Thursday, October 12, 2017

Upo umuhimu mkubwa kulitunza Pori Tengefu la Loliondo

Hamza Temba  ni ofisa habari wa Wizara ya

Hamza Temba  ni ofisa habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii. 

By Hamza Temba

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni miongoni mwa vivutio maarufu vya utalii duniani unaotokana na misafara ya nyumbu wanaohama kwa makundi makubwa.

Licha ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, nyumbu hawa pia hupita Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba Maswa, Ikorongo na Grumeti pamoja na Hifadhi ya Maasai-Mara ya Kenya.

Zaidi ya nyumbu milioni moja, pundamilia laki mbili na swala laki tatu hujumuika kwenye msafara huu wa kutafuta malisho na maji. Uhamaji wao umeipa sifa hifadhi hiyo hata kuwa moja ya maajabu saba ya asili ya barani Afrika.

Pamoja na umaarufu huo, uhai wa Serengeti unategemea zaidi ustawi wa Pori Tengefu Loliondo ambalo lilianzishwa mwaka 1959 likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 4,000. Lipo katika tarafa za Loliondo na Sale wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.

Kabla ya mwaka 1992 eneo hili ambalo pia ni kitalu cha uwindaji lilitumiwa na Shirika la Serikali la Wanayamapori (Tawico) na baadaye Kampuni ya OBC (Ortello Business Corporation) ikakabidhiwa kwa ajili ya uwindaji.

Katika pori hili kuna makazi, kilimo na ufugaji. Aidha, shughuli za uhifadhi wa wanyamapori, uwindaji wa kitalii na utalii wa picha pia hufanyika.

Tangu miaka ya 1990, eneo hili linakabiliwa na mgogoro unaohusisha wananchi wa Tarafa ya Loliondo, viongozi wa kisisasa, muwekezaji, Serikali na makundi mengine ya kijamii.

Takwimu za hifadhi hiyo zinaonesha mifugo 3,746 imekamatwa mwaka huu na watuhumiwa kutozwa faini ya Sh131 milioni.

Sababu nyingine iliyochochea mgogoro huo ni utaratibu wa baadhi ya viongozi wa kimila kuwaruhusu Wamasai wa Kenya (hasa Koo za Purko, Loitana Kisongo kwenye vijiji vya Ololosokwan, Kirtalo, Mondoros, Oloipiri, Arash, Mbukeni, Piyaya, na Malambo) kuhamishia mifugo yao ndani ya pori hilo hasa msimu wa kiangazi.

Changamoto nyingine ni uwepo wa mpaka wa wazi kati ya Tanzania na Kenya ambao unarahisisha wafugaji kuingia porini humo hadi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kufuata malisho. Kati ya Machi na Mei, wafugaji 175 kutoka Kenya wakiwa na mifugo zaidi ya 31,371.

Kilomita za mraba 2,500 zitakazosalia zitabaki kwa ajili ya matumizi ya wananchi, Lengo ikiwa ni kuwezesha jamii kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kuboresha maeneo ya malisho ya mifugo na makazi.

Wingi wa mifugo umesababisha mabadiliko ya uoto wa asili hivyo kuchangia uhaba wa malisho kwa wanyamapori na mifugo. Ukosefu wa malisho husababisha wananchi kuingiza mifugo hifadhini. Kutenga eneo hili kutatoa fursa ya kuimarisha malisho ya wanyamapori pamoja na mifugo.

Kwa miaka 10, Hifadhi ya Serengeti ambayo hutoa asilimia 41.6 ya mapato yote ya Tanapa, imechangia Sh537.12 bilioni. Mwaka uliopita wa fedha, Mamlaka ya Ngorongoro ilichangia Sh102 bilioni katika mfuko mkuu wa Serikali. Asilimia 80 ya mapato haya hutokana na utalii wakati mifugo ikichangia asilimia sita. Sekta ya utalii kwa ujumla inachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Zipo juhudi za kuondoa mifugo hifadhini humo. Tangu zilipoanza Agosti, maboma (ronjoo) 327 yamevunjwa. Kati ya hayo, maboma 86 yalikutwa ndani ya Hifadhi ya Serengeti huku 241 yakiwa katika mpaka wa Pori Tengefu Loliondo. Wafugaji wengi walihama kwa hiari kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Baadhi ya maboma hayo yalikutwa na pikipiki zenye namba za usajili za Kenya ambazo ni dalili kuwa maboma hayo yalikuwa yakikaliwa na wahamiaji haramu kutoka nchini humo.

Katika kipindi kifupi, maeneo yaliyosafishwa yameanza kurejea kwenye uoto wake wa asili ikiwamo vyanzo vya maji na mito. Hata wanyamapori wanarejea kutokana na kutopata usumbufu kutoka kwa wafugaji na mifugo.

Wakazi wengi wa Loliondo wakiwemo viongozi na watu kutoka vijiji vya Maalon, Oloipiri, Olerian, Wasso, Kirtalo na Piyaya wameunga mkono suala operesheni hiyo ambayo haikuwa na usumbufu.

Utalii ni sekta nyeti kwa uchumi na Pato la Taifa hivyo kila kivuti kinapaswa kulindwa kw anguvu zote. Wananchi wanatakiwa kushiriki kwenye hili kwa sababu wao huyazunguka maeneo ya vivutio hivi.

Kila mdau mwenye uwezo na nafasi ya kutoa elimu juu ya suala hili asisite kufanya hivyo ili kuwahamasisha wadau wote kuelewa na umuhimu wa kuvitunza vivutio tulivyonavyo.

Bodi ya Utalii nchini (TTB) imeanzisha kampeni ya kutangaza utalii wa kanda ya kusini kwa dhamira ya kukuza sekta hiyo maeneo hayo.

Mwandishi ni ofisa habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

-->