya kulipa kodi huwapongeza watu hao.

Kimsingi, hoja na kelele za muda mrefu ambazo zilikua zikielekezwa kwenye matumizi sahihi ya rasilimali zetu zimesikika kwa kuhakikisha utekelezaji wa haraka unafanyika ili keki hii adhimu iwanufashe wananchi wote kwa huduma bora za elimu, afya, maji na ujenzi wa miundombinu.

Ipo mifano ya baadhi ya nchi zilizonufaika zaidi na madini ya Tanzanite zikiwamo India, Afrika Kusini, Thailand na Kenya lakini wananchi waliopo eneo yanapotoka madini hayo wakiwa taaban kwa sababu ya miundombinu ya kuwawezesha kunufaika kutokuwekea udhibiti.

Nipongeze hatua za makusudi na uzalendo zilizochukuliwa na Rais Magufuli kujenga ukuta utakaotumika kudhibiti utoroshwaji na kuchangia serikali kukosa mapato yanayotakiwa kisheria.

Lengo la serikali yeyote duniani ni kuhakikisha inaweka mazingira rafiki kwa wananchi wake pamoja na wawekezaji kutumia fursa zilizopo kwa mujibu wa sheria kufanya biashara halali ili serikali ikusanye kodi na wafanyabishara wanufaike kupitia kazi zao.

Kama sheria inavyotamka kuwa madini ya vito yachimbwe na wenyeji, hili ni jambo la kizalendo kwani linalenga kufanya wananchi wamiliki uchumi wao badala ya kuwa wafanyakazi kwenye migodi inayosimamiwa na kampuni kubwa za uchimbaji duniani.

Hatua ya serikali kukabidhi machimbo ya Tanzanite kwa wazawa ni jambo linalotakiwa kupongezwa kwani faida yake ni kubwa ikilinganishwa na iliyokuwa inapata wakati eneo hilo likiwa chini ya wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Faida muhimu ni kuwa wazawa watatumia faida wanayopata kuanzisha biashara mpya ambayo itaongeza mapato ya serikali kupitia kodi lakini wananchi watapata ajira ambazo kila mara zimekuwa changamoto.

Ni imani yangu serikali itatumia busara kupata njia zinazofaa kuwajengea uwezo wawekezaji wazawa kumiliki uchumi wao bila kujali rangi, eneo wanakotoka, kabila au itikadi za kisiasa.

Ukuta huo unaojengwa kuzunguka eneo lenye utajiri mkubwa Afrika una urefu wa kilometa 24.5. Hili ni eneo kubwa litakalohitaji nguvukazi ya kutosha ambayo kwa mujibu wa kamanda wa opereshi ya ujenzi wa ukuta huo, Kanali Festus Mang’wela; vikosi 20 vya askari wa JKT vipo tayari kwenye eneo la mradi.

Huu ni wakati muafaka kwa wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na huduma nyingine za ugavi kukamata fursa katika matumizi ya Sh 4.8 bilioni zilizotengwa kukamilisha mradi huo.

Filbert ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha. Anapatikana: 0754 945 670