Wanariadha oneni fahari kupigania medali kwa mashindano yenu

Muktasari:

  • Wakenya wanachoangalia ni Gor Mahia na AFC Leopards, hapo utawaona angalau wanajiokoteza.

Nchini Kenya, hakuna kitu wanapenda kama riadha. Kwenye soka kidogo, japo nayo ina nafasi yake.

Wakenya wanachoangalia ni Gor Mahia na AFC Leopards, hapo utawaona angalau wanajiokoteza.

Mara kadhaa timu ya taifa, Harambee Stars, huwa wanakuwa nayo lakini inapofanya vizuri, ngoja wachemshe. Hakuna hata mwenye hamu nayo. Hiyo ndiyo hulka ya Wakenya wengi.

Kwa Kenya, ukweli yanapokuja mashindano ya riadha, inafikia hatua wanafanya mchujo kwanza ili kupata watu stahiki, kwa kuwa wanaojitokeza ni wengi.

Si kwa Kenya pekee, hata Uganda hali iko hivyo kwamba mashindano lazima wapatikane wale ambao hasa wanastahiki.

Tunaiona Rwanda, kadhalika wanafanya mashindano ya mchujo kupata timu hasa kwa ajili ya mashindano husika.

Nikiwaangalia Wakenya, ninakumbuka mwaka 2011, wakati Kenya ikijiandaa na mashindano ya dunia ya riadha yaliyofanyika Daegu, Korea Kusini ilikuwa ugomvi kwa wanariadha.

Wanariadha walikuwa wengi wenye sifa, waliandaa mashindano ya mchujo, wapo walioshindwa lakini waligomea wakiamini wakienda kwenye mashindano ya dunia wanaweza kufanya makubwa. Hata hivyo, msimamo ukawekwa na hawakuweza kushiriki mashindano hayo.

Kwa Tanzania sijawahi kusikia hicho kitu, kwamba inafikia hatua ni ugomvi, kila mmoja ana sifa, kila mmoja ameiva sasa mchujo ufanyike vipi.

Sasa, kwa upande mwingine, wapo wale ambao wanafikia hatua fulani, na wanaona kwamba mashindano fulani ni kwa ajili ya levo fulani, lakini kwa Tanzania sijaona wakimbiaji wake kujitokeza kwa wingi japo kuonyesha kuwa wana nia.

Nilitarajia kuona wakimbiaji wa Tanzania wakigombea nafasi ya kushiriki mashindano kama haya ya Kili Marathon kwa kilomita 21 na 42.

Mashindano hayo yamepangwa kufanyika mkoani Kilimanjaro Machi 4.

Hata mikoa, ingeweza kutengeneza wanariadha kwa ajili ya mbio hizo na kusema lazima zawadi ya kwanza hadi ya tano mathalani zibaki Tanzania.

Twende mbele, turudi nyuma, Kili Marathon kwa kilomita 42 au Tigo Kili Marathon kwa kilomita 21, ni mashindano makubwa, lakini wakimbiaji hawayapi nafasi, sio mmoja mmoja na si kwa ngazi ya mikoa.

Ingependeza kuona Watanzania wakichuana kwenye mbio hizo, wakiwatoa jasho wageni.

Inanishangaza kuona wageni wanakuja kuchukua zawadi na kuondoka na Watanzania wanaangalia kuona kama haki yao.

Kwa miaka miwili mfululizo, Tanzania haijafanya vyema ukiacha mwaka 2015 ambao mshindi alikuwa Fabiola William akifuatiwa na Roasline David wa Kenya na mwenzake Joan Cherop, hiyo ni kwa wanawake.

Kwa wanaume mwaka juzi, 2016, Matheka Benard na Muteti Daniel wote wa Kenya, walikuwa wa kwanza na pili na Mtanzania Gallet Ismail akafuatia na Naasi Fabian akawa wa nne.

Nafasi nyingine ni mwaka jana tu hapo, Wakenya, Moses Hengitti, William Koskei na Yangus Katum walitawala kwenye mbio za kilomita 42.

Ukija kwenye Kilomita 21 ambazo siku hizi zinaitwa Tigo Kili Marathon, kwa wanawake na wanaume, angalia nafasi ya Watanzania, sehemu kubwa wanatawala wageni. Labda zile mbio za kilomita tano za fan ran.

Ifike hatua, wakimbiaji wanaotaka kutoka kupitia riadha, kuanza maandalizi mapema na kutumia mbio hizo kama sehemu yao kuonyesha uhodari na uwezo wao katika riadha.

Msione akina Andrew Simbu au Emmanuel Giniki walianzia huku. Sasa wale ambao wanaamini kuwa wanataka kuwa nembo ya Tanzania wanatakiwa kuanza kutengeneza jina hapa.

Lakini kingine, ninashauri, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kuweka utaratibu wa mashindano mengi zaidi kwa mikoa. Kutoa nafasi kwa mikoa na kama vipi kufanya mashindano ya mara kwa mara kwa kanda na baadaye kufanya mashindano ya jumla.

Ni ubunifu tu, ukiacha mashindano ya taifa, kufanya mashindano kwa Kanda za Kaskazini, Ziwa, Kati, Nyanda za Juu na Mashariki.

Mfano, Machi Mashariki mikoa ya Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na Zanzibar. Dar najua kimichezo wilaya zinagawanyika kama mikoa.

Ukienda Ziwa hivyo, Nyanda za Juu Kusini na mwisho zinapatikana ‘cream’ zinakuja kuchuana Dar es Salaam kwa kanda na anapatikana bingwa wa kanda, riadha itachangamka tu Tanzania kuliko kusubiri mashindano ya Taifa au yanaweza kutumika hivyo kupata wakimbiaji bora kwa ngazi ya taifa.

Kikubwa ni ubunifu wa RT na zaidi kuangalia kwamba wana kila sababu ya kuifanya riadha isikike kama ilivyo Kenya na Ethiopia.

Ifike hatua na wanariadha wenyewe wajitokeze wanaposikia mashindano mbalimbali kama haya ya Kili Marathon na pia kuna Rock City Marathon, Karatu Marathon kuliko kusubiri mbio za taifa pekee.

Mikoa itoe sapoti kwa wale wanaotaka kwenda kwenye mashindano hayo kwani watakaposhinda, watabakia kuwa alama ya mkoa na lazima mikoa ione fahari kuwa na wanariadha wazuri ambao wameibuliwa na kuendelezwa.