Ushauri wa Profesa Tibaijuka ufanyiwe kazi

Muktasari:

  • Kwa baadhi ya maeneo kama ya Mkoa wa Dar es Salaam, imekuwa kama desturi kwamba mvua kubwa zinaponyesha wala hupasui kichwa kujua ni wapi ambako kadhia hii itakuwepo. Maeneo ya Jangwani, Tazara na eneo lote la bonde la Mto Msimbazi, Tegeta na Akiba yanajulikana kwamba shida mvua zinaponyesha.

Siku tatu zilizopita maeneo mengi ya Tanzania, kama taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilivyokuwa imetabiri, yalipata mvua zilizokuwa juu ya wastani, hali iliyosababisha maafa kama vifo, pia uharibifu wa miundombinu na wananchi wengi kukosa makazi.

Kwa baadhi ya maeneo kama ya Mkoa wa Dar es Salaam, imekuwa kama desturi kwamba mvua kubwa zinaponyesha wala hupasui kichwa kujua ni wapi ambako kadhia hii itakuwepo. Maeneo ya Jangwani, Tazara na eneo lote la bonde la Mto Msimbazi, Tegeta na Akiba yanajulikana kwamba shida mvua zinaponyesha.

Lilikuwapo eneo jingine la Mbezi Mwisho, lakini hili, pongezi ziwaendee wahandisi kwa kumaliza adha yake baada ya ukarabati mkubwa uliofanywa katika Daraja la Mto Mbezi kwa kuwa mvua za safari hii hazikusababisha adha yoyote kama ailivyokuwa wakati watu walpokuwa wakiripotiwa kufariki.

Kumekuwa na maswali mengi ya kwa nini hali hii ya mafuriko katika maeneo hayo haipatiwi ufumbuzi ilhali tunao wataalamu na ambao baadhi yao ni waathirika wa tatizo hilo?

Jana, Profesa Anna Tibaijuka alituma waraka ambao ulisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii akichambua sababu na kutoa ushauri ambao tunaamini kwamba ukizingatiwa, tunaweza kumaliza shida hii ya kila msimu wa mvua kubwa.

Kubwa alilosisitiza waziri huyo wa zamani wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi ni umuhimu wa kuheshimu mipango miji, akisema tatizo si mvua kubwa, bali kuziba mfumo wa asili wa mifereji hivyo maji ya mvua kushindwa kwenda baharini.

Anafafanua kwamba Bonde la Msimbazi ndiyo njia pekee kwa maji yote yatokayo Pugu, Ukonga Uwanja wa Ndege, Tazara, Tabata, Kigogo, Magomeni na Ilala kufika Jangwani na kuendelea na safari hadi Daraja la Salender yanapoingia baharini.

Pia, anabainisha kuwa njia ni hiyo tu moja kwa maji kutoka Ubungo, Manzese, Tandale, Magomeni Kagera, Kinondoni Hananasif, Muhimbili hadi Jangwani. Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mto Mbezi na Mto Mlalakuwa na Mto Mdumbwi (Kawe) kuna makazi ya watu hivyo njia za maji kuelekea baharini kuzibwa.

“Huhitaji kuwa mtaalamu wa mipango miji kufahamu kuwa maji yanafuata mkondo wake na kwamba katika baadhi ya miaka, mvua kubwa lazima itanyesha. Mambo yote haya yanatabirika,” anasema.

Alitoa mfano wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) ambao kituo chake kikuu kimejengwa Jangwani akisema uharaka wa kuukamilisha ulisababisha kutozingatiwa kwa masuala mengine ya kitaalamu.

Alisema bila ya kuwapo kwa utashi wa kisiasa, ujuzi na weledi wa wataalamu utapotea bora. Alisema ameona aelezee hili kwa watu wanaotaka kujua sababu za wataalamu kutufikisha hapa. Lakini anasema si wataalamu, bali utamaduni wa kutoheshimu utaalamu na wananchi kutaka suluhisho la haraka.

Alishauri kurejewa kwa mipango miji ya mwaka 1979 wa kutengeneza bustani katika eneo Bonde la Msimbazi na kuwalipa fidia waliojenga kama wanastahili na kisha kuzuia uendelezaji mpya holela.

Tunadhani, ushauri wa Profesa Tibaijuka hasa ikizingatiwa ufahamu wake usiotiliwa shaka wa masuala ya makazi, utazingatiwa na kufanyiwa kazi na Serikali ili kuokoa maisha na mali za wananchi hawa ambao wengi wao ni wa kipato cha chini.