Utamaduni ndiyo msingi wa maisha na maendeleo

Muktasari:

Najua tutatofautiana mawazo lakini naamini tutafika pazuri na kuafikiana. Nafanya hivi kwa faida ya kizazi cha sasa ambacho vijana wengi walizaliwa baada ya Azimio la Arusha, mwaka 1967; kipindi ambacho dhana hii iliibuliwa na kujadiliwa katika majukwaa ya kisiasa nchini.

Nimelazimika kuandika makala haya ili kutoa ufafanuzi kuhusu dhana ya ujamaa kwa kadri ya uelewa wangu baada ya kupata ukakasi kila niliposikia mjadala kuhusu siasa au itikadi ya Tanzania kutoka kwa wachambuzi mbalimbali.

Najua tutatofautiana mawazo lakini naamini tutafika pazuri na kuafikiana. Nafanya hivi kwa faida ya kizazi cha sasa ambacho vijana wengi walizaliwa baada ya Azimio la Arusha, mwaka 1967; kipindi ambacho dhana hii iliibuliwa na kujadiliwa katika majukwaa ya kisiasa nchini.

Japokuwa, ujamaa ulikuwepo tangu enzi za mababu, karne nyingi kabla ya kuwasili kwa wamisionari wa kwanza na wafanyabiashara kutoka mashariki ya kati na ya mbali, Azimio la Arusha liliongeza mjadala wake.

Neno ujamaa limetokana na neno jamaa au jamii. Linahusu mfumo mzima wa maisha, taratibu, mila na desturi, kanuni, misingi, miiko na taswira nzima ya utamaduni wa maisha baina ya jamaa katika jamii husika. Na hapa, nazungumzia jamii ya Kitanzania.

Mwalimu Julius Nyerere alipokabiliwa na changamoto za kulijenga upya taifa lenye makabila yasiyopungua 120, kila moja likiwa na lugha yake na mfumo wake wa maisha; alihitaji ‘utamaduni wa kijamaa’ kufanikisha jukumu hilo.

Pamoja na kuwapo kwa tofauti nyingi za kimila, desturi na lugha baina ya makabila yote hayo, kitu kimoja kilichokuwamo ndani ya kila kabila miongoni ni utamaduni wa maisha ya kijamaa.

Baada ya tafakuri ya kina, Mwalimu Nyerere alibaini mapema kwamba, kabla ya kuzungumzia masuala ya maendeleo au kurahisisha namna ya kuleta maendeleo ya nchi katika nyanja zote, ni lazima kuyaleta makabila yote pamoja na kuwa kitu kimoja. Kuijenga upya Tanzania itakayokuwa na utamaduni mmoja na lugha moja.

Nyenzo muhimu katika kujenga taifa litakalotanguliza utaifa mbele kabla ya mambo mengine binafsi, ni lugha na utamaduni mmoja wa Kitanzania.

Lugha itarahisisha mawasaliano baina ya makabila mbalimbali na utamaduni utasaidia kuyaleta makabila yote 120 pamoja na kuwa kitu kimoja. Ndipo utakapoweza kuweka malengo ya kitaifa katika maendeleo ya maisha ya wanajamii kwa pamoja.

Ili kufanikisha azma hiyo, Mwalimu Nyerere aliitumia vilivyo fursa iliyokuwapo mbele yake ya kutoa nafasi kwa Kiswahili kustawi na kushamiri kila pembe au kona ya nchi bila ya vipingamizi au masharti yoyote.

Lugha hii iliyoanza kuendelezwa na Watanzania mashuhuri na wabobezi wa akiwamo Shaaban Robert, ilipata mchepuo mpya wa kustawi zaidi chini ya uongozi na uangalizi wa Mwalimu Nyerere wakati huo akiwa ndiye muasisi wa taifa huru.

Hakuifanya kazi hiyo peke yake, chini ya uongozi wake, Kiswahili kilistawi nchini na kuvuka mipaka kwenda ulimwenguni kote.

Utamaduni wa taifa ndiyo msingi wa maisha na maendeleo ya nchi. Ndiyo uliweza kuyaunganisha makabila yote nchini, ujamaa.

Kwa bahati mbaya nikiri kwamba, utamaduni huu wa ujamaa baada ya kuibuliwa na Mwalimu haukupata vichwa vya kuutolea ufafanuzi wa kina na kuuendeleza kifikra ili uweze kuchukua nafasi yake stahiki kama mwongozo wa maisha ya kila siku ya Watanzania, kizazi hadi kizazi.

Kama nilivyosema awali, ujamaa siyo itikadi ya kisiasa, bali ni utamaduni wa Kitanzania japo ulifananishwa kimakosa na usoshalisti. Wenyewe ni nyenzo muhimu katika kutoa dira na mwelekeo wa mila na desturi, taratibu za maisha, nidhamu ya kazi na mfumo wa maisha ya jamii.

Ndiyo nguzo muhimu katika kuhakikisha itikadi yoyote ya kisiasa itakayopata nafasi ya kuongoza na kusimamia kanuni na taratibu za uzalishaji mali katika nchi, inajiwezesha ili isikinzane na utamaduni wa taifa.

Itikadi zinazofahamika zaidi duniani ni pamoja na usoshalisti, ukomunisti, usoshalisti wa kidemokrasia, uliberali, ubepari, na ubepari uliokithiri.

Kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kisiasa yaliyopatikana ulimwenguni, njia bora ya kuyaendeleza na kuyasimamia kwa tija maendeleo hayo ni mfumo wa utawala wa demokrasia ya vyama vyingi vya siasa na utawala bora utakaozingatia Katiba ya nchi.

Kila chama cha siasa huchagua aina ya itikadi itakayoona inafaa na yenye manufaa kwa taifa lakini hakuna chama chenye fursa ya kuwachagulia wananchi aina ya utamaduni utakaowafaa.

Kazi hiyo ilishafanywa na muasisi wa taifa hili. Itikadi ya kisiasa itakayoshindwa kuleta matunda yaliyotarajiwa ni rahisi kujaribu aina nyingine lakini utamaduni wa taifa ukigeuzwa kuwa itikadi, utakapofeli kuleta manufaa yaliyotarajiwa, hakutakuwa na mbadala. Taifa litaparaganyika.

Pamoja na kila kinachoendelea, maisha ya wananchi yataimarika kukiwa na uchumi imara unaotokana na kukua kwa shughuli za uzalishaji.

Biashara ni nyenzo ya kufanikisha hili hivyo ni muhimu ikawekewa mazingira mazuri ya kushamiri.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya uchumi; 0683 555 124.