Vijana igeni mfano wa mastaa kupima VVU ili mtambue hali zenu

Muktasari:

  • Mnamo Novemba 17, 2016 mwigizaji maarufu Charlie Sheen alikuwa akihojiwa katika kipindi maarufu nchini Marekani kiitwacho “Today Show” alikiri hadharani kuwa anaishi na virusi vya Ukimwi.

Kuna baadhi ya nukuu za Mwalimu Julius Nyerere zinazopatikana katika kitabu chake kiitwacho “Tujisahihishe” kilichotoka Mei, 1962 kuhusu tofauti ya elimu na kuelimika. Bado zinaishi hadi leo.

Mnamo Novemba 17, 2016 mwigizaji maarufu Charlie Sheen alikuwa akihojiwa katika kipindi maarufu nchini Marekani kiitwacho “Today Show” alikiri hadharani kuwa anaishi na virusi vya Ukimwi.

Alikiri kuwa alitumia fedha nyingi kuwalipa watu ili wamtunzie siri hiyo na kitendo hicho cha kuwalipa watu fedha alikiita makosa makubwa.

Mbali na Sheen, mwigizaji Rock Hudson anatajwa kuwa staa wa kwanza kukiri hadharani kuwa anaishi na virusi vya Ukimwi baada ya kufikia uamuzi huo Julai 25, 1985.

Staa huyo wa “Pillow Talk” alifariki akiwa na umri wa miaka 56.

Katika orodha ya watu maarufu ambao walikiri hadharani kuishi na VVU pia yupo mcheza kikapu wa zamani wa timu ya kikapu ya nchini Marekani ya Los Angeles (LA), Earvin “Magic’ Johnson aliyestaafu rasmi 1991 kushiriki ligi hiyo.

Kabla ya kustaafu aliuambia umma kuwa anaishi na virusi vya Ukimwi.

Hao ni mastaa wachache miongoni mwa wengi waliokiri hadharani kuishi na virusi vya Ukimwi.

Kwa bahati nzuri mastaa hao ni wanaume, inamaanisha walipima na kujua hali zao kabla ya kujitokeza hadharani na kukiri, huku wengi wao wakiwa na lengo la kuhamasisha wengine kupima na kutambua hali zao.

Tanzania inapambana na changamoto ya kuwahamasisha wanaume kupima virusi vya Ukimwi ili kutambua hali zao.

Kibaya zaidi hata waliopima na kutambua hali zao bado ni wagumu kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU na wakinywa hawafuati maelekezo ikiwamo mwendelezo wa matumizi sahihi ya dawa hizo.

Sitaki kuamini kuwa bado hawaamini kama kuna maradhi hayo kwa sababu hata wao wamekutwa nayo au kama hawajapima wanaona dalili zinazotajwa kuwa mwenye maradhi hayo anazo.

Mbali na mapambano dhidi ya wanaume kundi lingine linalohitaji elimu na kuiga mfano wa mastaa hao ni vijana.

Kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 hasa wa kike limetajwa kuwa ndilo kundi kubwa zaidi lililopo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi na linapaswa kupewa kipaumbele cha uelewa.

Utafiti uliofanywa mwaka 2012 Tanzania Bara ulionyesha vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ndio walioongoza kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Nachotaka kusema hapa ni kuwa ili kijana ubaki salama zaidi inakupasa kupima na kujua afya yako, ili iwe rahisi kujikinga na magonjwa nyemelezi ambayo mara nyingi husababisha udhaifu na hata vifo.

Hakuna haja ya kuogopa kupima ugonjwa huo kwa kudhani utaonekana mjinga kwani anayepima na kujua afya yake ni shujaa zaidi kwa sababu ana nafasi mbili za kujilinda.

Kwanza, iwapo atakuwa hajaambukizwa atakuwa na nafasi ya kuchukua hatua za kujilinda ili asiupate na pili, kama ameambukizwa atachukua hatua asiambukize wengine na asipate maambuziki kutoka kwa mtu mwingine ambayo wataalamu wanasema ni hatari.

Shime vijana jitokezeni kupima ili kuokoa kizazi kilichopo na kijacho kupata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Vijana fuateni kaulimbiu isemayo “Furaha Yangu Pima, Jitambue, Ishi.”