Wanachama Yanga wonyeshe umuhimu wao

Muktasari:

  • Inafurahisha, pale unapotaka kuzigusa, wanachama na mashabiki hao wanakuwa wakali kwelikweli, hawataki hata kitu kimoja kubadilishwa.

Simba na Yanga ni moja ya klabu kongwe Tanzania na ndizo zenye wanachama na mashabiki lukuki.

Inafurahisha, pale unapotaka kuzigusa, wanachama na mashabiki hao wanakuwa wakali kwelikweli, hawataki hata kitu kimoja kubadilishwa.

Inafikia hatua wengine kwenda mahakamani kupinga kila aina ya mabadiliko yanayotaka kufanyika.

Hali hiyo imeliamsha pia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambalo limeingilia kati kuhakikisha kuwa hakuna mabadiliko holela yanayofanywa katika klabu hizo.

Wiki iliyopita, kuliibuka madai kwamba wachezaji wa Yanga walikuwa katika mgomo wakidai haki zao na zaidi mishahara. Ilidaiwa kuwa sababu ya mgomo huo ni malimbikizo yao ambayo hawajalipwa kwa muda mrefu wao pamoja na sekretarieti nzima ya klabu hiyo bungwa Tanzania Bara.

Ifahamike kuwa, klabu ya Yanga ni ya wanachama na ndiyo maana wanakuwa wakali kwa kila kunapokuwa na dalili ya mabadiliko ambayo hawayaelewi, lakini cha kushangaza ni kwamba matatizo yanapotokea wanakuwa mbali na klabu.

Hii inaonyesha kuwa wapo miongoni mwao ambao hawatambui dhamana waliyonayo katika klabu hiyo.

Yanga imekuwa katika hali ngumu kifedha hasa baada ya Yusuf Manji kujiweka kando.

Manji ambaye alikuwa mwenyekiti, alikuwa akiisaidia kujikwamua katika maeneo mengi na kuondoka kwake kunailazimu kutafuta njia mbadala ili kusonga mbele.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa aliwahi kutangaza kuwapo kwa hali ngumu ya kifedha Yanga, lakini wanachama wakabaki kimya, hatukuuona uchungu ule wa asilimia 100 ambao tumekuwa tukiushuhudia katika masuala masuala mengine kama ya mabadiliko ya kimfumo.

Wanachama na mashabiki wengi wa Yanga wanaumia inapofanya vibaya na wanakuwa wakali kwelikweli wanachokitaka ni mafanikio tu lakini hawataki kuwa sehemu ya kuhakikisha yanapatikana.

Mashabiki wa Yanga hawataki kuona Yanga ikipoteza michezo yake ya Ligi Kuu, hawataki kuona mambo yanakwenda kombo klabuni wanachotaka mambo yaende wanavyotaka, wafurahi na kuwabeza wenzao wa Simba.

Hayo hayawezi kwenda bila fedha, uendeshaji wa klabu unahitaji gharama, wachezaji wanahitaji mishahara, sekretarieti inahitaji fedha kwa ajili ya kuhudumia mambo mbalimbali, na kwa kuwa klabu ni ya wanachama, wao ndiyo wanaotakiwa kuhakikisha hayo yanatimia. Kwa kuwa mpaka sasa mfumo wa klabu ni ule wa uanachama, basi kila mwenye kadi ajue anao wajibu wa kuisaidia kwa hali na mali. Asikae pembeni tu huku akichekelea au kulalamikia utendaji wa wenzake.

Tunadhani kwamba ipo haja kwa uongozi wa Yanga kuandaa mpango ambao utamfanya kila mwanachama kuwajibika. Njia ya msingi na ya kikatiba ni kuhakikisha kila mmoja anakuwa hai kwa kulipia stahili zake zote kila mwaka.

Hilo likifanywa kwa umakini sambamba na kuhamasisha mashabiki wake kwa mamilioni kuchukua kadi za uanachama, tunaamini kabisa kwamba utegemezi mkubwa klabu hii na hata watani wake Simba utakuwa umepatiwa tiba ya uhakika. Mfano wanachama 1,000,000 kila mmoja akitoka Sh10,000 kwa mwaka zitapatikana Sh10bilioni hizi zinatosha katika kusimamia mambo ya msingi ya klabu na inawezekana kuzipata, ni mipango tu.