Virutubisho halisi hutokana na vyakula vinavyotoka baharini

Muktasari:

Jamii nyingi huamini vyakula vya baharini, mito na maziwa vina faida kuliko vinavyopatikana nchi kavu

Tangu zama za mfumo wa ujima hadi leo, binadamu wamekuwa wakivuna mazao ya baharini, kwenye mito, maziwa na madimbwi kwa ajili ya chakula. Viumbe vya majini kama vile baadhi ya wanyama na mimea, ni miongoni mwa vile ambavyo binadamu wameendelea kuvivuna kutoka katika mazingira ya asili na kuvitumia vikiwa katika hali yake ya asili.

Maji ya bahari, maziwa na mito, ni chanzo kizuri kinachotupatia nyama, minofu ya samaki na mbogamboga za mimea ya baharini kama vile mwani.

Mwani ni magugu bahari yanayotumika kama chakula na dawa kwa ajili ya kutibu maradhi mbalimbali ya binadamu. Sehemu mbalimbali duniani, mwani hutumika kutengeneza supu na aina mbalimbali za saladi. Mwani pia hutumiwa kwa ajili ya kuzuia na kutibu tatizo la upungufu wa damu kutokana na ukweli kuwa, una asidi ya folate pamoja na rangi ya kijani inayojulikana kama chlorophyll ambavyo husaidia kuongeza damu na kutibu matatizo ya upungufu wa damu mwilini.

Kwa muda mrefu wanasayansi wamekuwa wakifanya utafiti mbalimbali kubaini faida za mazao ya bahari na maji mengine kuhusiana na afya ya binadamu. Ushahidi mwingi wa kisayansi unaonyesha kuwa, vyakula vinavyotoka majini huzuia uvimbe wa tezi shingo, hutupatia madini mbalimbali kama vile madini joto, madini chuma, calcium, magnesium, copper, zinc na aina mbalimbali za vitamini kama vile vitamini A, B-12, C, D, E na K.

Vyakula hivi pia hutupatia mafuta mazuri ya aina ya omega-3, ambayo ni mazuri kwa afya na utendaji wa moyo, ini na ubongo.

Wataalamu wa sayansi za lishe pia wanabainisha kuwa, vyakula hivi hupunguza kiasi cha mafuta mabaya mwilini, husaidia kupunguza unene na kupunguza hatari ya kupata maradhi ya moyo, kiharusi, kisukari, mafua yatokanayo na mzio pamoja na saratani.

Katika utafiti wake uliochapishwa mwaka 2013 katika jarida liitwalo Journal of Applied Phycology toleo namba 25(3), Dk Jane Teas, anadai kuwa, mbogamboga zinazotokana na mazao ya baharini zina kiasi kikubwa cha viinilishe aina ya lignans ambavyo husaidia kudhibiti homoni za oestrogen zinazoweza kuchochea kutokea kwa tatizo la saratani ya matiti.

Anaongeza kusema kwamba utumiaji wa mboga hizi kwa wingi, kinaweza kuwa ndicho kigezo cha kuwa na kiwango cha chini cha tatizo la saratani ya matiti nchini Japan.

Mazao ya baharini pia huimarisha afya ya mifupa, neva, macho na utendaji mzuri wa akili. Mbali na faida hizo, wataalamu wanaamini kuwa moja ya siri ya watu wa zamani kuishi maisha marefu, ni matumizi ya vyakula vya asili vilivyotokana na mazao yaliyovunwa kutoka majini.

Katika utafiti uliofanyika huko Okinawa kwa muda wa miaka 25 ukiwahusisha watu walioishi maisha marefu, ulionyesha kuwa mbogamboga za baharini zilikuwa ni miongoni mwa sehemu 7 hadi 10 za mboga na matunda waliyokuwa wanakula kila siku. Okinawa ni sehemu ambayo watu wengi wanaishi maisha marefu ambayo hufikia miaka 100 na zaidi.

Mtafiti aliyebobea katika sayansi ya bahari upande wa bayolojia ya masuala ya mwani kutoka Taasisi ya Sayansi za Mazao ya Baharini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyoko Zanzibar, Dk Flower Ezekiel Msuya, anasema kuwa mwani una faida nyingi mwilini kwa sababu una vitamini mbalimbali na virutubisho ambavyo husaidia kutibu ugonjwa wa tezi ya shingo, matatizo ya tumbo na ugonjwa wa ngozi.

Mafuta ya samaki na mbogamboga za baharini, hutumika kama malighafi za kutengeneza bidhaa za mafuta ya kupakaa mwilini aina ya losheni na vipodozi vya kutunza afya ya ngozi.

Mbali na kusheheni virutubisho, vyakula vyenye asili ya majini vina dawalishe ambazo husaidia mwili kupambana na vimelea vinavyosababisha magonjwa kama vile virusi na bakteria wa aina mbalimbali. Vyakula hivi pia husaidia mwili usipate maradhi yanayotokana na uvimbejoto pamoja na mchochota.

Katika utafiti uliofanywa na wataalamu waliobobea katika maswala ya sayansi za vyakula na Teknolojia kutoka katika Chuo Kikuu cha Peradeniya nchini Sri Lanka na kuchapishwa mwaka 2011 katika Jarida la ‘Advances in Food and Nutrition Research’ toleo namba 64, ilibainika kuwa vyakula vinavyotokana na mbogamboga za mimea ya baharini, mbali na kusheheni virutubisho, pia vina nyuzilishe muhimu kwa ajili ya utendaji mzuri wa mfumo wa chakula.

Dk George Pamplona-Roger ambaye ni bingwa wa upasuaji katika mfumo wa chakula, katika kitabu chake kiitwacho ‘Ecyclopedia of Foods and Their Healing Power’, anasema kwamba vyakula vinavyotokana na mbogamboga za mazao ya bahari husaidia mtu ashibe kwa muda mrefu na kupunguza hamu ya kutaka kula mara kwa mara.

“Hali hii hukifanya chakula hiki kuwa na manufaa sana katika mlo wa watu wanaotaka kupunguza uzito wa mwili,” anasema Dk Pamplona-Roger.

Pia chakula hiki hufyonza tindikali za tumboni na kupunguza kiungulia. Mbali na faida hizo, chakula hiki, hulainisha kinyesi na kufanya mtu ajisaidie vizuri bila kutumia nguvu nyingi za kusukuma au bila kupata maumivu wakati wa haja kubwa.

Tafiti kadhaa pia zinaonyesha kuwa chakula hiki huimarisha afya ya ngozi laini inayofunika sehemu ya ndani ya njia ya mfumo wa chakula na kuongeza idadi ya bakteria rafiki wanaoishi tumboni ambao wanaosaidia mtu kuwa na afya njema.

 

Tahadhari

Mbali na faida lukuki za afya na maisha marefu zinazotokana na vyakula tunavyovuna kutoka majini, wataalamu wanatahadharisha kuwa vyakula hivi vinaweza kusababisha madhara ya kiafya pale maji yanapochafuliwa na kinyesi cha binadamu pamoja na majitaka ya viwandani yenye kemikali hatari kama vile zebaki na dioxine.

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa miji mingi iliyoko pwani au karibu na mito mikubwa, hutiririsha maji taka yenye virusi na bakteria hatari kama salmonella kwenye maji ambayo ni makazi ya samaki na viumbe vingine vinavyoliwa na binadamu.

Tafiti hizi zinabainisha zaidi kuwa, vimelea hatari kama virusi ndani ya maji machafu yanayochafua mazalia ya samaki, vinaweza kusafiri na kufika umbali wa kilometa tano kutoka sehemu ambayo maji taka yameingizwa ziwani au baharini.

Vyakula hivi pia vinaweza kuwa hatari kutokana na uvuvi haramu wa kutumia sumu, mabomu au dawa za mimea zinazotumika mashambani wakati wa kilimo zinaposombwa wakati wa mvua kuelekea kwenye maji.

Matatizo mengine yanaweza kutokea kwa sababu ya vyakula hivi kuhifadhiwa kwa dawa zisizokubalika kiafya, chumvi nyingi au kukaushwa kwa moshi unaozalishwa na malighafi zenye sumu.

Katika utafiti mmoja uliofanyiwa mwaka 1997 na watafiti wa Chuo Kikuu cha Tiba ya Mifugo cha Saint Hyacinthe kilichoko Quebec huko Canada na kuchapishwa katika Jarida la ‘Preventive Veterinary Medicine’ ilibainika kuwa, tatizo jingine ambalo ni kubwa kutokana na chakula kinachovunwa majini, ni magonjwa ya samaki yanayotokana na uhifadhi mbaya wa mito, maziwa na bahari.

Ili kupata faida za kiafya na za kiuchumi zinazotokana na mazao ya baharini, maziwa na mito, jamii haina budi kutunza mazingira na kuzuia uchafuzi wa maji kwa kadri inavyowezekana.

Mamlaka za usimamizi wa afya na ubora wa mazingira pamoja na mamlaka za afya ya jamii, chakula na dawa, hazina budi kuwa makini zaidi kwa ajili ya maendeleo ya afya ya jamii kwa kusimamia uhifadhi endelevu maji na usalama wa vyakula vinavyovunwa majini.