Vipo vyombo vya usuluhishi wa migogoro ya ardhi kila mahali nchini, vitumie

Thursday December 7 2017Justine Kaleb

Justine Kaleb 

By Justine Kaleb

        Migogoro ya ardhi suala lililopo maeneo mengi nchini. Kutoafikiana, kutoelewana au kutokubaliana kuhusiana na ardhi kumeshaleta mapigano baina ya wakulima na wafugaji.

Migogoro husababishwa na mambo mengi ikiwamo umilikishaji wa watu wawili kwenye eneo moja, uvamizi wa eneo, kuvunjwa kwa mkataba wa mauziano au upangaji hata matumizi mabaya ya eneo yanayoleta madhara kwa majirani.

Pia inaweza kusababishwa na Serikali kuchukua maeneo ya wananchi pasipo kulipa fidia au kulipa fidia isiyostahili au kubadilisha matumizi ya eneo pasipo kuwashirikisha watumiaji wa awali wa eneo hilo na mwekezaji kupewa eneo la kijiji bila wananchi kushirikishwa. Wakati mwingine huweza kuchangiwa na kutoridhishwa na maamuzi ya vyombo vya sheria au dhuluma ya mirathi.

Bila kujali chanzo, zipo mammlaka zinazoshughulika na migogoro ya ardhi. Jambo la msingi kufahamu mgogoro wako unatakiwa upelekwe katika chombo gani kati ya hivyo kwani kutoupeleka mahali sahihi inaweza kukufanya ushindwe au uchelewe kupata haki zako.

Mamlaka hizi zinaanzia ngazi ya kijiji ambako kuna baraza la ardhi la kijiji likifuatiwa na baraza la kata kisha baraza la ardhi na nyumba la wilaya, Mahakama Kuu na hatimaye Mahakama ya Rufaa.

Baraza la ardhi la lina mamlaka ya kupokea malalamiko ya ardhi kutoka kwa wanakijiji na kuitisha mikutano ya kusikiliza migogoro na kusuluhisha migogoro yote iliyopo kwenye eneo lake. Endapo hutaridhika na maamuzi ya baraza hili unaweza kukata rufaa katika baraza la kata.

Baraza la kata linashughulikia migogoro yote ya kata husika. Jukumu lake ni kudumisha amani na utulivu kwa kuzipatanisha na kuzisaidia pande mbili zenye mgogoro kupata suluhisho la pamoja.

Baraza hili lina mamlaka ya kusikiliza kesi za maeneo yenye thamani isiyozidi Shilingi milioni tatu. Katika ngazi hii, wanasheria hawaruhusiwi kuwawakilisha wahusika wa kesi.

Baraza linaweza kutoa amri ya urejesho wa umiliki wa ardhi, utekelezaji wa mkataba, zuio, fidia, gharama, au amri yoyote itakaloona inafaa kwa mujibu wa sheria.

Utekelezaji wa amri inayotolewa na baraza hili ni lazima ufanyike kupitia baraza la ardhi na nyumba la wilaya. Ikiwa hujaridhika na maamuzi yake unaweza kukata rufaa katika baraza la ardhi na nyumba la wilaya ndani ya siku 45 baada ya hukumu.

Baraza la wilaya husikiliza na kutoa hukumu ya migogoro yote ya ardhi iliyopo katika wilaya, mkoa au kanda ya mahali ilipoanzishwa.

Linaweza kusikiliza kesi zote za mali isiyohamishika yenye thamani isiyozidi Sh50 milioni inayohamishika isiyozidi Sh40 milioni. Wanasheria wanaruhusiwa kuwawakilisha wahusika wa kesi.

Baraza hili pia lina mamlaka ya kusikiliza rufaa inayotoka baraza la kata na kutoa amri ya utekelezaji wa hukumu iliyotolewa huko. Maamuzi ya baraza hili yanaweza kutekelezwa na baraza lenyewe au baraza lenye mamlaka sawa au Mahakama Kuu. Ikiwa utakuwa hujaridhika na maamuzi unaweza kukata rufaa katika Mahakama Kuu ndani ya siku 60 baada ya hukumu.

Mahakama Kuu inacho kitengo cha ardhi kilichoanzishwa kwa ajili ya kushughulikia kesi zote za ardhi. Mahakama hii inaongozwa na jaji na ina mamlaka ya kusikiliza kesi za ardhi na nyumba zinazozidi Sh50 milioni kwa mali isiyohamishika na zinazozidi Sh40 milioni kwa mali inayohamishika.

Katika hatua hii pia mwanasheria anahitajika kwa ajili ya ushauri na uandaaji wa nyaraka mbalimbali za kesi ikiwa ni pamoja na kuisimamia kwa ujumla. Mahakama hii pia ina mamlaka ya kusikiliza kesi mbalimbali za ardhi zinazoihusu Serikali na rufaa kutoka mabaraza ya wilaya.

Hata hivyo kwa sasa Mahakama Kuu inao uwezo wa kusilikiliza kesi za ardhi licha ya kuwapo kwa kitengo hicho maalum cha ardhi. Endapo hujaridhika na uamuzi ya Mahakama Kuu unaweza kukata rufaa Mahakama ya Rufaa baada ya kupata kibali cha Mahakama Kuu.

Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ina mamlaka ya kupokea kesi zote zinazotoka Mahakama Kuu kitengo cha ardhi pamoja na mahakama kuu nyingine yoyote; bara na visiwani.

Mahakama hii ina mamlaka ya mwisho ya uamuzi wa kimahakama katika utoaji haki nchini. Huwezi kufungua kesi mpya mahakama ya rufaa, isipokuwa unaruhusiwa kukata rufaa au kuomba marejeo ya uamuzi baada ya kutoridhishwa.

Hakikisha unafahamu mamlaka ya kila chombo ili usipoteze haki zako na ardhi wakati vyombo vipo.

Mwandishi ni wakili wa kujitegemea. Anapatikana kwa 0755 545 600 au [email protected]     

Advertisement