Vinywaji lishe chakula bora kwa wagonjwa

Muktasari:

DOKEZO

Angalizo, kila mtu anaweza akatumia chakula hicho ila  watu wenye mzio wa soya au maziwa hawatakiwi kukitumia kwakuwa kimetengenezwa kwa bidhaa hizo kwa kiwango kikubwa, hivyo wanaweza wakapatwa na matatizo ya mzio ikiwamo mwili kuwasha, mdomo kuwaka moto kama mtu aliyekula pilipili, kichefuchefu na kutapika, kukumbwa na mafua ghafla, kizunguzungu au hata kubanwa na kifua kama maumivu ya ugonjwa wa pumu. Ukiona dalili hizo sitisha matumizi ya chakula hiki na haraka nenda ukamuone daktari ambaye atakupa msaada.

Bila shaka umeshawahi kuugua japo ugonjwa wa malaria tu ukiachilia mbali wengi waliougua kwa muda mrefu hadi kufikia hatua ya kulazwa hospitalini kwa maradhi ya aina tofauti.

Lakini tukumbuke kuwa maisha ni safari yenye changamoto nyingi ikiwamo ya magonjwa. Ila je, unakumbuka jinsi ulivyokosa hamu na nguvu ya kula chochote ulicholetewa na mtu aliyewahi kukuuguza?

Hali ya kukosa hamu ya kula humtokea kila mgonjwa ndiyo maana watu wenye jukumu la kuuguza wagonjwa hospitalini au nyumbani hupatwa na changamoto ya kuhakikisha amepata chakula cha kutosha kwa kuwa asipokipata cha kutosha, hali yake hudhoofu siku baada ya siku na hatimaye hupoteza maisha.

Na wakati mwingine si kwa ukubwa wa ugonjwa anaougua bali ni kutokana na mwili kushindwa kupambana na maradhi anayougua kwasababu ya njaa.

Kwa Tanzania, hili ni tatizo kubwa wagonjwa hupoteza maisha kwa kuwa wengi wao wanaowauguza hawajui kitaalamu mgonjwa anahitaji lishe ya aina gani ili aweze kumudu matumizi ya dawa anazopewa na madaktari ambazo nyingi huwa kali, humchosha mgonjwa na kugeuka sumu mwilini.

Kitaalamu kama unamuuguza mgonjwa na hana hamu ya kula chakula, unatakiwa umnunulie chakula maalumu ambacho atakunywa glasi moja tu kwa siku ambayo ni sawa na  milo yote mitatu kwa siku.

Ukiingia katika maduka ya dawa au yale makubwa ya vyakula, kuna aina nyingi tofauti za vyakula hivyo ambavyo ni aina ya maziwa ya unga yaliyoshindiliwa virutubisho takriban vyote vinavyopatikana kwenye vyakula vya kawaida.

Mgonjwa akikorogewa glasi moja tu na akanywa akaimaliza, inamfanya awe katika hali njema na ataweza kutumia dawa bila wasiwasi na itamsaidia kupona  haraka kuliko yule ambaye hapati chakula cha aina hiyo.

Kitaalamu vyakula hivyo huitwa ‘Nutritional Supplement Drink’ kinapatikana kwa majina mbalimbali ya kibiashara madukani.

Kinavyofanya kazi mwilini

Kutokana na wengi kutojua namna chakula hicho kinavyofanya kazi mwilini, wanakiita ‘dawa’ baada ya kuona mgonjwa aliyelala kwa kukosa nguvu ya kuamka kwa muda mrefu alipotumia tu chakula hicho kwa siku tano hadi 10 akinyanyuka na kuweza kuzungumza na hata kwenda msalani mwenyewe bila msaada, basi hujua ni dawa.

Wengi huona kama maajabu, lakini ndiyo teknolojia mpya duniani kote na ndiyo maana watu wengi hukimbilia kutibiwa nchi zilizoendelea kwani huko  wataalamu wa lishe (Nutritionist) ni wengi na wameajiriwa kwenye hospitali na hushiriki kikamilifu kuhakikisha afya za wagonjwa hazitetereki wanapotumia dawa kali.

Chakula hiki kimetengenezwaje?

Ni mkandamizo wa virutubisho (macronutrients) vya protini, wanga, sukari   na mafuta.

Kimetengenezwa maalumu kuwa mbadala wa chakula cha kawaida na si lazima uumwe ndiyo ukitumie, kwani  huongeza nguvu za mwili kwa kuujaza virutubisho, madini, vitamini na tindikali muhimu ikiwamo ya ‘amino acids’ zinazomfanya binadamu aondokewe na sonona ambazo kila mgonjwa huwa nazo anapougua.  Lakini pia chakula hiki kimetengenezwa mahususi kwa ajili ya kumpatia mgonjwa uzito, nguvu na huusaidia mwili kufanya kazi zake sawasawa ikiwamo umeng’enyaji wa chakula unaoweza kumfanya mgonjwa apate choo sawasawa ili atoe sumu za mwili.

Kukosa choo ni tatizo kubwa kwa wagonjwa wengi hasa waliopooza, wenye saratani na maradhi mengine yanayowalaza wagonjwa vitandani kwa muda mrefu.

Chakula hicho pia kitaweza kuupatia mwili kila hitaji kwa kuwa mchanganyiko wake hujumuisha kiasi kikubwa cha nishati, protini, Omega-3, fatty acids, lakini pia kina viwango vikubwa vya vitamin A, vitamin B1, Vitamin B2 vitamin B3, na vitamin B6 huku kikiwa na vizalishi vya vitamin D na virutubisho vingine.

Kitu cha ziada

Unapokuwa na mgonjwa ambaye tayari ametumia chakula hicho na ameanza kupata nguvu na hamu ya kula, ni vema ukaanza sasa kumuuliza chakula anachokipenda na umpe kama anavyohitaji.

Ieleweke kuwa mdomo wa binadamu hutamani aina ya chakula ambacho kina virutubisho vinavyohitajika mwilini na kwa mujibu wa madaktari wa lishe duniani kote chakula, aina ya dawa ziitwazo ‘Over the counter medicines’ ambazo binadamu huandikiwa na akili yake badala ya daktari ambaye kwa kawaida humuandikia mgonjwa dawa ziitwazo ‘Conventional Medicines’ ambazo mtu hatakiwi kutumia hovyo. Hapo utagundua kuwa ni muhimu kumsikiliza mgonjwa anapenda kula chakula gani kwani huenda kuna dawa ambazo mwili wake unazihitaji kupitia vyakula hivyo.

Matumizi yake

Matumizi ya chakula hicho hutofautiana kati ya bidhaa moja na nyingine. Kwani kila kampuni hutengeneza vyakula hivyo kwa mchanganyiko tofauti.

Zipo aina ambazo unashauriwa kutumia vijiko viwili, nyingine vitatu, vinne na kuendelea. Ila kampuni karibu zote huweka kijiko maalumu ndani ya mkebe wa chakula hicho kama kipimo na unashauriwa kujaza na kufuta inayozidi juu ili kupata kipimo sahihi.  

Unga huo unaweza kuuchanganya na maji ya baridi, ya uvuguvugu, au na juisi na maziwa. Ukishakoroga unampatia mgonjwa ambaye atakunywa glasi moja kwa siku hivyo hata kama hawezi kula kabisa unatakiwa uwe unampa kijiko kimoja-kimoja taratibu ili asitapike na baada ya siku 5 ataweza kunywa glasi hiyo kwa muda mfupi zaidi mpaka akifika siku 10 ataweza kushika mwenyewe glasi na kunywa yote bila tatizo na hapo tayari atakuwa ameanza kupona.

Dk John haule ni mtaalamu wa tiba lishe  +255 768 215 956