Usimamizi mbovu wa maji utaliangamiza Taifa

Muktasari:

  • Matumizi mazuri ya ‘damu’ hii yanatuhakikishia uhai na ustawi wa Taifa letu. Bila uhakika wa maji, taifa litakuwa kama mwili usiokuwa na damu. Tutaangamia.

Maji ni damu ya taifa lolote lile duniani. Katika Bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni, wabunge wote bila kujali itikadi zao, walisimama kidete wakitaka Serikali iwape uhakika wa maji wananchi.

Matumizi mazuri ya ‘damu’ hii yanatuhakikishia uhai na ustawi wa Taifa letu. Bila uhakika wa maji, taifa litakuwa kama mwili usiokuwa na damu. Tutaangamia.

Nilichokibaini ni kuwa nchi yetu ina udhaifu katika usimamizi wa maji; tusipochukua hatua tutaangamia.

Shughuli zinazohusu matumizi ya maji majumbani, kwenye kilimo, viwanda, uchimbaji wa madini na uzalishaji umeme unategemea usimamizi mzuri wa maji.

Taasisi za usimamizi wa maji nchini haziwajibiki ipasavyo katika mgawanyo wa maji, kudhibiti uharibifu wa vyanzo vya maji, kupungua na kuisha kwa maji.

Usimamizi mbovu wa maji umesababisha kupungua kwa maji na migogoro ambayo dhahiri inakwamisha vita dhidi ya umasikini na kuwa kikwazo dhidi ya uwekezaji na ukuzaji wa mitaji.

Kubadilisha mfumo wa usimamizi kutoka usimamizi kimikoa kwenda katika mamlaka za mabonde, bado hakujaleta tija na vipaumbele vyake havijawa wazi.

Mamlaka za mabonde hazina budi kutoa kipaumbele na kufanyia kazi kwa haraka uharibifu wa mazingira usiodhibitiwa.

Athari za uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na taka za majumbani na taka za viwandani, zinajulikana.

Japo uchafuzi wa mazingira ni kosa kisheria na mamlaka za mabonde na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), zina mamlaka kamili ya kusimamia utekelezaji wa sheria hizi, uchafuzi umeachwa utambe na kuchafua maji yetu.

Uchafuzi wa Mto Ngerengere mkoani Morogoro na Mto Msimbazi Dar es Salaam ni mifano sugu ambayo suluhisho la uhakika bado halijapatikana huku uharibifu ukiendelea.

Kuhakikisha mgawanyo sawa na wa haki miongoni mwa watumiaji kwa kutoa vibali vya matumizi ya maji ni jukumu msingi la bodi za mamlaka ya mabonde.

Mtumiaji maji anapaswa kupata kibali cha kisheria kutoka bodi ya mamlaka ya bonde ya eneo lake kitakachoonyesha jinsi atavyoweka miundombinu ya maji kwa ajili ya matumizi endelevu.

Pamoja na kuwa na jukumu hilo mamlaka za mabonde zimeshindwa kutoa vibali kwa waombaji wengine zaidi ya miaka saba tangu walipoomba.

Pia kuna miradi mikubwa ya umwagiliaji inafanyika pasipo kuwa na vibali kutoka mamlaka za mabonde husika.

Kama sheria inatamka kuwa kisima kilichochimbwa zaidi ya mita 15 au kinachotumia miundombinu ya kusukuma maji kinatakiwa kiombewe kibali, kuna watu wangapi katika mkoa kama Dar es Salaam waliovunja sheria na wako katika hatari ya kuadhibiwa kwa kulipishwa faini na kifungo bila wao kufahamu?

Ili tuwe na usimamizi imara utakaotupa taifa letu uhakika wa maji, ni lazima kwanza tuwe na uratibu imara wa makundi mbalimbali yenye maslahi katika utumiaji na usimamizi wa maji.

Jumuiya za watumiaji maji ni kiungo muhimu katika taaluma ya usimamizi wa maji, lakini umuhimu wao nchini mwetu bado haujaonekana. Muda umefika wa kuimarisha makundi haya.

Pili, tuwe na wataalamu wa kutosha wanaopewa motisha. Malalamiko ya upungufu wa wataalamu kutoka bodi za mamlaka za bonde kiasi cha kuwa kisingizio cha wao kukosa ufanisi, yasipuuzwe.

Aidha, yatupasa tuwe na uratibu mzuri wa kitaasisi, fedha za kutosha na kuwa na mifumo iliyo wazi ya uwajibikaji na udhibiti wa fedha.

Kuna mawasiliano hafifu baina ya bodi za mamlaka ya bonde na wadau na wakala wengine wanaohusiana nao kama vile Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), NEMC, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati na Madini, hasa kuhusu wawekezaji.

Uwekezaji umekuwa ukifanyika katika maeneo yenye uhaba wa maji, hivyo kusababisha maji kuisha na kuanzisha migogoro ambayo ingeweza kuepukika. Serikali inapaswa itambue kwa dhati umuhimu wa maji hivyo kuimarisha usimamizi wa ‘damu’ yetu ili tuwe na uhakika wa maisha, kwani uhakika wa maji ni uhakika wa maisha.

Katika mpango wa kwanza wa Maendeleo ya Sekta ya Maji, Serikali yetu haikuonyesha nia ya dhati katika usimamizi wa maji, kwani mpango wa usimamizi wa maji ulipata asilimia tano tu ya bajeti yake.

Katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali ilitenga Sh 915.1 bilioni; lakini fedha zilizotolewa kufikia Machi mwaka huu ni Sh 184.1 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 19.8 ya bajeti.

Maji ndio damu ya taifa letu. Tusipojirekebisha na kuchukua hatua tutajiangamiza sisi wenyewe. Kila mmoja wetu ajitoe kusimamia uhai wa taifa letu kwa kuhakikisha maji yanapatikana.

0713593797