Viwanda kufungwa kwa uhaba wa sukari ni aibu

Muktasari:

Murad pia alisema kuna viwanda vingine viko hatarini kufungwa kwa kuwa vimebakiwa na malighafi (sukari) ya kuzalisha kwa kipindi cha wiki moja. Alisema kwa mujibu wa wenye viwanda sukari waliyoiagiza ilifika nchini Desemba mwaka jana na wengine Januari, lakini haijapata kibali cha kutoka bandarini kwenda kwenye viwanda vyao kwa ajili ya uzalishaji.

        Gazeti hili toleo la jana ukurasa wa pili kulikuwa na habari iliyosomeka ‘Viwanda vyafungwa kwa uhaba wa sukari’. Habari hiyo ilimnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Sadiq Murad akisema baadhi ya viwanda vya vinywaji baridi vimefungwa kutokana na uhaba wa sukari ya uzalishaji.

Murad pia alisema kuna viwanda vingine viko hatarini kufungwa kwa kuwa vimebakiwa na malighafi (sukari) ya kuzalisha kwa kipindi cha wiki moja. Alisema kwa mujibu wa wenye viwanda sukari waliyoiagiza ilifika nchini Desemba mwaka jana na wengine Januari, lakini haijapata kibali cha kutoka bandarini kwenda kwenye viwanda vyao kwa ajili ya uzalishaji.

Hata hivyo, Murad alisema waliambiwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kwamba vibali vya sukari hutolewa na Shirika la Sukari Tanzania (Sudeco) lililopo chini ya Wizara ya Kilimo na anayetoa ruhusa ya vibali kwa msingi wa misamaha ya kodi ni Wizara ya Fedha na Mipango.

Tunachokiona hapa suala hili halikupaswa kufika kwenye Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Kwa hali iliyofikia sasa suala hili linaonekana kukuzwa pasina sababu za msingi na wala halipaswi kugeuka kaa la moto kwa wahusika kujiweka kando.

Utaratibu wa uagizaji sukari nje haukuanza leo wala jana, wizara tatu zilizotajwa kila moja ina nafasi yake katika kukamilisha taratibu za uingiaji wa sukari nchini. Hivyo, hatuoni sababu za viwanda kufungwa au kukaribia kufungwa kwa kuwa kuna uchelewaji wa kuiondoa bandarini.

Tunaamini wahusika kabla ya kufikisha malalamiko yao mbele ya Kamati ya Bunge walitoa taarifa kwa wahusika katika wizara hizo, tunaamini pengine kuchelewa kupata majibu ya hoja zao ndiko kumewasukuma kuieleza kamati hiyo.

Pia, wakati wazalishaji hawa wakilalamika uhaba wa sukari, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali alinukuliwa na Mwananchi akilalamika sukari inayozalishwa visiwani humo kukatazwa kuingia kwenye soko la Tanzania Bara.

Balozi Amina alisema amefikisha malalamiko hayo hadi kwa viongozi wa juu katika Serikali ya Muungano, lakini majibu ya Waziri Mwijage katika hilo yalikuwa hana taarifa hadi awaulize wasaidizi wake. Kauli yetu kwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na zingine zinazohusiana na masuala hayo zibadilike na kuongeza kasi ya kuifanya Tanzania ya Viwanda.

Masuala kama sukari kukwama bandarini au sukari ya Zanzibar kukatazwa kuuzwa katika soko la Tanzania Bara ni masuala ya kiutendaji yanayopaswa kumalizwa na mawaziri husika. Hakuna maana kama mawaziri wa Serikali iwe ya Jamhuri au ya Mapinduzi Zanzibar kushindwa kuzipatia ufumbuzi kero zinazohusu wananchi wao.

Hatuamini kama kero hizi zinasubiri maagizo ya Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.Inafahamika wazi kwamba mawaziri wana mamlaka kamili katika kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake na kama kuna kikwazo wanao uwezo wa kulifikisha kwenye Baraza la Mawaziri au kuonana binafsi na mwenye mamlaka juu yao.

Tunatoa rai kwa mawaziri watekeleze majukumu yao kwa weledi, kero kama hizi za kukwama sukari bandarini hadi viwanda kufungwa au sukari ya Zanzibar kukatazwa kuuzwa Bara, hayapaswi kutokea kwa sasa tunapoelekea Tanzania ya Viwanda. Viwanda kufungwa kwa uhaba wa sukari ni aibu.