Wanawake wa Tanzania wanathubutu, wazidi kujengewa uwezo

Muktasari:

  • Lakini lengo lake kuu miaka yote ni kutaka kuonyesha changamoto zinazowakabili wanawake katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa na kujaribu kuziwekea mikakati ya kukabiliana nazo.

Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka ina historia ndefu kimsingi.

Lakini lengo lake kuu miaka yote ni kutaka kuonyesha changamoto zinazowakabili wanawake katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa na kujaribu kuziwekea mikakati ya kukabiliana nazo.

Pia, siku hiyo ambayo inatumika kuonyesha mapambano ya wanawake dhidi ya hali ngumu wanayokutana nayo wanayofanyiwa katika sehemu zao za kazi na kupinga mifumo kandamizi katika familia zao na jamii zinazowazunguka.

Na katika siku hii wanawake na watawala huangalia na kutathimini pia mafanikio na michango mbalimbali ya wanawake inayotolewa kwa jamii kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.

Siku hii huendana na kauli mbiu na mwaka huu inasema ‘Wakati ni huu: wanaharakati wa mjini na vijijini kubadili maisha ya wanawake.’

Kwa hapa nchini naweza kusema siku hii ina maana kubwa sana mwaka huu, kwa sababu wakati wanawake wakiiadhimisha, wanajivunia mafanikio ya kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Pamoja na jitihada za Serikali za kutaka kuhakikisha wanawake wanaboreshewa mazingira ya kufanyia kazi hasa za ujasiriamali, lakini wao binafsi na kupitia katika asasi na vikundi vingi vya ujasiriamali, wameweza kuthubutu kwa imani ya kufikia malengo ya maendeleo waliyojipangia.

Jambo ambalo linawafurahisha wanawake wengi wa Tanzania walioadhimia kwa nia moja kutekeleza maendeleo kwa viendo.

Wengi wao hivi sasa wameamua kuungana na kuwa kitu kimoja kwa sauti moja, wakiwa wamelenga kulinda na kutetea haki zao bila kujali itikadi zao za kisisa wala kidini.

Aliwahi kusema Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mwaka jana kuwa mfumo wa uundaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini, yatawawezesha kufikia malengo ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kama Serikali inavyosisitiza.

Lakini hakuna jambo zuri linaloweza kutekelezwa bila kupitia changamoto, hivyo kunahitajika pia utashi wa kisiasa ili kuhakikisha mwanamke anakwenda sambamba na wanaume katika ujenzi wa uchumi imara kama kauli ya Makamu wa Rais itatafsiriwa vyema. Licha ya kuwa inaweza kuchukua muda mrefu kwa jamii hasa wanaume wa vijijini kuona umuhimu wa kuunga mkono jitihada zifanywazo na mwanamke za kusaka maendeleo, lakini tutafika tu, dalili zimeshaanza kuonekana kama nilivyoeleza hapo juu.

Kwa sababu miaka iliyopita, asilimia kubwa ya watu hawakuona wala hawakuwa na dhamira ya dhati ya kutaka kumshirikisha mwanamke kwenye masuala ya umiliki wa mali, kushiriki katika nafasi za uongozi na za uamuzi wala kazi za maendeleo, lakini kidogokidogo mambo yameanza kwenda.

Kwa sababu awali licha ya kuwapo rasilimali za kutosha, lakini ilichukua miaka mingi kushirikishwa.

Kwa mfano mwaka 2012, takwimu zinaonyesha wanawake pekee nchini walikuwa asilimia 51.3 lakini hata robo yao hawakushirikishwa katika masuala ya maendeleo.

Lakini kupitia asasi, taasisi na wadau wanaopambana kuona mwanamke anapata haki zake za msingi, wamefanya kazi kubwa ya ushawishi na sasa matunda yameanza kuonekana.

Hivyo, nguvu hii ya kumkomboa mwanamke iendane na kauli mbiu ya mwaka huu kwa wanaharakati kuongeza juhudi kwasababu mwanga umeshaanza kuonekana.

Pamoja na kuwapo kwa tofauti kubwa kati ya wanaume na wanawake katika kushiriki nyanja ya uchumi katika maeneo mengi kama lisemavyo Baraza la Dunia la Uchumi (WEF), lakini hiyo isikatishe tamaa, bali mapamabano yaendelee si ya kushikiana bunduki, bali ya kuona Tanzania inasonga mbele kimaendeleo yanayochangiwa na jamii yote. Pia, changamoto zilizopo zitumike kama fursa ya kusonga mbele katika kuwawezesha wanawake nchini.

Kimsingi, kelele nyingi ambazo zimepigwa za kuhitaji usawa na uwezeshaji wa wanawake kwa hapa nchini zimefanikiwa sana.

Nasema hivyo kwa sababu kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanawake kushiriki katika shughuli nyingi za kiuchumi, kisiasa na harakati nyingine.

Awali wanawake wengi walikuwa wakihofia hata kuwania nafasi kubwa za kisiasa kama za kiti cha urais, ubunge na nafasi nyingine za kiutendaji kutokana na hofu ya kutopewa.

Lakini mwaka 2005, mwanamke wa kwanza aliandika historia ya kuwania urais. Alikuwa Dk Anna Senkoro (sasa marehemu) aliwania kupitia chama cha PPT-Maendeleo. Na sasa tunaye Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haya ni maendeleo makubwa ya kujivunia.

Lilian ni mwandishi wa Mwananchi . Anapatikana kwa namba 0713 235309.