Viongozi Serengeti mliomba mkapewa, sasa mtekeleze

Muktasari:

Na mara nyingi viongozi wa ngazi za juu wakiwamo mawaziri wanapozitembelea wilaya au hata mikoa, taarifa wanazosomewa huambatana na maombi mbalimbali kulingana na mahitaji ya sehemu husika.

Aombaye hupewa hayo ni maneno yaliyozoeleka masikioni mwa wengi na nukuu hiyo imo hata katika maandiko Matakatifu ya Biblia.

Na mara nyingi viongozi wa ngazi za juu wakiwamo mawaziri wanapozitembelea wilaya au hata mikoa, taarifa wanazosomewa huambatana na maombi mbalimbali kulingana na mahitaji ya sehemu husika.

Nao wananchi wa maeneo hayo huamini viongozi kwa kufanya vile, wanaweza kupata ufumbuzi wa kero zao papo kwa hapo na nyingine huchukuliwa na viongozi waliombwa kwa ajili ya utekelezaji hapo baadaye.

Kama ilivyofanyika Novemba 29,mwaka jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizindua Mpango wa Ardhi wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, walimpenyezea ombi la kuanzishwa kwa baraza la ardhi na nyumba la wilaya kusudi liwe karibu na wananchi.

Waliofanya hivyo baada ya kuteseka kwa muda mrefu kufuata huduma za kufungua kesi za migogoro ya ardhi wilayani Tarime na Musoma wanakotumia gharama kubwa.

Kutokana na uzito huo, Waziri Lukuvi alikubali ombi hilo na aliwapa masharti nafuu kuwa waandae jengo lenye ukumbi wa kusikilizia mashauri na watoe mpiga chapa mmoja na wizara yake itampangia mwenyekiti mmoja kutoka Baraza la Musoma au Tarime ambaye kila mwezi angekuwa anafika kusikiliza mashauri hayo.

Alisema atafanya hivyo hadi hapo ajira za wenyeviti wa mabaraza ya ardhi na nyumba zitakapotoka. Waziri huyo alisema njia hiyo itasaidia kutatua malalamiko mengi na kuwawezesha wananchi kupata haki zao kwa karibu na haraka badala ya kusubiri.

Licha ya Lukuvi kutoa fursa hiyo, inaonekana ombi hilo lilitolewa na viongozi wa Serengeti bila maandalizi.

Kwani sasa ni zaidi ya miezi miwili imepita hakuna utekelezaji na kinachotokea kila kiongozi akija wananchi wanawasilisha malalamiko ya ardhi ambayo mengi yanaangukia kwenye mamlaka ya chombo hicho.

Hii inanipa mashaka kama taarifa zinazoandaliwa huwa zinafanyiwa utafiti kwanza au ndiyo mtu huamua tu kuzungumza ili onekane na wananchi kuwa anawajali kwa kuwasilisha matatizo ya wananchi au ndiyo mtindo wa funika kombe mwanaharamu apite.

Halmashauri kuwasilisha ombi kama hitaji la wananchi la muda mrefu kisha ikasuasua kutafuta jengo kwa kipindi chote hicho na kila kiongozi anayekuja wilayani hapa analakiwa kwa mabango yenye kero ambazo zingetatuliwa na baraza la ardhi, kweli wanajua dhana ya serikali ya Awamu ya Tano iliyojipanga kusikiliza na kuzitatua kero zao?

Binafsi nalitazama hili kwa jicho pana zaidi, ni dhahiri viongozi hawa waliomba kutatuliwa kero hiyo kwa mzaha, hawakuwa na nia, kama walikuwa na nia thabiti ya kuwasaidia wananchi kupata haki zao kwa kufuata sheria, wangeshakuwa wamejenga ama kutafuta jengo hilo kama alivyowaagiza Waziri Lukuvi.

Nachelea kuamini kama kuna siku wananchi hao wa Serengeti watakuja upata haki yao kama viongozi wao utendaji wao wa kazi una kasi ya kinyonga.

Ni kiongozi gani wilayani hapo hajui jinsi uamuzi wa mabaraza ya ardhi ya kata unavyosababisha migogoro ndani ya jamii kutokana na kutoa uamuzi usiozingatia sheria na matokeo yake watu wanamalizana kibabe?.

Ni mara ngapi wananchi wanaposhindwa kwenye mabaraza ya kata kwa kukosa nauli za kwenda Musoma au Tarime huenda ofisi ya mkurugenzi ama mkuu wa wilaya kusaka haki ambayo wangeipata kupitia Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya? Hivi nini kimewaroga kwa kushindwa kutekeleza aliyosema Waziri Lukuvi?.

Kabla ya Waziri Lukuvi kufika wilayani hapa, Makamu wa Rais Samia Suluhu alipofanya ziara yake ya kikazi alijikuta akipokelewa kwa mabango ambayo baadhi yalilalamikia migogoro ya ardhi. Hata Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kigoma Malima alipokuja kujitambulisha, wananchi wachache waliojua walimlaki wakiwa na mabango hayo. Hivi kuna faida gani kuitwa kiongozi wakati hushughulikii kero za wananchi kwa wakati kama anavyosisitiza Rais John Magufuli.

Baada ya Lukuvi alikuja Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa na kulakiwa na mabango lukuki kati ya hayo yakilalamikia umiliki wa ardhi na waliohusika kutoa majibu ni watendaji wa Halmashauri na mengi yalihusisha mtiririko wa vyombo vya uamuzi kwa masuala ya ardhi na nyumba.

Kwa utendaji huo tusubiri Rais John Magufuli siku akifanya ziara wilaya ya Serengeti lazima atapokelewa na mabango yenye kero zile zile ambazo watangulizi wake walipokewa na wengine kama Lukuvi akatoa maelekezo ya nini cha kufanya.

Hivi mnashindwaje kutengeneza sehemu kwa ajili ya huduma muhimu kama hiyo kwa wananchi lakini mnahangaika na mambo mengine ambayo hata yakichelewa hayana madhara makubwa kwa jamii?

Kama mliomba mkapewa mnataka nani aje atekeleze ombi lenu mliloona ni hitaji la msingi kwa wananchi wa wilaya yenu? Acheni hizo, tekelezeni kile mlichoagizwa na waziri ili wananchi wapate huduma jirani.

0787239480.